Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, amewataka Watanzania,
wakiwamo wanasiasa, kuacha kulalamika kwa kukosekana kwa haki, huku
akiwataka kujiuliza iwapo wametimiza wajibu wao.
Amesema
amekuwa akichukizwa na baadhi ya wanasiasa hapa nchini, ambao kila siku
wamekuwa wakilalamika kutaka haki, hali ya kuwa wao hawatimizi wajibu.
Rais
huyo mstaafu ametoa kauli hiyo huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa
baadhi ya viongozi wa upinzani kudai haki ya demokrasia na kupinga
kuzuiwa kufanya shughuli zao za kisiasa kupitia mikutano.
Hatua
hiyo imekuwa ikizua malalamiko ikiwemo kuwaomba marais wastafu
kujitokeza na kumshauri Rais Dk. John Magufuli kutokana na maamuzi yake
mbalimbali aliyoyachukua kwa nchi.
Kutokana
na hali hiyo, Mkapa amewataka wasomi na wafanyakazi kuendesha midahalo
na makongamano ya kuhakikisha nchi inajitegemea badala ya kulalamika
kila siku.
Kauli
hiyo aliitoa jana wilayani Itilima, mkoani Simiyu, alipokuwa akikabidhi
Jengo la Upasuaji (Theater) katika Kituo cha Afya Nkoma, lililojengwa
na Taasisi ya Mkapa Foundation kwa gharama ya Sh milioni 270.
Rais
huyo mstaafu alisema wanasiasa hao, licha ya kulalamika, lakini
hawatimiza wajibu wa kuhakikisha wanafanya kazi ili kuletea nchi
maendeleo.
Katika
kile kinachoonekana kuchukizwa na hali hiyo, Mkapa alisema kila
Mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha taifa linajitegemea na kuwaletea
wananchi wake maendeleo.
“Kila
siku utasikia watu wanadai haki, makongamano, midahalo ya kudai haki,
swali la kuwauliza wao je, wametimiza wajibu kama Watanzania… maana
hakuna haki bila wajibu, ni lazima kubadilika na kuendesha makongamano
ya kuonyesha nchi itajitegemea vipi,” alisema Mkapa.
Rais
huyo Mstaafu alisema ili kuweza kujitegemea, ni lazima kila Mtanzania
atimize wajibu wa kufanya kazi kama Rais Dk. John Magufuli anavyosema,
huku akitoa mfano katika nchi ya Japan ambapo wananchi wake jambo la
kwanza ni kufanya kazi.
“Kama
tunatarajia mataifa kuja kutuinua wakati sisi tumekaa ni dhana potofu,
viongozi tubuni miradi ili tujiendeleze na kujiletea maendeleo sisi
wenyewe, kama nchi ya Japan wanavyofanya,” alisema Mkapa.
Aliongeza
kuwa, toka utawala wa Baba wa Taifa na sera ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), tangu enzi ilikuwa ni ujamaa na kujitegemea, jambo ambalo
ameeleza lazima litekelezwe kwa kila mmoja katika kutimiza wajibu kwa
nafasi yake.
Akizungumzia
jengo hilo, Mkapa aliishukuru Japan, ambao walitoa fedha kwa ajili ya
ujenzi wa jengo hilo kupitia Taasisi ya Mkapa Foundation, lengo likiwa
ni kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.
“Nchi
yetu bado tunakabiliwa na changamoto ya vifo vya akina mama wajawazito
pamoja na watoto wachanga, nchi ya Japan wametoa msaada huo kwa ajili ya
kukabiliana na changamoto hii.
“… taasisi ya Mkapa itaendeleza ushirikiano na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali za afya,” alisema.
Baada ya kukabidhi jengo hilo la upasuaji, Rais Mkapa na msafara wake walielekea wilayani Chato
0 comments:
Post a Comment