Na Beatrice Lyimo- MAELEZO DODOMA
Serikali imepanga kuongeza idadi ya Maafisa Ugani wenye ujuzi katika kila Kata na Kijiji ili kuleta mapinduzi ya kilimo Nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri
wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. William Ole Nasha wakati akijibu swali
lililohusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inafanya mapinduzi ya
kilimo kwa kuwa na wataalamu wa kutosha, leo Bungeni mjini Dodoma.
Naibu Waziri huyo amesema kuwa
Serikali inatambua kuwa Sekta ya Kilimo ni muhimu na ndiyo yenye kuajiri
watanzania wengi hivyo mapinduzi ya kilimo yatachangiwa na uwepo wa
wataalam wa kutosha wenye taaluma na ujuzi stahiki ili waweze kushauri
matumizi ya teknolojia na kanuni bora za kilimo.
” Hadi kufikia mwaka 2016/2017
Serikali imeajiri maafisa ugani 8,756 sawa na asilimia 43 ya mahitaji ya
maafisa ugani 20,374 katika ngazi ya Kijiji, Kata na Wilaya” amefafanua
Naibu Waziri Ole Nasha.
Aidha, Naibu Waziri Ole Nasha
aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha na kuwezesha vituo vya
kilimo na vituo vya Rasilimali za kilimo za kata (WARCs) kwa ajili ya
kufundishia teknolojia mbalimbali za kilimo.
Vilevile alisema kuwa Serikali
itaendelea kutoa ushauri wa kitaalam na kuandaa miongozo na mafunzo ya
huduma za ugani, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi za Ugani
na kuboresha usambazaji wa teknolojia za kilimo bora kwa wakulima
nchini.
Mbali na hayo Serikali inaendelea kusomesha vijana na kuwaajiri kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
0 comments:
Post a Comment