Na Mwandishi Wetu-MAELEZO
DAR ES SALAAM,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Mwigulu Nchemba kesho ataongoza mkutano wa siku moja utakaozungumzia
suala la wakimbizi raia wa Burundi ikiwemo maandalizi ya kuwarejesha
kwao wakimbizi raia wa nchi hiyo waliojiandikisha kwa hiari kurejea
nyumbani.
Mkutano huo utakaofanyika katika
kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere Jijini Dar es
Salaam utahudhuriwa na nchi za Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia wakimbizi (UNHCR).
Mkutano huo unafanyika kwa mujibu
wa matakwa ya Sheria za kimataifa zinazohusu wakimbizi ambazo
zinazilazimu pande tatu katika suala hilo kukutana na kukubaliana kuhusu
namna ya kuwarejesha wakimbizi hao waliohiari kurejea nyumbani.
Katika mnasaba huo, makubaliano ya
mkutano huo yataipa fursa kwa upande mmoja Serikali ya Burundi kuingia
katika makambi ya wakimbizi kuhamasisha kurejea nyumbani na kwa upande
wa pili yatawapa fursa wakimbizi kupitia wawakilishi wao kutembelea
Burundi kuangalia hali halisi ili kujiridhisha kabla ya kurudi nchini
humo.
Baada ya hatua hizo kukamilika,
imeelezwa kuwa Jumuiya ya Kimataifa itatekeleza jukumu lake la
kuwarudisha wakimbizi hao nyumbani kwa ‘heshima’ ambapo chini ya
utaratibu huo wa ‘heshima’, Jumuiya hiyo itapaswa kuwawezesha wakimbizi
hao kuanza maisha mara wanaporejea ikiwemo huduma za chakula na makaazi
kwa wale ambao makaazi yao yatakuwa yameathirika.
Mkutano huo ambao umetanguliwa na
kikao cha siku mbili cha maandalizi, unawashirikisha wajumbe wa nchi
hizo katika ngazi za mawaziri, wakuu wa mikoa ambayo inahusika na
wakimbizi katika nchi hizo na mwakilishi mkaazi wa shirika la UNHCR.
Mkuu wa Mkoa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga ameieleza MAELEZO
kwa njia ya simu kuwa hadi tarehe 29 mwezi huu, tayari wakimbizi raia
wa Burundi 11,826 walikuwa wameshajiandikisha wakisubiri kurudishwa
nyumbani.
Kumekuwepo na juhudi za
kuwahamasisha wakimbizi wa nchi hiyo kurudi nyumbani tangu Rais John
Pombe Magufuli na Rais Pierre Nkurunziza walipotoa wito kwa wakimbizi
hao kurudi nyumbani wakati wa ziara ya viongozi hao huko wilayani Ngara,
Mkoa Kagera mapema mwezi uliopita.
“Tumekuwa tukiwahimiza kurejea
nyumbani kwa kuwa hali sasa ni shwari na hivi karibuni Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba alitembelea makambi kupigia chapuo wito
wa Marais wetu”anaeleza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Brigedia Jenerali Mstaafu Maganga
anaeleza kuwa wengi wa wakimbizi waliojiandikisha wangependa zoezi la
kuwarejesha nyumbani linaharakishwe kwa kuwa wanataka kuwahi msimu wa
kilimo nchini Burundi.
Mkutano huo unafanyika huku kukiwa
na taarifa za Shirika la Chakula (WFP) kupunguza mgao wa chakula kwa
wakimbizi kutokana na shirika hilo kukumbwa na ukosefu wa fedha.
Kuhusu taarifa hiyo ya WFP, Mkuu
wa Mkoa Kigoma anaeleza kuwa hali hiyo si nzuri na inaweza kusababisha
sintofahamu kati ya wakimbizi na wenyeji wao kwa kuwa wakimbizi hao
wanapokosa chakula wanalazimika kutoka na kuvamia mashamba ya wananchi
kukidhi mahitaji yao.
“Hali hiyo si nzuri, wanapopunguza
‘ration’ hicho kilichopungua ni lazima wakitafute na hawana pengine
hivyo wanavamia kwa makundi mashamba ya wenyeji na kusababisha vurugu”
alieleza Mkuu wa Mkoa.
Tangu wiki iliyopita mashirika ya
habari ya kitaifa pamoja na vyombo vya habari humu nchini vimekuwa
nikiripoti taarifa ya Shirika la Chakula la WFP kupunguza kiwango cha
chakula kwa wakimbizi kulikosababishwa na shirika hilo kukumbwa na
ukosefu wa fedha.
Kwa mujibu wa taarifa hizo Shirika
hilo ambalo linahitaji zaidi dola milioni 23 limetoa wito kwa washirika
na wadau mbalimbali kusaidia kutatua tatizo hilo ambalo limewaathiri
pia wakimbizi walio katika nchi nyingine barani Afrika.
0 comments:
Post a Comment