METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, June 28, 2017

JPM mgeni rasmi Sabasaba, mataifa 30 kushiriki

 Rais wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli

RAIS John Magufuli atakuwa mgeni rasmi Julai Mosi katika ufunguzi wa Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayosimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) yanayoanza rasmi Juni 28 hadi Julai 8, 2017 yakishirikisha makampuni toka nchi zipatazo 30.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya maonesho hayo vya Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam jana, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage alisema maonesho ya mwaka huu yamelenga zaidi kusaidia wajasiriamali wadogo ili kuifikisha Tanzania katika uchumi wa viwanda.

Alisema: “Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Ukuzaji wa biashara kwa maendeleo ya viwanda,’ kwa sababu tunaamini biashara ndiyo inayokuza viwanda na bila kuuza hakuna ukuaji wa viwanda.
Ndiyo maana lengo la maonesho haya ni kuwapa fursa wafanyabiashara kuonesha bidhaa zao na si kuuza, ili wanapomaliza maonesho wapate wateja na fursa pana zaidi.”

Alisema kila siku ya maonesho imetengwa kwa shughuli maalumu ya kumsaidia mshiriki kujiimarisha kibiashara, zipo siku za mazungumzo baina ya wafanyabiashara, siku za kukutana wafanyabiashara wa ukanda huu wa Afrika Mashariki na siku ya kujadili bidhaa.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema banda la bidhaa za ngozi litakuwa na shughuli maalumu ya kueleza faida ya bidhaa zitokanazo na ngozi pamoja na Gereza la Karanga kueleza azma ya kutengeneza soli za viatu na kuzisambaza nchini.

Awali akimkaribisha Waziri Mwijage, Kaimu Mkurugenzi wa TanTrade, Edwin Rutageruka alisema washiriki watumie maonyesho hayo kutangaza bidhaa zao badala ya kufikiria kuuza lakini pia wabadilishane ujuzi na wafanyabiashara wa kimataifa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com