METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, June 24, 2017

Kortini kwa ‘kutapeli’ mahujaji 119

Na Fransisca Emmanue
 
MKURUGENZI wa Kampuni ya Travel House Global, Sojan Varghese amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya kujipatia Dola za Marekani 88,012 (Sh milioni 184.8) alizopewa kwa ajili ya mahujaji zaidi ya 119 wa Chama cha Karismatiki Katoliki Tanzania.

Varghese alidaiwa kuchukua fedha hizo kutoka kwa John Ngotty kwa lengo la kukata tiketi za ndege kwa mahujaji hao waliokuwa wakitaka kusafiri kuelekea nchi za Roma, Italia na Israeli kwa ajili ya hija.

Akisoma mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Wakili wa Serikali, Adolf Mkini alidai kuwa Desemba 23, 2016 maeneo ya ofisi za Kampuni hiyo zilizopo mtaa wa Jamhuri, mshitakiwa alijipatia Dola za Marekani 7,012 kutoka kwa Ngotty fedha ambazo ni kwa ajili ya nauli ya kupata tiketi ya ndege kwa Wakarismatiki 119 kutoka Dar es Salaam kwenda Roma nchini Italia na Israel.

Pia alidai, Desemba 23, mwaka jana, maeneo ya ofisi hiyo, mshitakiwa alijipatia Dola 9,500 kupitia hundi namba 000005 kutoka kwa Ngotty kwa ajili ya kuwakatia tiketi ya ndege kwenda nchi hizo.
Mkini alidai katika mashitaka ya tatu kuwa, Januari 11, mwaka huu maeneo ya ofisi hizo, Varghese alijipatia Dola za Marekani 9,500 kutoka kwa Ngotty kwa lengo la kutumika kununulia tiketi za ndege kwa wanachama wa Wakarismatiki 119 kwenda hija Roma na Israel.

Katika mashitaka ya nne, mshitakiwa alidaiwa Januari 11, mwaka huu, alijipatia Dola za Marekani 9,500 kwa hundi namba 000008 kutoka kwa Ngotty. Aidha, inadaiwa Januari 31, mwaka huu, Varghese alijipatia Dola za Marekani 37,500 kutoka kwa Ngotty kwa ajili ya nauli ya tiketi ya ndege kwa wanachama 199 wa Karismatiki.

Mkini alidai, Aprili 12, mwaka huu, maeneo ya Ofisi za kampuni yake, alijipatia Dola za Marekani 15,000 kutoka kwa Ngotty kwa ajili ya kununulia tiketi kwa wanachama 119 wa Karismatiki waliokuwa wanakwenda hija nchi za Roma na Israeli.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com