Kamanda
wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema hajapelekewa
uthibitisho kuhusiana na maiti za wanaume watatu waliokutwa pembezoni
mwa Bahari ya Hindi eneo la Coco Beach.
Amesema kwamba iwapo atapelekewa udhibitisho huo ni lazima atatolea ufafanuzi suala hilo kiundani zaidi.
Maiti
za watu hao zilikutwa juzi Septemba 24 ambapo mbili zilifungwa kwenye
viroba huku nyingine zikiwa ikiwa imekutwa na jiwe kubwa lililofungwa na
kamba.
“Sijaletewa ‘fact’ nikiletewa nitalitolea ufafanuzi,”amesema Mambosasa.
Wafanyabiashara
wa mihogo wa eneo hilo wamesema wakiwa kwenye biashara zao asubuhi
ghafla waliona maiti moja ikielea karibu na miti aina ya mikoko ikiwa na
jiwe lililofungwa kifuani huku mikono yake ikifungwa na kamba.
Mmoja
wa wafanyabiashara, Aziza Ally amesema baada ya kuona maiti hiyo
walitoa taarifa polisi ambapo walifika saa 4 asubuhi na kuichukua kwenye
gari lao.
Amesema
ilipofika saa 8 mchana waliona maiti mbili kila moja ikiwa kwenye
kiroba zikielea ndipo mmoja wao alipoamua kutoa taarifa polisi baadaye
zikachukuliwa.
"Polisi
walipokuja kuchukua hizi maiti hakuna hata mtu mmoja aliyeruhusiwa
kusogelea na kupiga picha tulishangaa sana kuona ulinzi mkali tofauti
na siku zote na aliyebainika amepiga alipokonywa simu yake," amesema
Ally.
Mfanyabiashara mwingine Issa Isaya amesema cha kushangaza maiti zinazookotwa ni za kiume pekee.
Amesema wanaishi kwa wasiwasi kwasababu kila wiki wanakuta maiti zikiwa zinaelea kwenye maeneo hayo.
0 comments:
Post a Comment