Na Abdallah Ng’anzi
Kuna nyakati
unatafakari namna mambo yanavyokwenda hasa katika zama za hizi za
kidigitali, moja ya jambo kuu linaloumiza vichwa vya wahitimu wengi ni
ukosefu wa ajira.
Ajira
imekuwa changamoto si kwa Tanzania pekee bali kilio cha ukosefu wa ajira
kinasikika kila kona ya dunia.
Kwa mujibu
wa ripoti ya shirika la kazi duniani (ILO) mwaka 2017 idadi ya watu wasio na
ajira itaongezeka kwa asilimia 5.8 (awali ilikuwa asilimia 5.7) na kufanya
jumla ya watu wasio na ajira kufikia milioni 500.8 duniani.
Hili si
jambo zuri kulisikia likitamkwa kwani ndoto za wasomi wengi ni kujiajiri au
kuajiriwa na kufaidi kile ambacho wamekitafuta kwa zaidi ya miaka 18 wakiwa
darasani.
Zipo sababu
zinawakosesha ajira vijana wengi, miongoni mwa sababu hizo ni ujuzi binafsi wa
mtu ukiachana na vyeti alivyo navyo. Kwa mfano mhitimu akiulizwa mbali na elimu
aliyonayo ni kipi cha ziada alichonacho.
Katika dunia
ya sasa elimu siyo stashahada, shahada au zaidi. Elimu ni namna unavyoweza
kukabiliana na mazingira magumu ya ushindani. Kwa sasa kama Taifa tumeanza soko
la pamoja la Afrika Mashariki, lakini tukiwa kama Taifa tunachanganyika na watu
wa mataifa mengine.
Kuna fursa
nyingi tu zinazoweza kubadilisha maisha yetu zaidi ya kutegemea ajira rasmi.
Mathalani,
mara nyingi watu wanauliza kozi gani inalipa. Ukweli wa mambo ni kuwa kila
kilichopo duniani ukiweza kukitumia vizuri na kwa maarifa kinalipa. Lakini pia
lazima uelewe kuwa milango haipo wazi kana kwamba utaweza kupata kila kitu kama
unavyotarajia, inahitaji uvumilivu na kuvuja jasho.
Mambo
yamebadilika, kuna wasomi wengi wenye sifa wanazurura, vijana wanapaswa
kutambua kuwa soko la ajira la sasa haliangalii shahada wala stashahada,
linaangalia wewe kama mwajiriwa utaleta mabadiliko gani chanya katika kuliletea
maendeleo.
Waajiri
wanaangalia una kitu gani kinachokutofautisha na washindani wengine, nafasi
moja ya kazi inaweza kuombwa na watu 300, lazima uoneshe sifa
zitakazowashawishi kwanini wewe uajiriwe na si mwingine ambaye licha ya ukubwa
wa shahada yake lakini pia ana uzoefu kukuzidi.
Pili
unawezaje kujiuza kwa sababu nyote mliopeleka wasifu mna bidhaa ile ile, sasa
kwanini wakuajiri wewe, je bidhaa zako ni bora zaidi ya zile 299
zilizojitangaza kuwania nafasi hiyo?
Ninachotaka
kusema hapa ni kwamba, kuwa na shahada ya uzamili au udaktari bado
hakujakuhakikishia nafasi katika ushindani wa dunia ya leo. Ni jinsi gani
unajiuza na unaweza kuuza hizo degree zako.
Tena
teknolojia imesonga mbele , barua zinachaguliwa kwa kompyuta, suala la
kuajiriwa kwa kujuana linaanza kutoweka kwa waajiri kuhitaji ueledi zaidi na
sifa za ziada.
Ni vema
vijana wakafahamu kuwa si lazima kufanya kazi waliosomea tu bali wanaweza
kutumia elimu hiyo kama njia ya kufungua fursa mpya na kuziendeleza kwani kuwa
na elimu katika taaluma fulani hakumuzuii mtu kufanya kazi nyingine.
Katika dunia
ya leo kinachoweza kupunguza janga la ukosefu wa ajira kwa vijana wengi ni
kuona fursa na kuzitumia ili kujitengenezea kipato nje ya ajira zao badala ya
kutegemea elimu zao tu.
Ni kweli
vijana hususani hapa nchini hawajaona fursa hata katika sekta ya kilimo ambayo
hutegemewa kwa kiasi kikubwa katika maisha ya kila siku ya mwanadamu kwa kutoa
hitaji kuu na la lazima linalowezesha kuishi (chakula).
Naamini eneo
hili kama vijana wangeamua kujiajiari hapa na kuwekeza nguvu na fikira zao basi
kusingelikuwa na kundi kubwa la watu wanaolia kwa kukosa ajira maana
wangejiajiri wao na kuwaajiri wengine wengi.
Hebu fikiria
wakati huu ambao Kenya inakabiliwa na tishio la ukame unaosababisha wananchi
kukosa uhakika wa chakula na kuilazimu serikali nchini humo kuweka utaratibu wa
kila familia kununua mfuko mmoja tu wa unga wa mahindi kwa siku ili kuwezesha
walau kila familia kupata mkate wa kila siku, ingeweza kuwa fursa kwa vijana
kuongeza utajiri na kukuza soko kwa kuomba vibali vya kuuza nafaka nchini humo.
Naamini kuwa
ajira zinaweza kupatikana, vijana na jamii kwa ujumla waachane na dhana ya
kutaka kuajiriwa kwa kwenye sekta rasmi tu bali wafikirie kuhusu kujiajiri na
zaidi.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment