Na Mwandishi Wetu-MAELEZO
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip
Mpango amesema serikali inathamini mchango wa sekta binafsi na
itaendelea kushirikiana nayo katika kuhakikisha azma ya Tanzania ya
viwanda inafikiwa.
Dkt. Mpango alisema hayo Jijini Dar es
Salaam alipokuwa akizindua kitabu cha Safari ya Tanzania kuelekea katika
Uchumi wa Viwanda 2016- 2056, kilichoandikwa na watanzania wazalendo
Bw. Ali Mufuruki, Gilman Kasiga na Moremi Marwa.
‘’Kitabu hiki ni kama mkombozi kwa sisi
watunga sera kwani kitatusaidia katika kuyafanyia kazi mapendekezo
ambayo yametolewa ili kuhakikisha Tanzania ya viwanda inawezekana,
nimewaelekeza pia Tume ya Mipango na Idara ya sera katika Wizara ya
Fedha kuchukua mapendekezo ambayo wataona yataisaidia serikali katika
kutekeleza azma yake ya kuendeleza viwanda’’alisema Dkt. Mpango
Bw. Ali Mufuruki mmoja wa watunzi wa
kitabu hicho alisema wameamua kuunganisha mawazo yao pamoja na kutumia
utaalamu na uzoefu wao katika masuala mbalimbali ya maendeleo na uchumi
ili kuisaidia serikali kuweza kuondokana na uchumi unaotegemea kilimo na
hatimaye kuwa nchi ya viwanda.
‘’Kuna changamoto nyingi zinazozikabili
nchi zinazoendelea ikiwemo ukosefu wa utaalamu katika kilimo cha kisasa,
ukosefu wa mitaji pamoja na kutokuwa na teknolojia ya kutosha hivyo kwa
kuwa azma ya Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni kuwa na nchi ya
uchumi wa kati unaotegemea viwanda, tukaona tumuunge mkono katika
kutimiza ndoto hiyo kwa kuandika kitabu hiki’’ alisema Mufuruki.
Bw. Mufuruki alisema kuna mambo mengi
mazuri ya kulisaidia taifa ambayo yameainishwa katika kitabu hicho hivyo
ni vyema watanzania wa kawaida, wasomi, wachumi na hata wawekezaji
wakakisoma ili kuona kila mmoja katika nafasi yake anawezaje kuisaidia
nchi kutoka hapa ilipo na kufikia katika malengo iliyojiwekea.
Kwa upande wake Bw.Gilman Kasiga ambaye
pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya General Electric katika ukanda wa Afrika
Mashariki, alisema ni vyema Tanzania ikawekeza katika masomo kwa
kutambua vipaumbele kama inavyofanya nchi ya Ujerumani ambapo sio kila
anayesoma ni lazima afikie ngazi ya shahada ndipo aonekane anaweza
kuleta mchango katika maendeleo.
Bw. Kasiga alisema asilimia 70 ya
wanaomaliza shule hapa nchini wanakimbilia kusoma shahada na kusahau
kwamba kuna masomo mengine katika ngazi za astashahada na cheti ambayo
kama yakifundishwa kwa umakini na kwa kuzingatia fani husika yanaweza
kuzalisha wataalamu wengi ambao wataisaidia nchi kupiga hatua
kimaendeleo na pia wao kupata ajira kwa urahisi katika viwanda.
Alisema elimu ya vyuo vikuu ni ya
kuandaa wasimamizi yaani mameneja na sio watendaji au wafanya kazi na
mafundi hivyo ameshauri mitaala ya vyuo iendane na ukuaji wa viwanda ili
wataaalamu hao waweze kutumia taaluma zao katika kulitumikia taifa.
0 comments:
Post a Comment