METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, September 9, 2017

DC MUWANGO: WAGANGA WA JADI WILAYA YA NACHINGWEA WAJISAJILI ILI WATAMBULIKE



Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi Mhe Rukia Muwango alipokuwa akizungumza na Wanganga wa jadi/Kienyeji
Baadhi ya waganga wa jadi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi Mhe Rukia Muwango


Na Mathias Canal, Lindi

Kama ilivyo katika maeneo mengine nchini, Wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi kuna idadi kubwa ya waganga wa tiba asili (pamoja na waganga wa jadi/kienyeji) wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 120.

Uchunguzi unaonesha kuwa waganga wengi kati ya waganga waliopo nchini hawajasajiliwa kwa mujibu wa Sheria namba 23 ya mwaka 2002 ya Tiba za Asilia na Tiba Mbadala na hivyo wanaendesha shughuli zao kinyume cha taratibu.

Hayo yamesewa na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mhe Rukia Muwango alipokuwa akizungumza na Wanganga wa jadi/Kienyeji kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya kujadili namna bora ya kutambulika kwao na kuwataka kufuata kanuni, sheria na taratibu zilizopo Ikiwa ni pamoja na kusajiliwa katika baraza la waganga wa jadi na tiba asili la Taifa.

Mhe Muwango alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kupitia Mratibu wa waganga wa jadi Awasaidie waganga hao kufuatilia vibali katika wizara ya Afya na ustawi wa jamii ili vitoke kwa wakati.

Pia aliwataka kuwa na umoja wao ambao utakuwa ni chombo cha kurahisisha mawasiliano serikalini na taasisi mbalimbali lakini pia faida ya kuwa na umoja ni kufahamiana na kusaidiana.

Tanzania ni moja ya nchi zilizoridhia kuwepo kwa Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika baada ya mawaziri wa afya wa nchi 46 barani Afrika ambao pia ni wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, kuridhia kuwepo kwa sherehe hizo.

Nia ni kufufua ari na kujenga heshima ya huduma ya Tiba ya Asili
lakini mkazo ukiwa ni kutoa huduma sahihi. Historia inaonesha kwamba tiba za asili zimekuwepo kwa muda mrefu, zimekuwa zikiandikwa kwa maana ya kuonesha umuhimu wake na wakati mwingine kuonesha ubaya wake na hivyo kudharaulika.

Mhe Muwango alisema serikali inaendelea na mikakati ya kuboresha sekta hiyo kwani nchi kama China na India tiba asili kwa maana ya mitishamba imekuwa ikifanyiwa kazi, kuchunguzwa  kitaalamu na kuwekwa katika mfumo wa kisasa wa vidonge ama kwenye vifungashio bora. 

Sambamba na hayo pia amesisitiza zaidi swala la ulinzi na usalama kwani waganga wa jadi inafahamika kuwa wanazo taarifa nyingi za uhalifu hivyo kama wakishirikiana na serikali kuwafichua au kutoa taarifa dhidi ya wahalifu hao  Wilaya ya Nachingwea na Taifa kwa ujumla litakuwa mahala salama na wananchi wake kuendelea kuwa na amani na upendo ulioasisiwa na Hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Serikali ilionesha nia ya kuwa bega kwa bega na wataalamu wa tiba
mbadala na asili baada ya kutunga mwongozo wa utekelezaji wa sera kuhusu tiba ya asili iliyopitishwa mwaka 2000. Mwaka 2002 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisisha sheria namba 23 ya Tiba ya Asili na
tiba Mbadala.

Lakini pia serikali kuridhia uwepo wa siku ya Tiba Asili ambayo
huadhimishwa agosti 31 ya kila mwaka ni kuonesha kuthamini mchango wa tiba hizi. 

Kwa mara ya kwanza maadhimisho ya siku hii yalifanyika mwaka 2003 wilayani Temeke, Dar es Salaam yakilenga katika kuhamasisha uendelezaji na uboreshaji wa huduma ya tiba asili nchini na Afrika kwa ujumla.

“Wataalamu waliokwenda darasani wanashindwa kupata dawa ya Ukimwi leo mtu anaibuka eti ana dawa ya kuuponya. Matokeo yake inakuwa ni wagonjwa kuacha kutumia ARV na wanapokuja kurudi hospitali wanakuwa wameshaharibikiwa zaidi na hatimaye wanapoteza maisha.” Alisema Mhe Muwango
   
Alisema kuwa Ni vizuri pia waganga hao wakawa wanashauriana juu ya wale wanaowadanganya watu wanaoishi na VVU kuwa watawaponya kwa dawa zao.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com