Na Mwandishi Wetu, Nyamagana-Mwanza
Umoja Wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa umesema kuwa hauwezi kufumbia macho wanachama wa jumuiya hiyo walioomba nafasi Mbalimbali za kugombea ilihali wanajiimarisha katika safu za kisiasa.
Umoja huo umesema kuwa kupanga safu katika chaguzi Mbalimbali za Chama ni makosa makubwa kwa wagombea na hata wanachama wasiokuwa wagombea kwani kufanya hivyo ni kukiuka Mpango madhubuti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuimarisha nchi katika sekta ya kiuchumi na kijamii kupitia CCM Mpya na Tanzania Mpya.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Ndg Shaka Hamdu Shaka (MNEC) Leo Julai 25, 2017 Manispaa ya Nyamagana Mkoani Mwanza Wakati wa ziara ya siku moja alipokuwa akizungumza na Vijana wa Jumuiya ya Chama hicho (UVCCM) pamoja na wanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM) Mara baada ya kufungua shina la wakereketwa Eneo la Stendi ya Mwaloni maarufu kama Mererani.
Shaka alisema kuwa Jumuiya ya Vijana ni Jeshi mahususi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo kuelekea uchaguzi Mkuu wa Chama na Jumuiya zake CCM imejipanga kuwapata viongozi madhubuti watakaoweza kuimarisha usawa katika jamii na Kusimamia vyema utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Mwaka 2015-2020.
Alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi CCM Kimepewa dhamana kubwa na Wananchi ya kuwaletea maendeleo hivyo kufanya mikutano ya ndani nchini ni sehemu ya kuangalia namna utekelezaji wa Imani waliyoitoa Wananchi kupitia ilani inavyosimamiwa.
Shaka amewasihi Wananchi kutoa ushirikiano Mkubwa kwa madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli ili kutimiza ndoto ya Tanzania ya maendeleo endelevu.
Katika Ziara hiyo Kaimu Katibu Mkuu huyo ameshiriki ujenzi wa Ofisi ya CCM Tawi la Bugarika Kaskazini na kuahidi kumalizia katika upauaji jambo ambalo limemfanya pia Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mhe Stanislaus Mabula kuchangia Bando tatu za bati ili kumuunga mkono Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Taifa Ndg Shaka Hamdu Shaka.
Aidha, Shaka ameshiriki ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha Mawe yenye urefu wa Kilomita moja kwani itatoa urahisi wa Huduma za kijamii hususani kwa Wakati wa Kaya ya Mahina na Kata ya Pamba.
Alisema kuwa tayari Vijana wengi wamepata ajira kwenye ujenzi huo na kujipatia kipato kizuri kinachoanzia shilingi 28,000 mpaka Shilingi 40,000 kwa siku.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment