METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, July 12, 2017

Japan yakabidhi kiwanda cha mafuta kwa Chama cha Ushirika Chato, Kinauwezo wa kuzalisha lita 700 za mafuta kwa siku

 
Na,Emmanuel Twimanye     Geita,
 
Serikali ya Japan imekabidhi kiwanda cha kuchakata na Kuzalisha Mafuta ya Alizeti kwa chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko wilayani Chato Mkoani Geita chenye uwezo wa kuzalisha lita 700 za mafuta kwa siku.

Akikabidhi kiwanda hicho,Balozi wa Japani nchini Bw. Masaharu Yoshida amesema Serikali ya Japan itaendelea kuimarisha ushirikiano huo baina ya nchi hizo mbili katika kuleta maendeleo kwa wananchi Tanzania.

Mbunge wa Jimbo la Chato, Dk. Medard Kalemani aliyeshiriki kwenye makabidhiano hayo amesema serikali ya Japani licha ya kujenga kiwanda hicho Chenye Thamani ya Sh. 170 milioni, pia Japan inatekeleza ujenzi wa mradi wa soko la samaki la Kimataifa katika kijiji cha Kasenda litakalogharimu Sh. 320 milioni.

Awali mwenyekiti wa Chama cha Ushirika na Masoko, Elias Kaswahili na Meneja wa Mradi huo Faidaya Misango wamesema uzalishalishaji wa Mafuta ni mkubwa ukilinganisha na upatikanaji wa Alizeti na hivyo kutoa wito kwa wananchi kulima zao hilo ili kuwezesha kiwanda hicho kufanya kazi.

Aidha, kwa niaba ya Wananchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ameipongeza serikali ya Japan ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

Japan ni nchi ambayo imetajwa kuwa rafiki wa karibu na Tanzania na hii inajidhihirisha katika kutoa ufadhili wa miradi ya mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya miundombinu ya barabara, masoko, reli na elimu.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com