MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu
leo September 4, 2017, imeruhusu mfanyabiashara Yusuf Manji na wenzake
wahojiwe na Jeshi la Polisi ili kukamilisha upelelezi wa kesi ya uhujumu
uchumi inayowakabili.
Ruhusa hiyo imekuja baada ya
upande wa mashitaka kuieleza mahakama hiyo kuwa waliomba hati ya kuwatoa
washitakiwa mahabusu ili kufanyiwa mahojiano katika kesi namba 33/2017
na kwamba polisi wakabidhiwe watuhuiwa hao.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama
hiyo, Huruma Shaidi alisema jana kuwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam (ZCO), alimuandikia barua kuomba washitakiwa wahojiwe na
kusema mahakama imekuwa ikisisitiza kesi za uhujumu uchumi zikamilishwe
upelelezi ili ziweze kusikilizwa.
“Tusingeweza kukataa maombi
hayo kwa sababu tutapingana na kauli yetu ya kukamilisha upelelezi. Ndio
maana tumetoa hati ya kuwatoa mahabusu kwa ajili ya mahojiano. Hii sio
mara ya kwanza kuwatoa washitakiwa kwa upelelezi.”
Aidha, amewataka Polisi kuzingatia
haki za washtakiwa kwa kuhakikisha wana afya njema na wapate uhuru wa
kuwakilishwa na Mawakili wao kwenye jambo lolote na isiwe kificho.
“Namkabidhi Koplo Dotto kama
barua inavyoelekeza kwa kuwa Sajenti Mkombozi ambaye nilitakiwa
kumkabidhi hayupo. Washitakiwa warudishwe muda wa kazi.”
Mbali na Manji, washitakiwa
wengine katika kesi hiyo ni Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality
Group Ltd, Deogratius Kisinda, Mtunza Stoo, Abdallah Sangey na Thobias
Fwere mkazi wa Chanika wanakabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi.
Awali, akiwasilisha maombi hayo,
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa Mahakama
iruhusu washitakiwa waweze kukabidhiwa kwa Polisi ili kutimiza matakwa
ya upelelezi akisema kwa mujibu wa Kifungu cha 59 cha Mwenendo wa Makosa
ya Jinai kinawapa mamlaka Polisi kufanya upelelezi.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa
utetezi, Hudson Ndusyepo alidai Mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa
amri kama ilivyoombwa na upande wa mashtaka kwa sababu shauri hilo
halijapata hati ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kuipa mamlaka
Mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo.
Ndusyepo alidai Mahakama hiyo
imefungwa mikono ya kutoa amri dhidi ya maombi hayo akisema kifungu cha
sheria kilichotajwa kinazungumzia ufanyaji wa upelelezi kwa ujumla.
Wakili Hajra Mungula alidai kuwa
washitakiwa hao wako chini ya ulinzi na kwamba upande wa mashtaka
uliwashitaki huku wakijua kwamba hawajakamilisha upelelezi na wametoa
hati ya kuzuia dhamana.
“Tunaomba ombi hili likataliwe na upande wa mashtaka waelekezwe kuzingatia sheria na haki za washitakiwa.”
Hata hivyo, wakili Kishenyi alidai
Mahakama imekuwa ikisisitiza kukamilisha upelelezi na kwamba
wanachofanya ni sehemu ya kukamilisha upelelezi akisema washtakiwa hao
wana haki ya kuwakilishwa hivyo maombi yao yakubaliwe.
0 comments:
Post a Comment