Wanafunzi wa Sekondari ya Wasichana. Rais Magufuli amesema hataruhusu
katika utawala wake wanafunzi watakaobeba ujauzito kuendelea na masomo
SHIRIKA la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, kambi ya upinzani na
wadau wengine wameunga mkono msimamo wa Rais John Magufuli kuhusu
wasichana wanaopata mimba na kujifungua kutorejea shuleni kuendelea na
masomo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, wadau hao wamesema
wanakubaliana na Rais Magufuli kwa masimamo wake kama mzazi makini na
mwenye uchungu na watoto.
Mkurugenzi wa Prolife-Tanzania, Emil Hagamu alisema anaunga mkono
kauli na msimamo wa Rais kwa kuwa ni mzuri na pamoja na mambo mengine,
unawasaidia wazazi, walezi na viongozi wa dini kuimarisha malezi na
maadili kwa watoto.
“Namuunga mkono Rais wetu; hili lilikuwa miongoni mwa malalamiko
makubwa ya watu kupinga mimba za utotoni kwa sababu watoto hao bado
wadogo, hivyo, hawapaswi kukubali kushiriki vitendo wanavyojua vinakiuka
maadili ya jamii katika familia, shule na hata dini zao,” alisema
Hagamu.
Akasisitiza, “Kuruhusu watoto wakipata ujauzito waende wajifungue
kisha warudi shuleni, utakuwa umeruhusu vitendo vya ngono kwa sababu ni
watoto.
“Unajua mtoto wa shule anapopata mimba, huwa na msongo na matazamio
ya kuwa mama na kwamba tafiti nyingi zilizofanywa kuhusu watoto
waliopata mimba shuleni zinaonesha hawana matokeo mazuri shuleni,”
alisema.
Kwa mujibu wa Hagamu, kauli ya Rais ikizingatiwa sambamba na maadili
yanayofundishwa katika jamii na dini mbalimbali, ni wazi hata vifo na
madhara yanayotokana na utoaji mimba vitapungua.
Alisema lazima maadili ya nchi na jamii yazingatiwe sambamba na
kuwachukulia hatua kali zaidi wanaosababisha ujauzito kwa watoto wa
shule na wenye umri wa chini ya miaka 18.
“Lazima turejeshe maadili yetu ya zamani ili watoto wetu wawe na
nafasi ya kuzingatia masomo na wafanye vizuri zaidi katika masomo yao
ili baadaye watumikie vema taifa, dini na familia zao,” alisema.
Mkurugenzi huyo wa Prolife alikwenda mbali na kusema, “Namshauri Rais
atazame hata mfumo wa sasa wa elimu ambapo wanafunzi kuanzia darasa la
tano wanafundishwa elimu inayohusisha mambo ya ngono kwa kuwa elimu hiyo
kwa watoto, inahamasisha watoto kujaribu na kuangamia katika magonjwa
na mimba.” “Wanasaikolojia wanasema mtoto anapofundishwa elimu inayohusu
ngono mapema, ndivyo anavyoshawishika kujaribu mapema,” alisema Hagamu.
Kwa upande wa wazazi, Emerenciana Mkony mkazi wa Dar es Salaam
alisema msimamo wa Rais umetazama mbali katika kujenga taifa la watu
adilifu na wanaozingatia wakati wa kufanya kila jambo.
“Msimamo huu wa Magufuli ni msimamo nzuri kwa sababu ikiwa watoto
wataruhusiwa kurudi shule baada ya kujifungua, maadili yatazidi
kuporomoka na mwisho wa siku taifa litakosa watu wenye nidhamu,”
alisema.
Kwa upande wake, Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo amesema kambi
hiyo haiungi mkono suala la watoto kupata mimba wakiwa shuleni.
Aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
ikiwa ni siku moja baada ya Rais John Magufuli kupiga marufuku mpango
unaopigiwa debe wa kuruhusu wanafunzi wanaobeba ujauzito wakiwa shuleni
waruhusiwe kurejea shuleni baada ya kujifungua.
“Sisi kama kambi ya upinzani ni kweli tunapinga kabisa na suala la
watoto kupata mimba kwa maana ya kufanya mapenzi, tukiweza kuboresha
elimu yetu na miundombinu ya shule zetu ni wazi tatizo hili kubwa la
mimba litaweza kuepukika na hata haya tunayojadili hayatakuwepo,”
alisema Lyimo.
Naye mmoja wa wadau wa elimu na maadili, Gladness Munuo alisema
anaiunga mkono kauli ya Rais Magufuli kwa asilimia 100 kwani ni hatua
nzuri itakayosaidia jamii kuwa na nidhamu.
“Namuunga mkono Rais, sio kwamba sitaki watoto wa kike wasome la
hasha, bali hali ilikuwa mbaya; asilimia kubwa ya watoto wa kike chini
ya miaka 18 walikuwa wanaacha masomo kwa sababu ya mimba, sasa ukisema
unaruhusu wajifungue kisha warudi shule hapo hapatakuwa na maadili tena,
bali tutazidi kuwafanya waone vitendo vya uasherati ni jambo la kawaida
hata wakiwamo masomoni jambo ambalo si kweli na ni hatari kwa ustawi wa
jamii,” alisema Munuo.
Munuo alisema jamii ikiungana kuziba mianya yote ya watoto
kujihusisha na uasherati hata wawapo shuleni, itafanikiwa kupunguza
mimba za utotoni, utoaji mimba na pia, kutakuwa na uwezekano mkubwa wa
kudhibiti ongezeko la watoto wa mitaani kutokana na wengine kuzaliwa na
mama ambao ni watoto wenzao.
Alisema nchi imekuwa ikipiga kelele kupunguza vifo vya watoto wenye
umri chini ya miaka mitano na madhara ya watoto kujifungua wakiwa katika
umri wa utoto.
Kwa mujibu wa Munuo, takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa miongoni mwa
wanaopoteza maisha katika kujifungua, ni pamoja na wanawake wenye umri
chini ya miaka 18 kwa kuwa maumbile yao hayajajiandaa kwa jukumu la
uzazi.
Alisema hali hiyo inawaweka katika hatari ya kifo wakati wa
kujifungua au baada ya kujifungua. Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana
wa Chadema (Bavicha) Tanzania Bara, Getrude Ndibalema, yeye alisisitiza
maadili tangu katika familia na elimu zaidi kutolewa ili umma uelewe
vizuri Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana
ya Mwaka 1998 zinazozuia vitendo vya ngono na mwanafunzi au mtu mwenye
umri chini ya miaka 18.
Alisisitiza kuboresha miundombinu ya elimu, maadili na usalama kwa
watoto wa kike tangu nyumbani, njiani na shuleni. Habari hii imeandaliwa
na Anastazia Anyimike (Dodoma), Ikunda Eric na Joseph Sabinus (Dar).
CREDIT: HABARI LEO
Saturday, June 24, 2017
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali...
-
Wafanyakazi wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, wakiwa wamejipanga tayari kwa maandamano katika maadhimisho ya S...
-
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akifurahia jambo pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment