IGP Simon Sirro
Na Katuma MasambaJESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa watatu wa ujambazi pamoja na silaha mbili na risasi katika majibizano ya risasi na askari.
Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya alisema jana kuwa, maeneo ya Kigogo Luhanga, polisi walifanikiwa kuwakamata majambazi wawili wakiwa na bunduki aina ya Shotgun.
“Askari polisi wakiwa doria waliziona pikipiki mbili zilizokuwa na watu wawili kila moja na hivyo kuanza kuzifuatilia, baadaye majambazi walibaini walifuatiliwa na ndipo walipoamua kurusha risasi kwa askari hao,” alisema Mkondya.
Alisema katika majibizano hayo, askari hao walijibu mapigo na hatimaye kuwajeruhi watu wawili. Aidha, uchunguzi wa awali ulionesha majambazi hao walihusika katika tukio la mauaji maeneo ya Makuburi.
Katika tukio jingine, Mkondya alisema, Juni 22, katika maeneo ya Mabibo Mpakani, polisi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa raia wema, walifanikiwa kukamata silaha aina ya Pistol CZ iliyofutwa namba zake.
Alisema askari walifuatilia watu wawili waliowatilia shaka na watu hao walipobaini kuwa wanafuatiliwa, walitoa silaha hiyo na kuanza kuwarushia askari risasi na katika kujibizana askari walimpiga risasi moja kwenye mkono wa kushoto mtu aliyefahamika kwa jina la Mmari Lyimo (28) mkazi wa Chamazi na kukamata silaha hiyo.
Jeshi hilo pia limefanikiwa kukamata injini 23 za pikipiki na watuhumiwa watatu waliohusika katika kuiba injini hizo, ambazo zilikuwa 50 katika kampuni ya Tanzania China Trade and Tourism Development Limited .
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Soteri Kipesha (24) mkazi wa Kimara na dalali wa magari, Mbarak Nuhu (26) mfanyabiashara na mkazi wa Manzese na Shaaban Ramadhani (27) mlinzi na mkazi wa Vingunguti.
0 comments:
Post a Comment