Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu Agosti 30, 2017 itatoa hukumu katika kesi ya
kushindwa kuhifadhi silaha na risasi inayomkabili Askofu wa Kanisa la
ufufuo na uzima, Josephat Gwajima na wenzake watatu.
Hukumu
hiyo ilipaswa kutolewa leo Jumatatu, Julai 31 kwa Hakimu Mfawidhi,
Cyprian Mkeha lakini ilishindikana kwa sababu hakimu huyo alikuwa na
udhuru.
Hata
hivyo, Wakili Peter Kibatala amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey
Mwambapa wakati kesi ilipoitwa mbele yake kuwa Askofu Gwajima ni mgonjwa
na mahakamani hapo amewakilishwa na mdhamini wake.
Hayo
yametokea baada wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro kuiambia mahakama
kuwa washtakiwa George Mzava, Msaidizi wa Askofu Gwajima, Yekonia
Bihagaze (39) na Georgey Milulu wapo mahakamani lakini Askofu Gwajima
hayupo.
Pia,
amedai kesi ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa hukumu
lakini wamepata taarifa Hakimu Mfawidhi, Mkeha anayeisikiliza kesi hiyo
anaudhuru.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo kesi imeahirishwa hadi Agosti 30, 2017 ambapo watasomewa hukumu.
Mzava,
Bihagaze na Milulu wao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa
wakimiliki bastola aina ya berretta pamoja na risasi 20 kinyume cha
sheria.
Hukumu
hiyo inatarajiwa kutolewa siku hiyo na Hakimu Mfawidhi wa mahakama
hiyo, Cyprian Mkeha mara baada ya mashahidi wa upande wa mashtaka na
utetezi kutoa ushahidi wao na kuufunga.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali, Shedrack Kimaro na Joseph Maugo.
Huku
upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Peter Kibatala ambapo
washtakiwa walijitetea pamoja na mashahidi wao wawili akiwamo Nesi wa
hospitali ya TMJ, Devotha Bayona na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima George Kiwia.
Katika
ushahidi wa upande wa utetezi wa shahidi, Devotha alidai kuwa yeye ni
afisa muugizi daraja la pili katika Hospitali ya TMJ na yupo kitengo cha
ICU.
Machi
29, 2015 aliingia zamu usiku akipokea zamu toka kwa Nesi Rebecca ambaye
aliacha kazi 2016 wakati huo Askofu alikuwa amelazwa katika hospitali
hiyo kwa siku ya tatu.
Anakumbuka
siku hiyo walikwenda askari wawili na mtu mwingine Bihagaze wakagonga
mlango wa ICU wakahitaji begi la mgonjwa, walivyojitambulisha alitaka
kuhakikisha ni kweli akamfuata Gwajima na kumuuliza. Alieleza ushahidi.
Amedai
Gwajima alimueleza ni kweli Bihagaze ni msaidizi wake na kwamba
Bihagaze alimwambia yupo pamoja na askari hao wanataka begi la mgonjwa.
Muuguzi
huyo amesema Gwajima alisema hawezi kutoa begi hadi wapewe maelezo
maalumu na kwamba begi hilo lilikuwepo pembeni ya kitanda cha Gwajima.
Baada
ya kupewa majibu hayo na Gwajima, aliwaambia polisi amesema hawezi
kulitoa hadi polisi waandike maelezo, wakamueleza wanachohitaji ni begi
na maelezo wataandika kesho.
Wakati wanajibizana Gwajima alisikia na akamwambia nesi atawapa hilo begi kwa sababu ndani Lina silaha yake.
“Polisi walitaka kuingia kinguvu nikawaambia hapa ni ICU hamuwezi kuingia kinguvu, " alieleza nesi huyo na kwamba Gwajima alimwambia kama wanalihitaji kinguvu chukua begi mpe Bihagaze awape polisi.
Amedai
kabla hajampatia begi hilo Bihagaze polisi walimpokonya, akafunga
mlango akaendelea na mgonjwa wake lakini alimuona mgonjwa anamawazo.
Washtakiwa
wengine mbali na Gwajima wao wanadaiwa kuwa Machi 29, 2015 katika
Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A walikutwa wakimiliki Bastola aina
ya Berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali toka kwa
mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.
Imeendelea
kudaiwa kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha
32 (1) na cha 34 (1) (2) na(3) cha sheria ya Silaha na Milipuko sura ya
223 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Pia,
wanadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio washtakiwa hao pia walikutwa
wakimiliki isivyo halali risasi tatu za bastola pamoja na risasi 17 za
bunduki aina ya Shotgun.
Washtakiwa
hao wapo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti waliyopewa ya
kuwa kila mshtakiwa awe na mdhamini mmoja anayeaminika ambaye alisaini
hati ya maneno ya dhamana yenye thamani ya Sh1 milioni.
0 comments:
Post a Comment