SERIKALI imesema hivi sasa inatoa sh. bilioni 22.2 kila mwezi ili kuboresha elimu ya msingi na sekondari hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana
(Jumamosi, Septemba 2, 2017) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI,
Bw. George Simbachawene wakati akizungumza na wahitimu 166 wa darasa la
saba wa shule ya msingi ya Martin Luther, kwenye sherehe za mahafali ya
10 zilizofanyika shuleni hapo katika Manispaa ya Dodoma.
Waziri Simbachawene ambaye
alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, alisema Serikali itaendelea kuboresha elimu ya sekondari kwa
kuajiri walimu wengi zaidi wa masomo ya sayansi.
“Wazazi wa wanafunzi wanaohitimu
tunawakaribisha kwenye shule za sekondari kwa sababu zote zina walimu wa
kutosha, madawati na vifaa vya kufundishia. Kila mwezi tunatenga sh.
bilioni 22.2 kuendesha shule za msingi na za sekondari hadi kidato cha
nne,” alisema.
Alisema hivi sasa, baadhi ya
shule zinakabiliwa na changamoto ndogo ya upungufu wa walimu wa sayansi
lakini nayo itatuliwa hivi karibuni kwa sababu vibali vya ajira vimeanza
kutolewa.
“Tunaendelea kuziboresha na
tumeshuhudia miaka ya karibuni wanafunzi bora kitaifa wakitoka katika
shule za Serikali ambazo wengi wamezoea kuziita ni shule za kata. Hakuna
shule za kata. Zote ni zimejengwa na Serikali,” alisisitiza.
“Ukienda vyuo vikuu, wanafunzi na ufaulu wa juu wengi wao ni wale waliotoka kwenye shule za Serikali,” aliongeza.
Aliwataka wanafunzi wanaojiandaa
kufanya mitihani yao Septemba 6 na 7, wasiwe na hofu kwani kufanya hivyo
ni chanzo cha kuwafanya wachanganye mambo na kisha kufeli.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
shule hiyo, Bw. Rabbiely Mmanga aliwaasa wazazi na kuwaomba wasiwaingize
watoto kwenye migogoro kwani matendo hayo yanawajisi watoto na
kuwaathiri kisaikolojia hata wawapo shuleni.
“Ninawaomba sana wazazi, tofauti
zenu ziishie chumbani na zisifike masikioni mwa watoto kwa sababu
zinawasumbua kisaikolojia na kuwaharibia concentration yao kimasomo.
Tumewahoji baadhi na wamesema wanaumia kwa kukumbuka adha ambayo mama
anaipata kutoka kwa baba, au baba anaipata kutoka kwa mama,” alisema.
Katika mahafali hayo, wanafunzi
mbalimbali walipewa vyeti kwa kufanya vizuri kwenye masomo mbalimbali
huku Ismail Milambo na Nise-Magreth Malila wakiibuka kidedea kwenye
masomo yote (best academic performers). Tuzo za nidhamu bora
(discipline) zilichukuliwa na Michael Nyalusi na Sayuni Kampuni.
Wanafunzi wengine waliopata tuzo
na masomo yao kwenye mabano ni Ismail Milambo (Hisabati), William Terry
William (Kiingereza), Majaliwa K. Majaliwa (Sayansi), Nise Malira
(Kiswahili), Clinton Dotto (Social Studies) na Justin Kilimali
(Kompyuta).
Wengine walipewa tuzo kwenye vipengele vya michezo, uchoraji na sanaa, usafi, uongozi shuleni, uimbaji na uongozi wa ibada.
Katika risala yao, wanafunzi
wanaohitimu walisema wanaamini misingi ya elimu walioipata kwenye shule
ya Martin luther haitapotea bure na wakaahidi kufanya mitihani yao kwa
umakini ili watoke na ufaulu wa hali ya juu.
Wanafunzi wa darasa la saba kote nchini, wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kitaifa Septemba 6 na 7, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment