Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyevaa kofia ya pama)
akisalimiana na baadhi ya Viongozi wanaosimamia Uwanja wa Nangwanda
Mtwara wakati alipofanya ziara kujionea changamoto katika uwanja huo 25
Septemba, 2017 Mkoani Mtwara.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyevaa kofia ya pama)
akiongea na baadhi ya Viongozi wanaosimamia Uwanja wa Nangwanda Mtwara
wakati alipofanya ziara kujionea changamoto katika uwanja huo 25
Septemba, 2017 Mkoani Mtwara.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyevaa kofia ya pama)
akiangalia eneo la uwanja wa mpira wa miguu akiwa na baadhi ya Viongozi
wanaosimamia Uwanja wa Nangwanda Mtwara wakati alipofanya ziara kujionea
changamoto katika uwanja huo 25 Septemba, 2017 Mkoani Mtwara.
PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM
…………………
Na Benedict Liwenga-WHUSM.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kwamba pindi Uwanja wa
Taifa Dar es Salaam utakapokamilia kufanyiwa ukarabati atahakikisha
anapatikana Mkandarasi Mpya mwenye vigezo na ambaye ataleta mabadiliko
hususani katika utoaji tiketi kulingana na namba za viti vilivyopo ndani
ya Uwanja huo.
Kauli hiyo ameitoa jana Mkoani
Mtwara wakati alipotembelea Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Nangwanda ili
kujionea miundombinu ya uwanja huo ikiwemo baadhi ya changamoto
zinazoikabili kiwanja hicho.
Dkt. Mwakyembe ameeleza kwamba,
kumekuwa na changamoto ya kutofahamika idadi kamili ya watu wanaoingia
ndani ya uwanja hali inayopelekea watu kukaa ovyo katika sehemu zisizo
rasmi na wengine kulundikana nje ya uwanja wakati pesa za viingilio
wamelipia ambapo ameweka wazi kuwa hali hiyo inasababishwa na urataibu
mbovu wa utoaji tiketi.
Akiongea na Uongozi wa Uwanja huo
wa Nangwanda Mkoani hapo alisema kwamba, kwakuwa sasa Uwanja wa Taifa
uko katika ukarabati, pindi utakapokamilika Mkandarasi mpya lazima
apatikane ili pindi mtu anunuapo tiketi yake iendane na kiti chake
atakachokaa na sio vinginevyo kwakuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia
kuboresha sura za viwanja nchini.
“Napenda kusisitiza suala hili
kuwa, ntahitaji apatikane Mkandarasi atakaetoa tiketi kulingana na siti
atakayokaa mtazamaji wa mpira, kwasababu kumekuwa na kero kubwa katika
utoaji tiketi hapo mwanzo jambo ambalo halileti sura nzuri kwa jamii”,
alisema Dkt. Mwakyembe.
Aliongeza kuwa Watanzania
hawanabudi kuiga mifano ya nchi nyingine ambazo zimejidhatiti katika
masuala ya utoaji tiketi wakati wa michezo.
Sambamba na hayo, Waziri Mwakyembe
ameupongeza uongozi wa uwanja huo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya
kuutunza uwanja wa Nangwanda huku akiaihidi kuzifikisha changamoto za
uwanja huo katika Viongozi wa Juu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ili
waweze kushirikiana kwa pamoja kuona namna ya kuzitatua.
Uwanja wa Nagwanda ulianzishwa
miaka ya 1980 ambapo awali ulikuwa ukiitwa jina la Uwanja wa Umoja
Mtwara na baadaye kupewa jina la Uwanja wa Nagwanda lililotokana na jina
la mtu maarufu wakati huo.
0 comments:
Post a Comment