METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, August 11, 2017

Uhuru Kenyatta atangazwa mshindi, Raila Odinga apinga

media
Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto baada ya kupokea vyeti vya ushindi Agosti 11 2017

Tume ya Uchaguzi nchini Kenya imemtangaza rais Uhuru Kenyatta kama mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa urais uliofanyika siku ya Jumanne wiki hii.

Baada ya kuhakiki upya kwa fomu zinazoonesha matokeo zilizopewa jina la 34 A na 34 B kutoka maeneo bunge na vituo vya kupigia kura, Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati amesema rais Kenyatta alipata kura Milioni 8.2 sawa na asilimia 54.2 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Raila Odinga aliyepata kura Milioni 6.7 sawa na asilimia 44.7.

Ushindi huu unamaana kuwa rais Kenyatta alipata asilimia 50 na kura moja, ya jumla ya kura zilizopigwa lakini pia asilimia 25 ya kura zote angalau katika kaunti 24 kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.

Chebukati ameeleza kuwa kati ya wapiga kura zaidi ya Milioni 19 waliojiadikisha kupiga kura, Wakenya takriban Milioni 15 walishiriiki katika Uchaguzi huo.

Baada ya kutangazwa mshindi, rais Kenyatta amewaomba wanasiasa wa upinzani kuungana naye, kuongoza nchi kwa muhula wa pili.
 
"Namwomba Mheshimiwa, Raila Odinga na wafuasi wake waungane nami, tuendeleze nchi yetu pamoja," alisema Kenyatta.

Ushindi wa Kenyatta umekataliwa na muungano wa upinzani NASA na kusema, kura za mgombea wake ziliibiwa na matokeo yalibadilishwa.

Kabla ya kutangazwa kwa mshindi, NASA walikutana na Makamishena wa IEBC na kueleza hoja zao ikiwa ni pamoja na kutaka wadau wote kuruhusiwa kuthathmini mfumo wa tume hiyo.Mes Raila Odinga
Raila Odinga, aliyekuwa mgombea wa NASA akipinga matokeo ya Uchaguzi wa urais

Hata hivyo, Mawakala wa Odinga ambao ni Musalia Mudavadi na James Orengo, wamesema madai yao hayajatatuliwa licha ya kuahidiwa na Tume hiyo mapema Ijumaa mchana.

“Pamoja na kwamba walikubali kushughulikia madai yetu, wamekataa kuyafanyia kazi, tunaodoka hapa Bomas,” amesema Mudavadi.

Katiba ya Kenya inaeleza kuwa, yeyote anayekataa matokeo anaweza kwenda Mahakamani lakini, NASA wameonesha kuwa huenda wasiende kulalamikia matokeo haya.

“Tunawaachia Wakenya waone kilichofanyika, imani yetu ipo kwa wakenya,” amesema Orengo.
Aidha, upinzani umewashtumu waangalizi wa Kimataifa na kusema kauli yao haikuwa sahihi kuhusu Uchaguzi huo.

“Mwangalizi wa Jumuiya ya Madola, rais wa zamani wa Ghana John Mahama, hana uhusiano mzuri na mgombea wetu kwa sababu ni mpinzani wa rais wa sasa Ghana ambaye ni mwandani wa mgombea wetu,” amesema Orengo.

"Hawa waangalizi walikimbilia uamuzi wa kusema kuwa Uchaguzi huu ulikuwa huru na haki, wangehakikiwa kwanza," ameongeza.

Kutangazwa kwa matokeo haya kumewahuzunisha wafuasi wa upinzani huku ikiwa ni furaha kwa wafuasi wa rais Kenyatta.

Hali ni ya wasiwasi katika ngome ya wafuasi wa upinzani hasa mjini Kisumu.

Chanzo:RFI
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com