METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, August 4, 2017

SERIKALI YADHAMIRIA KUIMARISHA USIMAMIZI WA KILIMO CHA MKATABA

Na Mathias Canal, Lindi

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi imedhamiria kuimarisha usimamizi wa kilimo cha mkataba kwa kuzingatia changamoto mbalimbali ambazo hujitokeza kwa utekelezaji wa kilimo hicho kwenye mazao mbalimbali.

Changamoto na mafanikio yanayopatikana ni njia mojawapo ya kuandaa sheria na kanuni za sheria ya kusimamia kilimo cha mkataba ili kuhakikisha sheria hiyo haitoi mwanya kwa upande wowote kuivunja au kuikiuka.

Serikali kupitia wizara ya kilimo inatambua umuhimu mkubwa wa sekta binafsi kama mhimili wa ukuaji wa sekta ndogo ya mazao na uendelezaji wa kilimo cha mkataba ambapo katika kutekeleza msimamo huo serikali imeweka msukumo katika kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kilimo.

Kilimo cha mkataba ni utaratibu ambao mkulima na mnunuzi wanaingia makubaliano maalumu ya uzalishaji ambapo mnunuzi anaahidi kutoa huduma mbalimbali kwa mkulima na anajifunga ili kuhakikisha anatumia huduma zilizotolewa kwa lengo la kuboresha tija na uzalishaji katika kilimo.

Kilimo cha mkataba kinaweza kutekelezwa kwa mifumo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mfumo wa ushindani uliodhibitiwa (Restrictive contract farming) na mfumo wenye ushindani wa wazi (Competitive contract farming).

Mfumo wa ushindani wa wazi unawawezesha wanaotaka kuingia kwenye kilimo cha mkataba na wakulima kujinadi kwa wakulima na hatimaye wakulima kuchagua mtoa huduma wamtakaye na kuingia kwenye mkataba naye.

Kilimo cha mkataba cha ushindani uliodhibitiwa hufanywa kwenye maeneo yenye uzalishaji mdogo na hivyo wakulima huwa wachache ambapo watoa huduma hushindana kwanza ili kubakia wachache ambapo wanaweza kuingia kwenye mikataba na wakulima katika maeneo hayo.

Lengo la kuanzisha kilimo cha mkataba limetokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa masoko ya uhakika, ubora hafifu wa mazao na uzalishaji mdogo unaombatana na gharama kubwa za uzalishaji, upatikanaji hafifu wa huduma muhimu kwa mkulima kama vile pembejeo za kilimo pamoja na huduma za ugani na wakulima kukosa haki stahiki ya kupata bei ya mazao yao na kuwategemea wadhamini waliokuwa wakitoa huduma kwa wakulima hao ambao hawakuwa na njia nyinginezo zaidi ya kutegemea wadhamini ili kuweza kuuza mazao yao.

Aidha, Zipo faida nyingi za kilimo cha mkataba ambazo ni pamoja na kuwa na uhakika wa soko ambapo mazao yake yatanunuliwa, Kuuza mazao katika bei stahili iliyopo katika soko la dunia hivyo kuwa na uhakika wa kupata faida kubwa, Kupata pembejeo za uzalishaji kwa urahisi sambamba na kupata mtaji, elimu kuhusu kilimo cha mkataba, teknolojia pamoja na huduma za ugani.

MWISHO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhandisi Methew J. Mtigumwe 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com