METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 24, 2017

UVCCM: FEDHA ZA UMMA NI LAZIMA ZITUMIKE KAMA ZILIVYOKUSUDIWA, ILEMELA YAPONGEZWA KWA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM

Na Mathias Canal, Ilemela-Mwanza

Umoja Wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa umesema kuwa fedha nyingi Serikalini zimekuwa zikitumika Tofauti na kusudio la bajeti jambo ambalo limepelekea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulaumiwa na wananchi kwa makosa ya watendaji wachache.

UVCCCM imesema kuwa katika kipindi hiki Watendaji wengi Serikalini wamehuishwa pia Vijana waliofunzwa vizuri itikadi za Chama Cha Mapinduzi jambo ambalo limeamsha ari ya uwajibikaji na utendaji mkubwa ambao umeibua hamasa na kuonyesha namna ambavyo Vijana watokanao na Umoja Wa Vijana UVCCM wana uzalendo na nchi yao.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Ndg Shaka Hamdu Shaka (MNEC) Julai 24, 2017 Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza Wakati wa ziara ya siku moja alipokuwa akizungumza na Vijana wa Jumuiya ya Chama hicho (UVCCM) pamoja na  wanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano wa ndani uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Shaka amepongeza utekelezwaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi unaofanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela hususani katika utoaji wa asilimia 5 ya mikopo kwa Vijana kama ilivyoainishwa na Ilani ya Ushindi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2015-2020.

Alisema kuwa Halmashauri zote nchini zinapaswa kuiga uwajibikaji unaofanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kuanzisha miradi Mbalimbali na kuwapatia mikopo ile ya asilimia tano kwa Vijana.

Shaka amepongeza Mradi wa Utengenezaji matofali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika Jimbo Ilemela awamu ya kwanza, Mara baada ya kutembelea Mradi huo unaosimamiwa na Taasisi ya The Angeline Foundation na kufadhiliwa na shirika la nyumba la Taifa (NHC).

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Mratibu wa Taasisi ya The Angeline Foundation Ndg Emmanuel S. Michael imeeleza kuwa Mradi huo ulianzishwa kwa juhudi binafsi za Mhe Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula kwa ushirikiano na Taasisi ya The Angeline Foundation ikiwa ni matokeo ya harambee iliyofanyika mwaka 2016 Mwezi Julai katika Ukumbi wa Rockycity Mall kwa dhumuni la kusaidia sekta ya Elimu katika Jimbo la Ilemela na wananchi wake.

Shaka alisema kuwa Miradi kama hiyo inapoanzishwa kwa Vijana kuna mategemeo makubwa ya Vijana wengi kupata elimu ya ufundi stadi hususani katika ujenzi wa nyumba bora na utengenezaji wa matofali ya kisasa,Vijana kupata ajira za muda mfupi, Ongezeko la kipato kwa Vijana na hatimaye kuacha kushinda vijiweni, ambapo zaidi Vijana wengi wanapojumuika pamoja wanapata fursa ya Kujiunga katika vikundi Mbalimbali vya kudumu na kupata usajili wa kudumu chini ya Halmashauri.

Aidha Shaka amewasihi Vijana kuwa wavumilivu wanapojumuika katika vikundi mbalimbali kwani mafanikio hayapatikani ndani ya siku moja badala yake ni mchakato wa muda mrefu.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com