Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Mhe. Selemani Jafo amezitaka
halmashauri zote kukamilisha miradi ya ujenzi wa madarasa, mabweni, vyoo,
maabara, na miundombinu mingine ya shule za msingi na sekondari kabla tarehe 30
Novemba mwaka huu.
Jafo aliyasema hayo leo hii alipokuwa akifanya ukaguzi wa miradi
hiyo katika shule ya Nzasa na Ihumwa zilizopo katika manispaa ya Dodoma.
Mnamo mwezi Juni serikali ilitoa fedha kupitia mpango wa lipa
kwa matokeo (P4R) sh.bilioni 16 kwa ajili ya miundo mbalimbali kwa shule 63 za
sekondari na shule 56 za msingi katika halmashauri mbalimbali ili kuboresha
mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Hata hivyo bado kuna halmashauri chache zinasuasua kukamilisha
ujenzi huo hali iliyomlazimu Naibu Waziri huyo kuagiza halmashauri zote hapa
nchini kukamilisha miradi iliyo pangwa katika maeneo yao kabla tarehe hiyo.
Jafo amesema kwamba hataki kusikia au kuona halmashauri yeyote
ambayo itakuwa haijakamilisha miradi hiyo kwa kipindi kilichopangwa.
“Hatua kali itachukuliwa kwa yeyote atakayefanya uzembe ambao
utasababisha ujenzi huo kutokamilika,”amesema Jafo
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Jafo amelipongeza sana jeshi
la wananchi kutoka kikosi cha Ihumwa kwa kushirikiana na manispaa ya
Dodoma kwa kufanikisha ujenzi katika shule ya Nzasa na Ihumwa na ameviomba
vikosi vingine hapa nchini kuiga mfano huo mzuri ambao umewezesha kukamilisha
miundombinu hiyo kwa gharama ndogo.
Jafo anaendelea na ziara zake za kikazi za kukagua miradi
ya maendeleo katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua
ujenzi wa majengo ya shule Manispaa ya Dodoma
Moja ya nyumba ya walimu iliyojengwa katika shule ya msingi
Nzasa
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa na
wanafunzi wa shule ya msingi Ihumwa alipokuwa akikagua ujenzi wa madarasa na
vyoo
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo
akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule ya msingi Ihumwa.
0 comments:
Post a Comment