METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, August 11, 2017

IEBC: Tutatangaza matokeo ya uchaguzi wa rais kwa mujibu wa sheria

media
Katika kituo cha kupigia kura cha Gatundu, nchini Kenya.
Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Kenya imesema kuwa matokeo itakayoyatangaza yatakuwa ni kwa mujibu wa sheria na sio kwa maelekezo ya mtu au kundi fulani la wanasiasa.

Kauli ya IEBC imekuja ikiwa ni saa chache tu zimepita toka muungano wa upinzani nchinuij Kenya, NASA utangaze matokeo yake iliyosema yametokana na uhakiki walioufanya kupitia kwenye fomu zilizowekwa kwa kanzi data ya IEBC inayotumiwa kujumusha matokeo.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amekiri kupokea barua ya muungano wa NASA ambapo amesema tayari wameshawarudishia majibu ambayo nao wamesisitiza kuwa matokeo waliyo nayo sio rasmi.

IEBC inasisitiza kuwa matokeo yatakayotangazwa hayatatokana na karatasi peke yake lakini yatatokana na idadi ya wapiga kura waliojitokeza na kupiga kura kuchagua kiongozi wanaemtaka.

Chebukati amewataka wanasiasa kujiepusha na kufanya kazi za tume yake ambayo ndio yenye mamlaka ya mwisho kumtangaza mshindi.

Tume imejibu barua hii na matokeo sahihi na yakisheria yatatangazwa baada ya tume kupokea fomu zote za matokeo namba 34 B, kwa mantiki hiyo tume itatangaza matokeo ya urais kama inavyoelekezwa na ibara ya 138-3C na ile ya 138-10 ya katiba”

Awali mmoja wa vinara wa muungano wa NASA Musalia Mudavadi wakati akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, alieleza kuwa muungano wao umefanya uhakiki wa fomu zilizoko kwenye kanzi data ya IEBC na kujiridhisha kuwa mgombea wao Raila Odinga ndie mshindi.

Mudavadi alienda mbali zaidi na hata kuitaka tume ya uchaguzi kutotangaza matokeo ambayo yatakuwa kinyume na yale ambayo wamethibitisha kupitia kwenye mtandao wao.

Mpaka sasa ukweli haujajulikana kuhusu nani ameibuka mshindi kati ya rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga ambapo kwa mujibu wa tume ya uchaguzi IEBC, matokeo rasmi huenda yakatangazwa leo mchana baada ya kukamilisha uhakiki wa fomu namba 34 A na B kutoka kwa maafisa wa uchaguzi.

Shughuli nyingi zimeendelea kusimama jijini Nairobi na kwenye maeneo mengine ya nchi, ambapo wafanyakazi wachache wa uma walifika ofisini huku maelfu wakishindwa kutokana na hofu ya kutokea vurugu.

Siku ya Alhamisi waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi pia walitoa taarifa zao za awali ambapo wengi walieleza kuridhishwa na namna tume ya uchaguzi IEBC iliandaa uchaguzi ambao wamesema kwa kiwango kikubwa ulikuwa Huru na Haki.

Chanzo:RFI
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com