Jovina Bujulu-MAELEZO
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea
nchini (TFRA) imeandaa kanuni za mfumo wa manunuzi ya mbolea kwa pamoja
ili kuongeza upatikanaji na kupunguza bei ya mbolea kwa wakulima.
Mfumo huo utasaidia kuimarisha
usambazaji wa mbolea ambapo wadau watapata mbolea kwa ushindani na
utawawezesha wafanyabiashara wadogo kukua na kushiriki katika biashara
ya mbolea na kuimarisha mtandao wa usambazaji hadi ngazi ya mkulima.
Aidha, mfumo huo utadhibiti bei
ya mbolea iwapo kutajitokeza ongezeko lisilo na sababu na utaongeza
ufanisi wa kudhibiti mbolea kutoka nje ya nchi kwa kuingiza mara chache
kwa kiwango kikubwa.
Akiwasilisha bajeti ya makadirio
ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka
2017/2018, Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo Dkt. Charles Tizeba
amesema kuwa Mamlaka hiyo ina jukumu la kusajili mbolea na kutoa vibali
kwa makampuni na mawakala wa mbolea nchini.
Dkt. Tizeba ameongeza kuwa
Mamlaka hiyo itakuwa na jukumu la kudhibiti soko lake pamoja na kutoa
ushauri wa kitaalamu kwa Serikali na Taasisi zinazojishughulisha na
masuala ya kilimo na mbolea.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka hiyo Bwana Lazaro Kitandu, kabla ya kuanzishwa
Mamlaka hiyo kulikuwa na matatizo ya utunzaji na utumiaji wa mbolea
yenye kiwango kinachotakiwa na hivyo kufanya kuwepo kwa tatizo la
upatikanaji wa mbolea bora ambayo inakidhi viwango.
Kaimu Mkurugenzi huyo ameeleza
kwamba, Mamlaka hiyo imeundwa mahsusi kwa ajili ya kuangalia mwenendo wa
bidhaa hii ya mbolea kuanzia inapotengenezwa, kusafirishwa hadi
kutumiwa na wakulima.
Zaidi ya hayo Bwa. Kitundu
amesema kuwa Mamlaka inafanya ukaguzi katika maghala, maduka na Mawakala
wa mbolea hapa nchini ili kuhakikisha kuwa mbolea waliyonayo ina ubora
unaotakiwa kabla ya kuwauzia wakulima.
Akizungumzia namna Mamlaka
inavyofanya kazi ya udhibiti, Bw. Kitundu alisema kuwa mbolea
inapoingizwa nchini wanapima Sampuli katika maabara zilizopo katika
vituo vya utafiti wa kilimo vya hapa nchini.
Alizitaja maabara hizo kuwa ni
pamoja na vituo vya TPRI na Seliani vilivyopo mkoani Arusha, Mlingano
Tanga, Sokoine Morogoro, na maabara ya TORITA iliyopo Tabora ambayo ni
maalumu kwa ajili ya kupima mbolea ya tumbaku.
“Kabla ya kuwafikishia wakulima,
wafanyabiashara na wakala wanawajibika kufikisha sampuli za mbolea
katika maabara ambazo zipo karibu nao” amesema Bw. Kitandu.
Amefafanua kwamba, tasnia ya
mbolea hapa nchini bado ipo chini kwani asilimia 90 ya mbolea yote
inayotumika inatoka nje ya nchi ambapo makampuni na mawakala binafsi
ndio waingizaji wa mbolea hiyo .
Makampuni yanayoleta mbolea hapa
nchini ni Pemium Agrochem Ltd, ETG Inputs Ltd, TFC, DRTC Trading
Company, STACO, Elia-gro Company Ltd, TATA Africa Holdings, Mohamed
Enterprises (T) Ltd, Yara (T) Ltd, Swiss Singapore Overseas Enterprises
Ltd na Rubuye Agro-business Company Ltd.
Makampuni mengine ni Agrichem
Africa (T), Bajuta International (T) Ltd, Flue and Dark Tobacco Company,
Crop Care (T) Ltd,One AcreFund , Nutri care (T) Ltd na Ludod Agro
Industy Comp Ltd.
Aidha, Bwana Katandu amesema
kuwa hapa nchini kiwanda cha mbolea kipo Minjingu mkoani Manyara na
kinazalisha mbolea kwa matumizi ya ndani na mara chache kinazalisha kwa
ajili ya kupeleka nje ya nchi ambapo mwaka 2016 kiwanda hicho
kilisafirisha kiasi kidogo cha tani 74,000 nje ya nchi.
Akizungumzia namna ambavyo
wakulima wanaweza kujua kuwa mbolea ipo chini ya kiwango, Bw. Kitandu
alisema kuwa wanapaswa kuangalia kibandiko kilichopo katika mfuko wa
mbolea ambacho kinaonesha muda wa mwisho wa matumizi na virutubisho
vilivyomo katika mbolea hiyo.
Sababu zinazofanya mbolea kuwa
chini ya kiwango kuwa ni pamoja na kuwekwa juani, kuwekwa katika ghala
linalovuja, kuwekwa mahali pa wazi na kufungua mifuko ya mbolea na kuuza
kwa ujazo mdogo hivyo kusababisha kupoteza virutubisho.
Bwana Kitandu amesisitiza kuwa
mtu yoyote anayebainika kuchakachua mbolea au kuuza mbolea ambayo ipo
chini ya kiwango atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na
kunyang’anywa leseni, kutozwa faini na kutumikia kifungo jela.
Ameongeza kusema kuwa tangu
Mamlaka ianze kufanya kazi, tatizo la mbolea zisizokuwa na kiwango na
zilizochakachuliwa limekwisha na amewataka wakulima kutokuwa na
wasiwasi na mbolea wanayotumia kwa sasa.
“Tunafanya kazi kwa kushirikiana
na Halmashauri zote hapa nchini, hivyo tuna wataalamu kila kijiji,
wilaya, na mikoa. Wataalamu hawa wanashiriki katika kutoa elimu kuhusu
matumizi sahihi ya mbolea inayoendana na ukubwa wa eneo” amesema Bw.
Kitandu.
Akizungumzia mbolea zinazotumika
kwa wingi hapa nchini, Bw. Kitandu amezitaja kuwa ni mbolea aina ya DAP
ambayo ni ya kupandia na UREA ambayo ni ya kukuzia.
Pamoja na ktumika mbolea hizo,
Bw. Kitundu amesema kuwa mbolea hizo zinatumiwa kwa zaidi ya asilimia 50
ya mbolea zote. Aina nyingine ya mbolea zinazoingizwa na zinazotumiwa
kutoka nje ya nchi ni pamoja na NPK, CAN, SA, MOP, TSP, Biofertilizer na
mbolea za maji aina ya “foliar”.
Kuhusu mahitaji ya mbolea hapa
nchini, Bw. Kitandu amesema kuwa yameongezeka tofauti na miaka 10
iliyopita ambapo mwaka 2016 jumla ya tani 380 ziliingizwa na inakadiria
kuwa mwaka huu mbolea itakayoingizwa nchini itafikia tani 400 hadi 450.
Taarifa ya Mpango wa Taifa wa
miaka mitano 2016/2017 hadi 2020/2021 inaonyesha kuwa sekta ya kilimo
ambayo ni tegemeo kubwa la Watanzania walio wengi imeajiri takribani
asilimia 66.9 ya Watanzania wote na inachangia asilimia 23 ya pato la
Taifa.
Ni dhahiri uwepo kwa mamlaka ya
udhibiti wa mbolea utachochea kukuza kilimo chenye tija kwa kuongeza
wingi wa mazao yaliyo bora na kuinua uchumi wa nchi.
Mamlaka ya Kudhibiti Mbolea ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 9, ya Mwaka 2009, na ilianza kufanya kazi rasmi mwaka 2012.
0 comments:
Post a Comment