METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, June 27, 2017

TATIZO LA UJAUZITO MASHULENI JAMII HAIJATIMIZA WAJIBU WAKE

Na Debora Charles

Elimu ya Msingi na Sekondari ndio kiunganishi kikubwa cha ndoto aliyonayo mwanafunzi kufikia malengo aliyojiwekea katika kuchochea Maendeleo yake mwenyewe na Jamii kwa ujumla kupitia elimu. Inaaminika duniani kote kupitia tafiti mbalimbali kuwa, elimu huhusishwa na Maendeleo ya jamii kupitia Uimarishaji wa fursa, Stadi Mahususi pamoja na kupanua wigo wa Mitandao ya watu.

Kwa kutambua hilo, Serikali imeendelea na jitihada kubwa za kupanua na kuboresha upatikanaji wa huduma za elimu ya Msingi na Sekondari kupitia Sera mbalimbali kama vile Sera ya “Elimu Bure” ambapo mpaka sasa zinatengwa Shilingi Bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kukidhi hitaji hilo. Jambo ambalo linatoa fursa kwa watoto wote maskini na tajiri kupata huduma hiyo. Kadhalika zipo Sera mbalimbali zinazowezesha makundi mengine kama vile watoto na walemavu kupata Elimu katika mazingira mengine rafiki ukiachilia mbali ongezeko la miundombinu kama madawati na vyumba vya madarasa ambavyo Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutekeleza.

Ufanisi wa Elimu ya Msingi na Sekondari hasa kwa watoto wa kike utaendelea kuimarika zaidi pale tu jamii itaungana kwa dhati kabisa kupinga vikali na kukemea masuala yote yanayokiuka misingi ya Maadili, Mila, Desturi, Dini na hata Mazingira ya Taifa letu.

Kutunza Maadili na Tunu za nchi huleta ustawi na nguvu ya kujipambanua Utaifa wetu kwa mataifa mengine. Ili kurudisha heshma ya Elimu ya Msingi na Sekondari lazima watoto wajengewe hofu ya kutenda mambo yanayokiuka Misingi na Maadili ya nchi yao. Lazima wakuwe wakiamini kuwa kukiuka misingi na Maadili ya nchi ni kukosa heshima kwa Taifa, Jamii na hata familia zao.

Ripoti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inaonyesha, wasichana 8,000 kila mwaka huacha shule kutokana na ujauzito. Kati yao 3,000 ni wanafunzi wa shule za msingi na 5,000 ni wanafunzi wa shule za Sekondari. Kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaopata ujauzito mashuleni ni dhahiri kabisa kuwa kuna mahali kama Taifa haijalishi watoto wenyewe, wazazi au jamii tumejikwaa katika kutimiza wajibu wetu. Hatuwezi kujidanganya kuwa kutatua tatizo hili ni kuruhusu watoto hawa waendelee na masomo. Kufanya hivyo ni kuhamasisha ongezeko la vitendo vya Ngono kwa watoto mashuleni.

Takwimu zinaonyesha kuwa, kila siku wajawazito 24 hufa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kujifungua. Wanawake watano hadi sita wanaokufa kati ya hao ni watoto wadogo. Kadhalika Asilimia 17 ya wanawake wa Tanzania wa umri kati ya miaka 15 na 19, wamehawi kuzaa na kuwa wazazi na asilimia 6 ni wajawazito.

Takwimu zinaendelea kuonyesha kuwa, mbali na kuhatarisha uhai wao wakati wote wa ujauzito na kujifungua, wasichana chini ya umri wa miaka 20 ni tishio pia kwa watoto wanaozaliwa nao. Wasichana hao wanakabiliwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI vinavyosambaa kwa kasi nchini.

Ipo haja kama watanzania kushiriki kuwajengea watoto fikra za kujikita kwenye masomo yao kwanza kuliko kuhamasisha uhuru wa kufanya ngono ili kuwaondoa kwenye athari za kulemaa kifikra, vifo vinavyotokana na mimba za utotoni, maambukizi ya virusi vya UKIMWI na kupunguza nguvukazi ya Taifa.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) inaonyesha watoto 13,822 ambao wamezaliwa katika mwaka 2005 na 2010 ifikapo 2020 watakuwa wameolewa chini ya miaka 18. Hii ni kutokana na kasi ya ongezeko la mimba za utotoni, ambazo kama jamii lazima tutimize wajibu wetu kuzikemea.

Kuwarudisha mashuleni watoto wanaopata ujauzito ni kuwachelewesha kutafuta fursa nyingine za kujikwamua kimaisha kutokana na wengi kushindwa kumudu malezi na masomo na hata wengine kushindwa kufaulu kutokana na aibu ya kuchangamana na wenzao.

Takwimu zinaonyesha wanaowapa mimba watoto wa shule wengi wao ni vijana wenzao ambao mara nyingi huwa ni wanafunzi wenzao. Hali hii hupelekea kuongeza idadi ya watoto tegemezi na idadi kubwa ya watoto wa mitaani kutokana  na wazazi wengi hasa wa kiume kutelekeza watoto wao.

Ipo haja ya viongozi na waumini wa dini zote kuwa mstali wa mbele kukemea vitendo hivi vya upatiakanaji wa Mimba mashuleni kupitia maneno na matendo yao ili jamii iwatazame na kujifunza kutoka kwao.

Ili kuondoa ongezeko la mimba za utotoni, Ipo haja ya Serikali kufanya Marekebisho kwenye Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayomruhusu mtoto wa kike kuweza kuolewa akiwa na miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi wake.

Ipo haja ya kuendelea kutumia Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 kifungu cha 35 na kanuni zake na marekebisho yaliyofanyika mwaka 1995 na 2002 kinachosema “Mtoto wa kike akipata mimba akiwa shuleni ni ushahidi tosha kuwa amefanya ngono kinyume na sheria hivyo adhabu yake ni kufukuzwa shule”. Isipokuwa iboreshwe kwa kumtafutia njia wezeshi itakayompa fursa ya kujikomboa kiuchumi.

Ipo haja kwa wazazi hasa walioko vijijini kuongeza muamuko kwa watoto wao juu ya umuhimu wa elimu. Ripoti ya Twaweza kupitia utafiti wake wa  ”Sauti za Wananchi” August, 2016 ilibaini kuwa wazazi kutojihusisha na masuala ya elimu ni tatizo kubwa linaloikabili sekta ya elimu. Lazima wazazi watengeneze mahusiano mazuri na watoto wao, walimu wa watoto wao na hata mazingira ya shule wanazosoma watoto wao.

Ipo haja ya wawakilishi wa wananchi hususani wabunge na madiwani kuendelea kutetea upatikanaji wa huduma nzuri za afya kwa vijana na kusaidia uanzishwaji wa elimu za stadi za maisha kama ambavyo Serikali imeendelea kuchukua hatua.

Ipo haja ya Serikali kuendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaume wote wanaohusika kuwabebesha ujauzito wanafunzi mashuleni sanjari na kuongeza nguvu katika ujenzi wa mabweni ya wanafunzi ili kuwaepusha na vishawishi wanapokuwa nje na maeneo ya shule.

Ipo haja ya kuwachukulia hatua kali za kisheria walimu wote wanaohusika kufanya vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike mashuleni ikiwemo kuwalazimisha kufanya ngono ili wawafaulishe mitihani yao.

Ipo haja ya kuendelea kutoa elimu kwa vijana kuhusu madhara ya mimba za utotoni ili kuongeza kasi ya kujitambua kwa watoto wa kike.

Ipo haja ya wazazi kuendelea kutoa Elimu ya malezi kwa watoto wao. Lazima turudi kwenye Utamaduni wa kuwawajibisha watoto wetu pindi wanapokuwa wamekiuka maadili na taratibu za jamii hususani kwenye masuala ya kuanza ngono katika umri mdogo.

Kufanya hivyo ni kuongeza haja ya kuendelea kumuunga Mkono Mhe. Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli katika juhudi anazozifanya za kuongeza Thamani ya Utu wa kila mtanzania hususani watoto wa kike mashuleni.

Share:

1 comment:

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com