METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, June 9, 2017

Yericko Nyerere apandishwa tena kizimbani

Mfanyabiashara Yericko Nyerere amefikishwa leo (Ijumaa) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kupandishwa kizimbani akikabiliwa na kesi nyingine ya kuchapisha maneno yenye nia ya uchochezi kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

Akisomewa shtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa  kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage, Yericko anadaiwa kuwa  Mei 28, 2017 kwa nia ya kuwachochea Watanzania alichapisha maneno kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook yasemayo:


 “Maazimio ya Baraza Kuu yalikuwa (1) Katiba Mpya, (2) Tume Huru, (3) Bunge, (4) Haki ya Kikatiba ya kuishi (Ben Saanane), (5) Haki ya Kikatiba ya kukutana na kuzungumza (Mikutano ya Hadhara ya Kisiasa) Hayo ndiyo yatahubiriwa katika Operesheni Ukuta.

Baraza Kuu limeridhia kwa kauli moja kwamba vita rasmi ya kulikomboa Taifa imezinduliwa na kama wewe Mtanzania unaogopa kulitetea Taifa hili ni bora uka kaa kando, nenda huko CCM ambako michemsho na supu vipo kwa wingi…kufa kwetu ni ukombozi wa Tanzania….” Mwisho wa kunukuu.

Yericko ambaye anatetewa na Wakili Peter Kibatala baada ya kusomewa shtaka hilo amekana  na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wake bado haujakamilika.

Hakimu Mwijage amemtaka mshtakiwa huyo kuwa na mdhamini mmoja ambaye amesaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh10 milioni, amekamilisha na kuachiwa huru. Kesi imeahirishwa hadi Julai 6, 2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com