METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, June 6, 2017

Upatikanaji wa maji ya uhakika bado tatizo kwa wakulima-Sendeka

MKUU wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amegusia upatikanaji maji ya uhakika kuwa ni changamoto kubwa, inayowakumba wakulima katika mkoa wake na mikoa ya jirani katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.
Alisema hayo jana katika mkutano siku mbili wa kufanya tathmini maendeleo ya Kongani ya Ihemi iliyo chini ya mpango wa kuendeleza kilimo wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Ushoroba wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), ambapo alibainisha shughuli za kibinadamu ndizo zinazosababisha vyanzo vya maji kukauka.
“Hatuwezi kuwa na kilimo chenye tija ikiwa bado tunahagaika kuwa na teknolojia ya kisasa ya kupata maji ya uhakika, vyanzo vya maji vimekauka kutokana na kuharibiwa na shughuli za kibinadamu zinazoathiri mazingira.
Tuache kilimo cha vinyungu pembezoni mwa vyanzo vya maji,” alisema Ole Sendeka ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo na kusisitiza: “Tufahamu kuwa kilimo endelevu chenye tija ndio kichocheo cha kuzalisha malighafi za viwanda.
Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kuwa na uchumi wa kati na kuanzisha viwanda, malighafi zote za viwandani zinatoka kwenye kilimo.” Awali, akifungua mkutano huo, Mkuu wa Maendeleo ya Kongani ya Ihemi inayojumuisha mikoa miwili ya Njombe na Iringa, Maria Ijumba aligusia umuhimu wa kushirikiana wakulima wadogo na wakubwa ili kuimarisha shughuli za kilimo na kubadilishana uzoefu.
Alisema wadau wote wa kilimo wakiwemo wakulima wenyewe, mashirika ya maendeleo, wafanyabiashara wa mazao, wamiliki wa viwanda na viongozi wa serikali kwa nafasi zao wajitathmini wameifanyia nini kongania ya Ihemi ili kuona kama kuna uwezekano wa kuhamia kongani nyingine.
“Tujipime tupo wapi, mipango tuliyokuwa nayo miaka mitatu iliyopita wakati tukianzisha kongani hii imefanikiwa kwa kiasi gani,” alihoji Bibi Ijumba na kuongeza, “Kitu muhimu cha kuangalia kama tumepiga hatua ni miundombinu ikiwemo barabara, upatikanaji maji, mawasiliano ikiwemo umeme, maghala ya kuhifadhia chakula.
Tuangalie wakulima wanauza vipi mazao yao na wananunuaje pembejeo za kilimo na uhakika wa viwanda vya kuchakata mazao.” Alisema hapo ndipo wanaweza kusema wamefanikiwa na wapo tayari kuhamia kongani nyingine kati ya sita, ambazo SAGCOT wameziainisha kusaidia wakulima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Geofrey Kirenga alisema kilimo ndilo eneo linalogusa maisha ya wanadamu moja kwa moja, hivyo atahakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anawafanya wakulima wanufaike kupitia shughuli hii.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com