METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, July 7, 2017

KATIBU WILAYA YA UBUNGO AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA MABALOZI WA MASHINA 50 KATA YA MBURAHATI

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ubungo Ndg. Salum Kali amekutana na kufanya mkutano na mabalozi wa Mashina 50, wajumbe wa kamati za shina, kamati ya siasa ya Kata na Matawi yaliyopo katika Kata ya Mburahati.

Mkutano huo umefanyika leo katika ukumbi wa CCM Mburahati uliopo Mburahati Barafu.

Wakati wa Kikao hicho kilichokuwa na agenda mbalimbali ikiwemo kujitambulisha kwa mabalozi, wajumbe wa kamati za shina, kamati ya siasa ya Kata na Matawi, Katibu Kali aliwataka kumuunga mkono kwa vitendo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

"Rais wetu ana nia ya dhati ya kuwatumikia watanzania bila kujali dini, Chama wala kabila, kwa hiyo na sisi kama viongozi tuliopewa dhamana ya kuwaongoza wananchi tumuunge mkono Rais wetu kwa vitendo kwa yale yote anayoyafanya" alisema Katibu Kali.

Pia aliwataka mabalozi hao kuwahamasisha wananchi wanaoishi katika maeneo yao kujiunga katika vikundi vya ujasiliamali ili kuweza kupata mikopo ya asilimia 5 kwa Vijana na asilimia 5 kwa wakina mama.

Sambamba na hilo aliwataka mabalozi pamoja na wana CCM wanaoishi Kata hiyo kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi ngazi ya Wilaya ambapo fomu zimeanza kutolewa tangu tarehe 02/07/2017  mpaka 10/07/2017.

"Ndugu wana CCM fomu za kugombea uongozi ngazi ya Wilaya zimeanza kutolewa tangu tarehe 02/07/2017 na mwisho ni tarehe 10/07/2017 kwa hiyo jipime na ukiona unatosha kachukue fomu ugombee uongozi ndani ya Chama " alisema Katibu

Pia aliwataka mabalozi hao kuhakikisha wanawaandikisha wananchi wanaoishi kwenye maeneo yao kwenye daftari la wakazi pia wawe makini na mamluki wanaoingizwa kwenye daftari hilo wakati wa uchaguzi.

Mwisho Katibu Kali aliwataka wana CCM kuwa na umoja sambamba na mshikamano kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

IMETOLEWA NA
OFISI YA KATIBU WA CCM WILAYA
WILAYA YA UBUNGO
DAR ES SALAAM

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com