Na Mathias Canal, Lindi
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi
imedhamiria kuimarisha usimamizi wa kilimo cha mkataba kwa kuzingatia
changamoto mbalimbali ambazo hujitokeza kwa utekelezaji wa kilimo hicho kwenye
mazao mbalimbali.
Changamoto na mafanikio yanayopatikana ni njia
mojawapo ya kuandaa sheria na kanuni za sheria ya kusimamia kilimo cha mkataba
ili kuhakikisha sheria hiyo haitoi mwanya kwa upande wowote kuivunja au kuikiuka.
Serikali kupitia wizara ya kilimo inatambua umuhimu
mkubwa wa sekta binafsi kama mhimili wa ukuaji wa sekta ndogo ya mazao na
uendelezaji wa kilimo cha mkataba ambapo katika kutekeleza msimamo huo serikali
imeweka msukumo katika kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kilimo.
Kilimo cha mkataba ni utaratibu ambao mkulima na
mnunuzi wanaingia makubaliano maalumu ya uzalishaji ambapo mnunuzi anaahidi
kutoa huduma mbalimbali kwa mkulima na anajifunga ili kuhakikisha anatumia
huduma zilizotolewa kwa lengo la kuboresha tija na uzalishaji katika kilimo.
Kilimo cha mkataba kinaweza kutekelezwa kwa mifumo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na mfumo wa ushindani uliodhibitiwa (Restrictive
contract farming) na mfumo wenye ushindani wa wazi (Competitive contract
farming).
Mfumo wa ushindani wa wazi unawawezesha wanaotaka
kuingia kwenye kilimo cha mkataba na wakulima kujinadi kwa wakulima na hatimaye
wakulima kuchagua mtoa huduma wamtakaye na kuingia kwenye mkataba naye.
Kilimo cha mkataba cha ushindani uliodhibitiwa hufanywa
kwenye maeneo yenye uzalishaji mdogo na hivyo wakulima huwa wachache ambapo
watoa huduma hushindana kwanza ili kubakia wachache ambapo wanaweza kuingia
kwenye mikataba na wakulima katika maeneo hayo.
Lengo la kuanzisha kilimo cha mkataba limetokana na
sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa masoko ya uhakika, ubora hafifu
wa mazao na uzalishaji mdogo unaombatana na gharama kubwa za uzalishaji,
upatikanaji hafifu wa huduma muhimu kwa mkulima kama vile pembejeo za kilimo
pamoja na huduma za ugani na wakulima kukosa haki stahiki ya kupata bei ya
mazao yao na kuwategemea wadhamini waliokuwa wakitoa huduma kwa wakulima hao
ambao hawakuwa na njia nyinginezo zaidi ya kutegemea wadhamini ili kuweza kuuza
mazao yao.
Aidha, Zipo faida nyingi za kilimo cha mkataba
ambazo ni pamoja na kuwa na uhakika wa soko ambapo mazao yake yatanunuliwa,
Kuuza mazao katika bei stahili iliyopo katika soko la dunia hivyo kuwa na
uhakika wa kupata faida kubwa, Kupata pembejeo za uzalishaji kwa urahisi
sambamba na kupata mtaji, elimu kuhusu kilimo cha mkataba, teknolojia pamoja na
huduma za ugani.
MWISHO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhandisi Methew J. Mtigumwe
0 comments:
Post a Comment