Wanaojifungulia nyumbani waonywa
WANAWAKE katika Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma wametakiwa kuondokana na tabia ya kujifungulia majumbani ili kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa, Amour Hamad Amour mara baada ya kuweka jiwe la msingi la uboreshaji wa miundombinu ya zahanati ya Bolisa iliyopo halmashauri ya Mji wa Kondoa. Alisema ifike wakati kinamama waondokane na tabia ya kujifungulia nyumbani kwani kuna athari kubwa kiafya na wakati mwingine husababisha vifo ambavyo vinaweza kuepukika.
“Ukijifungulia kwenye kituo cha afya unapunguza uwezekano wa kutokea vifo vinavyotokana na uzazi, wakunga wanatakiwa kuwaelimisha wanawake wanaokuja hospitali baada ya kujifungulia majumbani, lazima muwape elimu ya kutosha ili waone umuhimu wa kujifungulia kwenye vituo vya afya,” alisema. Awali akisoma taarifa ya mradi wa maji katika zahanati ya kijiji cha Bolisa, Katibu wa Afya wa Hospitali ya Kondoa, Alpha Cholobi alisema ujenzi wa mradi huo ulianza Novemba mwaka jana kwa ufadhili wa Serikali ya Uswis kupitia Shirika la Mkaji (Maji kwa Jamii).
Alisema miongoni mwa kazi zilizofanyika ni kuchimba kisima kirefu ambapo kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kutoa maji kiasi cha mita za ujazo 14,000 kwa saa, uwekaji wa tanki la juu lenye ujazo wa lita 5,000, ujenzi wa choo na kufunga miundombinu ya maji ndani ya zahanati na shughuli zilizobaki ni kufunga umeme na mashine ya maji. Cholobi alisema lengo la mradi huo ni kusambaza maji katika zahanati na kusaidia kinamama wanaokuja kujifungua na malengo ya baadaye ni kusambaza maji kijiji kizima cha Bolisa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Sezeria Makota alisema mradi huo ni wa kipekee kwani awali ilikuwa ni shida kwa wanawake kujifungulia kituoni hapo kutokana na ukosefu wa maji. Alisema kupatikana kwa maji kutafanya wanawake wengi zaidi kujifungulia kituoni hapo.
Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Amina Jumanne alisema walikuwa wakipata shida kubwa kupeleka mzazi kujifungua kituoni hapo kwani walilazimika kubeba maji umbali mrefu. Alisema hali hiyo ilifanya wawe wanaondoka na nguo chafu nyumbani. “Tunaishukuru sana serikali kuleta maji kwenye hospitali hii tuna hakika mzazi ataoga, tutafua nguo na kwenda nyumbani wasafi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment