Mkazi
wa jijini Dar es Salaam, Khairat Omary, ameishtaki Hospitali ya Kairuki
na kudai fidia ya Sh milioni 155 kwa kumsababishia matatizo katika
mfuko wa uzazi yaliyofanya aondolewe kizazi.
Khairat
kupitia Kampuni ya Uwakili ya Jonas amefungua kesi ya madai namba 184
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na imepangwa kusikilizwa mbele ya
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Katika
madai hayo, mdai anadai alikuwa akihudhuria kliniki wakati wa ujauzito
katika hospitali hiyo na Desemba 15 mwaka jana alijifungua kwa upasuaji,
akaruhusiwa Desemba 17 mwaka huo na kutakiwa kurudi tena Desemba 21.
Mdai
akiwa nyumbani alianza kusikia maumivu ikiwamo kutapika, ilipofika
Desemba 21 alirudi hospitali akaeleza maumivu anayopata kwa daktari
ambaye alielekeza afanyiwe kipimo cha Ultra Sound.
Majibu yalipotoka daktari akampatia dawa za kutuliza maumivu na kumtaka apumzike hali itaendelea kuimarika.
“Akiwa
nyumbani hali iliendelea kuwa mbaya, alisikia maumivu makali ya kichwa
na alianza kubadilika rangi ambapo alikimbizwa hospitali ya jirani,
walipompima wakaelekeza apelekwe Regency Hospital kwa matibabu zaidi.
“Regency
walimfanyia vipimo na kubaini kuna tatizo katika mfuko wa uzazi na
kumuhamishia Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako pia walimfanyia vipimo
na kubaini wakati alipofanyiwa upasuaji kuna vitu vilibakia kama pamba
ambavyo vimesababisha mfuko wa uzazi kuharibika,” ilisema sehemu ya hati
hiyo ya madai.
Anadai
ili kuokoa maisha yake alishauriwa kuondolewa kizazi, hata hivyo licha
ya kuondolewa alibakia na tatizo la fístula lililosababishwa na pamba
zilizoachwa wakati anajifungua.
Mdai
anadai kutokana na uzembe huo wa kutokuwa makini wakati wa kumzalisha
anaomba mahakama iamuru alipwe Sh milioni 20 gharama za matibabu, Sh
milioni 25 fidia kwa kukosa kipato wakati anaumwa, Sh milioni 80 gharama
za adhabu na Sh milioni 30 fidia.
Wadaiwa wanatakiwa kupeleka utete wao mahakamani na kesi hiyo itatajwa Agost 31, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment