METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, August 11, 2017

Trump asema Korea Kaskazini wanafaa kuwa na wasiwasi sana

Donald Trump Bedminster National Golf Club in New Jersey 10 August 2017
Trump amesema huenda hajakuwa akiweka ukali wa kutosha akiionya Korea Kaskazini awali
Rais wa Marekani Donald Trump ameitahadharisha Korea Kaskazini kwamba inafaa kuwa na "wasiwasi sana" iwapo itatenda lolote kwa Marekani.

Amesema utawala wa taifa hilo utakuwa shida kubwa "ambayo ni mataifa machache sana yaliyowahi kukumbana nayo" iwapo "hawatabadilika".

Amesema hayo saa chache baada ya Korea Kaskazini kutangaza kwamba ina mpango wa kurusha makombora manne karibu na kisiwa cha Marekani cha Guam.

Waziri wa ulinzi wa Marekani James Mattis ametahadharisha kwamba mzozo wa kivita na Korea Kaskazini utakuwa na "madhara makubwa" na akadokeza kwamba juhudi za kidiplomasia kwa sasa zinaanza kuzaa matunda.

"Juhudi za Marekani zinaongozwa na diplomasia, zina msukumo wa kidiplomasia, na zinapata matokeo kidiplomasia," amesema.
Waziri mkuu wa Australia Malcolm Turnbull amesema taifa lake liko tayari kushiriki katika vita dhidi ya Korea Kaskazini iwapo nchi hiyo ya rasi ya Korea itatekeleza shambulio dhidi ya Marekani.

"Iwapo kutakuwa na shambulio dhidi ya Marekani, Mkataba wa Anzus utaanza kutekelezwa na Australia itajitokeza kuisaidia Marekani," alisema kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, "vile vile ambavyo Marekani ingefika kutusaidia iwapo tutashambuliwa."

Hali ya wasiwasi imeanza kuongezeka wiki za karibuni baada ya Korea Kaskazini kufanyia majaribio makombora mawili ya kuruka kutoka bara moja hadi nyingine mwezi Julai.

Umoja wa Mataifa hivi majuzi uliongeza vikwazo dhidi ya Pyongyang kutokana na mpango wake wa silaha za nyuklia.

Akiongea Alhamisi Bedminster, New Jersey, Bw Trump alidokeza kuwa huenda taarifa zake kuhusu Korea Kaskazini hazijakuwa na ukali wa kutosha, licha ya kuionya Korea Kaskazini wiki hii kwamba itanyeshewa na "moto na ghadhabu" kutoka kwa Marekani.

Korea Kaskazini imepuuzilia mbali vitisho vya Marekani kama "upuuzi".

Bw Trump alishutumu serikali za awali za Marekani akisema zilionyesha udhaifu sana zikikabiliana na Korea Kaskazini na pia akashutumu mshirika wa karibu wa Korea Kaskazini, akisema kwamba inafaa "kufanya juhudi zaidi."
Alisema: "Nawaambia, iwapo Korea Kaskazini itafanya jambo lolote hata kwa kufikiria tu kuhusu kumshambulia mtu tunayempenda au tunayewakilisha au washirika wetu au sisi wenyewe inaweza kuwa na wasiwasi sana, sana."

"Nitawaambia ni kwa nini...ni kwa sabbau mambo yatawatendekea ambayo hawajawahi kufikirtia kwamba yanaweza kutokea."

Hata hivyo, aliongeza kwamba Marekani bado iko huru kushiriki katika mashauriano.

Aliongeza: "Nawaambia hivi, Korea Kaskazini inafaa kujiweka sawa au wataona shida kubwa kiasi ambacho ni nchi chache sana zilizowahi kushuhudia."
Andersen Air Force Base, Guam July 18, 2017
Marekani ina kambi ya jeshi la wanahewa la Andersen kisiwa cha Guam\
Korea Kaskazini ilisema Jumatano kwamba inapanga kurusha makombora ya masafa wa wastani na ya masafa marefu kuelekea kisiwa cha Guam, ambapo kuna kambi ya ndege za kivita za kuangusha mabomu za Marekani.

Hata hivyo, kufikia sasa hakujakuwa na dalili zozote kwamba huenda kisiwa hicho cha Guam kikashambuliwa.
Map showing Guam

Kisiwa cha Guam na umuhimu wake

  • Kisiwa cha Guam kina ukubwa wa kilomita mraba 541 (maili mraba 209) na kinapatikana bahari ya Pasifiki kati ya Ufilipino na Hawaii.
  • Ni jimbo "lisilo na mpangilio wowote, na lisilojumuishwa kikamilifu" la Marekani, lenye wakazi karibu 163,000.
  • Kambi za jeshi la Marekani hutumia karibu robo ya ardhi ya kisiwa hicho. Marekani ina wanajeshi 6,000 kisiwa hicho na kuna mipango ya kuwasafirisha maelfu wengine huko.
  • Ni kituo muhimu katika shughuli za kijeshi za Marekani, ambapo huwezesha wanajeshi wa nchi hiyo kufika maeneo mengi muhimu Pasifiki, mfano eneo la bahari linalozozaniwa la South China Sea, rasi ya Korea na mlango wa bahari wa Taiwan.
Bw Trump alikuwa amewaambia wanahabari Jumanne kwamba: "Korea Kaskazini wasidhubutu kutoa vitisho zaidi kwa Marekani. Watajibiwa kwa moto na ghadhabu ambayo ulimwengu haujawahi kushuhudia."
Seneta mkongwe wa Marekani John McCain hata hivyo alikuwa na shaka kuhusu tamko la Trump.
"Viongozi wengi wakuu ambao nimewahi kuwaona, huwa hawatoi vitisho ikiwa hawako tayari kuvitekeleza na sina uhakika kwamba Rais Trump yuko tayari kuchukua hatua," alisema Bw McCain.
Korea Kaskazini ilikuwa imeghadhabishwa na vikwazo vipya ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa siku ya Jumamosi.
Vikwazo hivyo vina lengo la kupunguza mapato kutoka kwa mauzo ya bidhaa nje ya Korea Kaskazini kwa theluthi moja.
KCNA imesema Korea Kaskazini, ambayo imefanyia majaribio silaha za nyuklia mara tano, itajibu vikali na kwamba "Marekani italipia" kwa kuchangia kutunga vikwazo hivyo.
CHanzo:BBC
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com