METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, July 27, 2017

UVCCM yahimiza Wananchi kutunza barabara

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umewataka wananchi wa Kata za Pamba na Maina zilzopo katika Manispaa ya Nyamagana  kuitunza barabara inayojengwa na Serikali ili iwasaidie katika kuimarisha huduma zao za kijamii ikiwemo mawasiliano, kazi  na biashara. 

Pia Umoja huo umeeleza kufurshishwa kwake na ujenzi wa barabara hiyo  inayotumia malighafi ya mawe toka kwenye miamba ya mawe na kuajiri vijana wengi katika  ukandarasi wake Mkoani Mwanza .

Hayo yameelezwa  na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Shaka Hamdu Shaka aliposhiriki katika ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kutumia mawe na mchanga yenye urefu wa kilomita 2.5 itakayagharimu jumla ya shilingi bilioni 1.5 

Shaka alisema barabara huwaunganisha watu na kuwarahisishia upatikanaji wa mawasiliano, wepesi wa kuzifikia huduma muhimu za kijamii lakini pia hurahisha usafiri na usalama wa maisha ya watu. 

Alisema Serikali za Chama Cha Mapinduzi hazitaacha kazi ya kuwatumikia na kuwahudumia wananchi wake kwasababu hilo ni sharti na jukumu la kimkataba kati ya wananchi na serikali walioiweka madarakani kikatiba na kisheria. 

"Haya ndiyo mambo yanayohimizwa na Rais wetu, anataka vijana tufanye kazi, msiwe wategemezi au kushinda vijiweni, bila kufanya  kazi huwezi kupata maisha bora, kazi yoyote ni kazi ilimradi iwe halali na yenye kulinda utu na heshima "Alieleza 

Aidha Kaimu  Katibu Mkuu aliwataka wananchi katika wilaya ya Nyamagana kuendelea kuamini Serikali yao  abadan haitaacha kutimiza majukumu yake ya kimsingi kuwahuduma mahali popote.

Pia aliwakumbusha wenyeviti wa serikali za mitaa, madiwani na wabunge kuendelea kuwatumikia wananchi na kuwawakilisha vyema kwenye vikao vya baraza la madiwani ikiwa ni pamoja na kufuatilia miradi ya maendeleo.

Mbunge wa Nyamagana  Stanslaus Mabula alimueleza Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM  akiwa mbunge wa jimbo hilo, hataacha kutekeleza ilani ya uchaguzi ya ccm au kujitega na wajibu wa kuwatumikia wananchi. 

Mabula alieleza kuwa amekuwa katika juhudi kubwa za kuharakisha utatuzi wa kero ya barabara hiyo na nyingine zinatatuka kwa uharaka ili wananchi wapate manufaa na kuweza kutumia fursa mbalimbali. 

"Nimechaguliwa kuwa mbunge kwa tiketi ya ccm, walionipigia kura ni wananchi wa Nyamagana , mkataba wetu na wananchi ni kuwatumikia, kuwawakilisha na kutatua kero zinazowakabili kihuduma, kijamii  na kiuchumi "Alieleza Mabula 

Hata hivyo alisifu juhudi zinazofanywa na kaimu katibu mkuu wa UVCCM  Shaka Hamdu Shaka katika kuuboresha na kuupa nguvu umoja huo kwa kufanya ziara nchi nzima kuwaamsha vijana na makundi mengine na  kuitetea serikali kila inapobidi. 

Shaka ameanza ziara katika wilaya ya Nyamagana baada ya kuhitimisha ziara yake katika halmashauri ya  wilaya ya Manispaa ya Ilemela akitokea wikaya ya Ukerewe.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com