METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, July 25, 2017

SPIKA WA BUNGE LA TANZANIA APOKEA BARUA YA KUFUKUZWA UWANACHAMA WABUNGE WA CUF

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Job Ndugai leo tarehe 25, Julai 2017 amepokea barua kutoka kwa Mwenyekiti wa chama cha wananchi (CUF) Mh. Ibrahim Lipumba na Mh. Magdalena Sakaya (Mb) – kaimu katibu mkuu (CUF), inayohusu kumpa taarifa ya kuwafukuza wabunge wanane (8) na madiwani wawili (2) kwa makosa mbalimbali ya kinidhamu. Hii imetokana na uamuzi wa Baraza kuu la chama cha wananchi (CUF)  lililoketi tarehe 23, Julai 2017 na kutoa adhabu hiyo.

Katika barua hiyo, wabunge waliofukuzwa uwanachama ni Riziki Shahali Ngwali (Mbunge Viti Maalum), Saverina Mwijage (Mbunge Viti Maalum), Salma Mwassa (Mbunge Viti Maalum), na Saumu Sakala (Mbunge Viti Maalum)

Wabunge wengine waliokumbwa na adhabu hiyo ya kufukuzwa uwanachama ni pamoja na Raisa Abdallah Mussa (Mbunge Viti Maalum), Miza Bakari (Mbunge Viti Maalum),Halima Ali Mohammed (Mbunge Viti Maalum), na Khadija El Kassim (Mbunge Viti Maalum)

Madiwani wawili (2) waliofukuzwa uwanachama majina yao ni Elizabeth Magwaja (Diwani Viti Maalum) na Leila Hussein (Diwani Viti Maalum).

Pia barua hiyo imeainisha makosa waliyoyafanya ya kuenenda kinyume na kifungu cha 83(4) na (5) cha katiba ya CUF kwa kutenda makosa yafuatayo

1.Kukihujumu chama katika uchaguzi wa marudio wa madiwani wa tarehe 22 Januari, 2017

2.Kumkashfu na kumdhalilisha mwenyekiti wa taifa wa chama hicho Mh. Prof. Ibrahim H. Lipumba, Naibu katibu mkuu na Mbunge wa kaliua Mh. Magdalena Sakaya (Mb) na Mkurugenzi wa chama

3.Kushirikiana na chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kupanga oparesheni waliyoiita “ ONDOA MSALITI BUGURUNI” wakiwa na lengo la kumuondoa mwenyekiti halali wa chama hicho ni kinyume nataratibu za kitiba ya CUF na sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.

4.Kuruhusu na kuipa fursa CHADEMA kuwa msemaji wa masuala ya CUF kinyume na matakwa ya katiba ya CUF.

5.Kulipa pango na kufungua ofisi ya CUF Magomeni bila kufuata taratibu za kikatiba; na

6. Kuchangia Fedha zilizotumika kukodisha ma bouncer kwa lengo la kuwadhuru viongozi watiifu wa chama akiwemo mwenyekiti wa Taifa, Prof. Ibrahim H. Lipumba, Naibu katibu mkuu Mh. Mgdalena Sakaya (Mb), Mh. Maftaha Nachuma (Mb) mkurugenzi wa CUF wa mambo ya nje na mbunge wa mtwara mjini.

Mh. Spika Job Ndugai amesema kuwa kila chama kina utaratibu wake wa kuwaondoa wanachama wake kulingana na utashi au katiba ya chama husika, na akaongeza kusema kuwa bado anaendelea kuitafakari barua hiyo na hapo baadae atatoa taarifa rasmi ya maamuzi ya spika kwa wabunge na madiwani waliofukuzwa uwanachama na Baraza kuu la CUF

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com