WAZIRI
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe
amewataka wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kutumia fursa waliyoipata
ya usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri chini ya
miaka mitano kufanya hivyo kwa maslahi ya watoto na taifa.
Dkt. Mwakyembe alisema hayo wakati akizundua mpango huo wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara.
Alisema
uandikishaji wa watoto utasaidia kuwa na rekodi sahihi ya idadi ya
vizazi na vifo ambapo inasaidia serikali katika kuangalia mipango yake
na mahitaji ya wananchi katika masuala ya afya, jamii na uchumi.
Aidha
vyeti vinavyopatikana pamoja na kuonesha utambuzi wa mtoto, pia
vinamsaidia kumpatia haki zake nyingine kwa mujibu wa sheria.
Akihutubia
katika uzinduzi wa kampeni hiyo ambayo kauli mbiu yake ni Mtoto
anastahili cheti za kuzaliwa, mpe haki yake ya kuzaliwa, Waziri
Mwakyembe alisema kwamba kampeni hiyo kwa mikoa ya Mtwara na Lindi
inatarajia kuwanufaisha watoto zaidi ya 290,000 wenye umri chini ya
miaka mitano.
Akihutubia
kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba John Aidan
Mwaluko Kabudi ambaye shughuli hiyo iko katika mkono ya ofisi yake
alisema kwamba wananchi wa Lindi na Mtwara walikuwa nyuma katika usajili
kama walivyokuwa watu wa Njombe na kutumaini watafanya vyema kama
wananchi wenzao walivyofanya.
Wananchi
wa Njombe kabla ya kampeni walikuwa wameandikisha kwa asilimia 8.9 toka
Uhuru upatikane lakini baada ya kuanza kwa kampeni katika kipindi cha
miezi mitatu wamefikia asilimia 99.
Kampeni
ya kuandikisha vyeti watoto chini ya miaka mitano imelenga kuondoa kero
za uandikishaji na kuweka sawa mfumo wa uandikishaji wa vizazi na vifo
hivyo kusaidia mipango ya serikali kwa kuwa na takwimu halisi na hivyo
kupanga maendeleo halisi.
Mpango
huo uliozinduliwa jana unafikisha huduma ya usajili karibu na wananchi
kwa kuanzisha vituo vya usajili katika vituo vya afya ambavyo pia ndio
vinavyosaidia elimu ya afya ya uzazi, kiliniki na uzazi.
Pia
vituo hivyo vya usajili vitakuwepo katika ofisi za kata, ikiwa ni sehemu
ya utekelezaji wa sera ya taifa ya ugatuaji madaraka.
Kueplekewa
kwa vituo hivyo katika mtindo huo kutawafanya wazazi kuwa na vituo 7809
vya kuandikisha watoto ukilinganisha na vituo kumi vilivyokuwepo awali.
Pia imeelezwa kuwa kutakuwa na watendaji 1,500 waliofunzwa namna ya kuandikisha vyeti.
Pia ili kufanikisha zoezi hilo serikali imeondoa ada ya usajili kwa watoto wa miaka chini ya mitano.
Uandikishaji huo utatumia teknolojia ya simu na hivyo kuwa rafiki zake katika ukusanyaji wa takwimu.
Kaimu
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA),
Bibi Emmy Hudson amesema kwamba mfumo unaotumika sasa utachagiza
uandikishaji wa watoto na kuwapatia vyeti vyao vya kuzaliwa baada ya
shughuli hiyo kusuasua kwa muda mrefu.
“Tunafanya mabadiliko makubwa katika mfumo ili iwe rahisi kwa watoto na familia zao kupata vyeti vya kuzaliwa,” anasema Hudson.
Aidha
alisema kwamba mfumo huo mpya wa uandikishaji umesaidia maelfu ya
wazazi kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wao katika maeneo ambayo
tayari unafanyakazi.
Pia
alishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto la UNICEF,
Kampuni ya simu ya mkononi ya Tigo na Serikali ya Canada kwa kutoa
mchango mkubwa katika kufanikisha mfumo huo mpya wa uandikishaji.
Mwakilishi
wa UNICEF nchini Tanzania Bi Maniza Zaman alisema kwamba kila mtoto ana
haki ya kuandikishwa na kupewa cheti chake cha kuzaliwa. Alisisitiza
kwamba cheti za kuzaliwa ni rekodi sahihi ambayo mtoto anahitaji wakati
akizaliwa.
Alisema
kampeni ya sasa itawaingiza katika rekodi mamilioni ya watoto ambao
hawaonekani na hivyo kusaidia watoto kupata haki zao.
Pamoja
na watoto kupata haki zao, serikali pia inakuwa na uwezo wa kutambua
idadi ya watoto na kuweka mipango madhubuti ya kuwainua.
Uzinduzi wa mpango huo kwa mikoa ya Mtwara na Lindi unaongeza zaidi idadi ya mikoa ambayo imefikiwa.
Mikoa
ya Lindi na Mtwara inaingia katika mikoa 7 ambayo tayari imefikiwa
tangu mpango huo uanze mwaka 2012 kwa msaada wa fedha za serikali ya
Canada. Mikoa hiyo ni Geita, Shinyanga, Mbeya, Songwe, Mwanza, Iringa na
Njombe.Unadikishaji watoto katika mikoa hiyo tayari umefikia milioni
1.64 walio chini ya miaka mitano.
Balozi wa Canada nchini Ian
Myles akizungumza kwa niaba ya serikali ya nchi yake amesema kwamba
itaendelea kufadhili mpango huo kutokana na wao kuamini katika haki za
mtoto ikiwamo upatikanaji wa cheti chake cha kuzaliwa na takwimu
kusaidia serikali kutekeleza wajibu wake kwa watoto ikiwamo masuala ya
afya na elimu.
Fedha zilizotolewa zimelenga kusaidia kuandikisha watoto milioni 3.5 chini ya umri wa miaka mitano.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Tigo, Simon Karikari alisema kampuni yake imeunga mkono shughuli hiyo
kwa kutambua umuhimu wake na pia katika matumizi ya teknolojia
kurahisisha maisha ya wananchi.
Alisema Tigo inatoa mchango wake kwa kuweka aplikesheni inayotakiwa ambayo inatendakazi kwa haraka na ukamilifu.
Sensa ya watu na makazi ya mwaka
2012 inaonesha kwamba ni asilimia 13 tu ya watoto chini ya miaka mine
wana vyeti vya kuzaliwa huku Tanzania Bara ikiwa chini ya asilimia 12.
Wakizungumza katika uzinduzi huo wananchi wameelezea kufurahishwa kwao kwa kusogezewa huduma karibu ili waweze kuitumia.
Zuwena Abdallah Mawazo ambaye
alifika na mtoto wake alisema amefurahishwa sana na serikali kuleta
huduma hiyo ambayo amesema imeondolewa usumbufu wa njoo leo nenda kesho.
Alisema kwamba hatua walioifanya
serikali ni ya muhimu kwani hataki mtoto wake kuja kusumbuka baadae
kutafuta huduma mbalimbali kwa kutokuwa na cheti cha kuzaliwa.
Aidha alisema kwamba
amefurahishwa na kuondolewa kwa tozo na kutaka wazazi wenzake
kuwafikisha watoto ili wapatiwe vyeti vya kuzaliwa.
Mkazi mwingine wa Tandahimba
ambaye alijitambulisha kwa jina la maarufu Fumao Kavahana alisema kwamba
amefika kumwandikisha mtoto wake wa miaka miwili ili kuondokana na
usumbufu wa baadae.
Aidha alisema kwamba amefika
pale na mtoto wake huyo kwa kuwa yeye na mzazi mwenzake wametengana
lakini alimfikishia mtoto ili ampeleke kuandikishwa wakati yeye akienda
kumsaidia baba yake kulima Korosho Manyanga.
Fumao mwenye umri wa miaka 36
alisema kwamba alikuwa na mtoto mwingine wa miaka 11 ambaye
hajamwandikisha na kwamba anatarajia kuchukua hatua hapo baadae za
kumwandikisha.
Aidha alitoa wito kwa wanaume wenzake kuhimiza watoto waandikishwe na kuwasaidia wanawake kazi hiyo kwa kuwa watoto ni wawote.
0 comments:
Post a Comment