Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kujionea ujenzi wa majengo ya mabweni ya wanafunzi katika shule ya sekondari Msalato nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma.
Akiongea wakati wa ziara hiyo na kumkaribisha Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Jafo amesema kwamba agenda kubwa ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ni kubadilisha mandhari ya shule kongwe na kuendelea kuzifanya ziwe bora.
“Sisi tuliopewa dhamana na Mheshimiwa Rais, katika Ofisi yake, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, katika fedha zilizotengwa, katika kusimamia miundo mbinu hii, lakini katika agenda kubwa ya kubadilisha shule hizi kongwe, Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nikuhakikishie tunaifanya kazi hii kwa nguvu zote”
Amesema kuimarika kwa mazingira ya kusomea kumewavutia wanafunzi wengi ambapo katika kipindi cha likizo ni wanafunzi 50 tu ndio watakaokwenda likizo lakini takribani wanafunzi 850 hawatakwenda likizo ili kujisomea shuleni hapo lakini pia amesema Serikali itakuwa na mpango utakaoandaliwa ili kupata wanafunzi bora watakaojiunga na shule maalum za vipaji katika kipindi kifupi kijacho kwani kwa sasa kidato cha tano na sita wamekwisha tumia utaratibu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Jasson Rweikiza ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Vijijini amesema mpango wa kukarati na kujenga majengo ya shule utaboresha mazingira ya kusomea, “kuna mpango wa Serikali ya CCM wa kujenga au kukarabati majengo na miundo mbinu ya shule 88 Tanzania, miundo mbinu hiyo ni pamoja na mabweni, madarasa, mabwalo, maabara, nyumba za walimu, majengo yote ya shule, vyoo na kadhalika”
Mhe. Rweikiza amelishukuru Shirika la nyumba la Taifa(NHC) kwa kujenga majengo yanayokidhi kiwango kinachokubalika na hivyo kazi kubwa ni kwa wanafunzi kujisomea kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Saada Mkuya amesema mazingira ya kusomea tayari ni rafiki kwa wanafunzi bali pia maslahi ya walimu yaangaliwe pia. “Tumeona sasa mazingira ya yamekuwa mazuri mno, kwamba kiasi ambacho kinafanya wanafunzi wao wenyewe wajisikie wapo vizuri lakini pia maslahi ya walimu katika mapato yao yafikiriwe”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Bw. Godwin Kunambi amesema kuwa mazingira ya kusomea yameboreshwa, madawati pia yapo ikiwemo ya ziada, pia Halmashauri ya Manispaa imetoa gari shuleni hapo kwa ajili ya usafiri na hivyo anategemea Manispaa ya Dodoma kuwa miongoni mwa shule bora zitakazotoa wanafunzi wa kumi bora kutoka katika shule hiyo.
0 comments:
Post a Comment