METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, June 28, 2017

HOJA NA HAJA YA MAGEUZI ENDELEVU YA KITAASISI YA  UVCCM

Na Jabiri O. Makame

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ni chombo kinachowaunganisha vijana wote nchini wanaounga mkono sera, siasa na itikadi ya Chama Cha Mapinduzi. Shabaha ya Chama Cha Mapinduzi kuunda chombo hiki ni kuwa shule ya kuandaa wanachama safi na viongozi bora wa Chama na Taifa kwa ujumla (Kanuni ya UVCCM, Toleo 2017). Kwa kuwa UVCCM ni chombo cha vijana kilicho ndani ya chama kinachoongoza serikali, matarajio ya CCM, vijana na watanzania wote ni kuona UVCCM wakati wote unakuwa mstari wa mbele katika kuongoza, kusimamia na kutekeleza shughuli zote zinazohusu vijana, kutetea maslahi ya vijana bila kujali itikadi zao za kisiasa sambamba na kuhakikisha kwamba vijana wote nchini wanaendelea kukiona Chama Cha Mapinduzi kuwa ni chama pekee kinachoweza kuongoza taifa na kudumisha umoja, amani, demokrasia na kujenga taifa imara kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni. 

Wimbi la mageuzi ya kisiasa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni ambapo nguvu ya upinzani imeongezeka nchini, inaifanya chama cha mapinduzi kubadili mfumo wake wa uongozi na Menejimenti ndani ya chama ili kuendana na kasi ya mabadiliko hayo, hivyo kujenga chama chenye taswira chanya mbele ya macho ya umma wa watanzania kama ambavyo Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe. Dr. John Pombe Magufuli, alivyotoa wito alipokuwa anawahutubia wajumbe wa mkutano mkuu wa ccm ya kwamba;

“Suala la kuimarisha utendaji wa chama ni muhimu sana. Kama alivyokuwa akisema Baba wa Taifa letu Mwalimu Nyerere kuwa, Chama legelege huzaa Serikali legelege. Nitashirikiana nanyi kujenga Chama madhubuti chenye uwezo wa kuisimamia vizuri Serikali ili itekeleze ipasavyo majukumu yake, ikiwezekana tutapitia upya Katiba na Kanuni zetu ili kukidhi mazingira ya sasa na kuweza kuwatumikia wananchi ipasavyo”.

Katika jitihada hizi za kuimarisha chama chetu jumuiya za chama; UWT, WAZAZI na UVCCM zinabeba dhamana kubwa katika kukifanya chama cha mapinduzi kufikia malengo yake.

Aidha, UVCCM umebeba wajibu wa ziada kwa chama na taifa letu ukilinganisha na jumuiya zingine, kutokana na ukweli kwamba;

Mosi, umoja wa vijana una wanachama ambao wana sifa ya kuwa katika jumuiya zote za chama,

Pili, imani ya watanzania kwa viongozi vijana ni kubwa ukilinganisha na imani waliyonayo kwa viongozi wa rika zingine.

Tatu, kundi la vijana katika Taifa letu ni kubwa kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 pamoja na takwimu za tafiti mbalimbali za hivi karibuni.

Vilevile vijana ndiyo kundi linalokabiliwa na changamoto lukuki kama vile ukosefu wa ajira, biashara ya madawa ya kulevya, hali ngumu ya kiuchumi, matatizo ya mikopo ya elimu ya juu pamoja na changamoto zingine, na mwisho historia inaonesha kwamba nguvu ya vijana ni kubwa na haijawahi kushindwa pale wanapoungana na kutaka mabadiliko katika jamii.
                            
Ili kutekeleza wajibu huu kwa chama na taifa, UVCCM hauna budi kujenga uwezo imara wa ndani na nje wa taasisi (Strong internal and external institutional capacity) kwa kufanya mageuzi ya kitaasisi ili kuongeza uwezo wa kutekeleza majukumu yake. Uwezo wa ndani wa taasisi unatokana na:-

Uchumi imara wa taasisi unaotokana na uwezo wa jumuiya kubuni vyanzo vya mapato, kusimamia vyema vyanzo hivyo vya mapato, matumizi sahihi ya rasirimali za taasisi na mfumo imara wa kisera na kisheria wa udhibiti wa mali za jumuiya. Ni kujijengea uwezo wa kirasirimali, kunzia ngazi ya Taifa, mikoa, wilaya, kata na matawi na  kuzielekeza rasirimali  hizo katika ujenzi wa taasisi kwa manufaa ya vijana.

Vilevile uwezo wa ndani wa taasisi unategemea mifumo imara ya utawala na usimamizi (stable administrative and management principles) kama vile taratibu bora za uwajiri, kupandisha vyeo, kutatua kero za watumishi, kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi, kuwa na mipango ya muda mrefu na muda mfupi, kuitekeleza na kufanya tathmini ya utekelezaji wake, kuwapa motisha wale wanaofanya vizuri na kuwasadia kubadilika wale wasiofanya vizuri.

Kuwa na viongozi wenye sifa na wanaoweza kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ubunifu, uzalendo, uaminifu na uadilifu ulitukuka, huku wakiweka mbele maslahi ya taasisi yao kuliko maslahi yao binafsi. Viongozi hao lazima waelewe dira (vision) ya taasisi, wawe na uwezo wa kujenga timu bora ya wasaidizi wao, wasaidie wasaidizi hao kuielewa dira ya taasisi, wawasaidie kuandaa mikakati ya kuifikia dira hiyo na wawe na uwezo wa kusimamia utendaji ili kuifikia dira hiyo.

Uwezo huo imara wa ndani ya taasisi hatimaye hujenga uwezo imara wa nje ya taasisi kwa maana uwezo wa UVCCM kuwa na ushawishi ndani ya chama na Taifa kwa ujumla katika masuala yanayogusa maslahi ya vijana, kama vile sera za taifa, sheria na maamuzi mbalimbali yanayofanywa na vyombo vya maamuzi yanayogusa mustakabali wa taifa kwa ujumla. Hii inatokana na ukweli kwamba sauti ya UVCCM ina nguvu ukilinganisha na sauti za jumuiya zingine za vyama vya siasa na taasisi zingine za vijana.

Kama Chama cha Mapinduzi ni baba, mama, babu na bibi wa vyama vyoye vya siasa barani Afrika, basi Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi unatazamiwa kuwa kaka na dada wa jumuiya na taasisi zote za vijana Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Hivyo, taasisi hii inapaswa kuwa na uwezo wa kuongoza taasisi zingine za vijana katika kupigania, kutetea na kuwa chimbuko la vuguvugu la masuala ya vijana ndani ya Tanzania, katika jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika. Hii ndiyo kazi iliyofanywa na TANU Youth League wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, na hii ndiyo kazi inayopaswa kufanywa na UVCCM  katika kipindi hiki ambacho ajenda kuu siyo ukombozi wa kisiasa tena, bali ni ukombozi wa kiuchumi ambapo kwa kiasi kikubwa vijana ndiyo nguvu kazi ya kufanikisha agenda hii muhimu.

Katika kufanikisha adhma hii sambamba na kuitikia wito wa mageuzi uliotolewa na Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa Mhe. John Pombe Magufuli ambaye ameonesha dhamira ya dhati ya kuleta mapinduzi ya kweli ndani ya chama na serikali, itakumbukwa mwezi Agosti 2016 kupitia ukurasa wangu wa Facebook @Jabiri Omari niliandika makala yeye kichwa cha habari “Azma ya Kuwasilisha Hoja Binafsi ya Mageuzi ya Kitaasisi ya UVCCM”  (Fungua hii link kuisoma,
https://m.facebook.com/story.php?story_fbid=1175698035825904&id=100001571569676 ).

Katika makala hiyo nilieleza kwa muhtasari hoja yangu binafsi ambayo niliomba kuwasilisha kwenye kikao cha Baraza Kuu la Vijana Taifa cha tarehe Agosti 13, 2016, lakini ilikosa nafasi ya kuingizwa kwenye ajenda za kikao kutokana na sababu ambazo hazikuweza kuzuilika, hivyo nilikabidhi kwa uongozi wa UVCCM kwa ajili ya kufanyiwa kazi na kupewa nafasi katika vikao vilivyofuata.

Homa ya Mageuzi ya Kitaasisi ilianza kupata ahueni baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Mh. Dr. John Magufuli, iliyokaa katika Mkutano wake wa mwenzi Desemba 2016, ambacho kilipuliza rasmi parapanda la mageuzi ya Chama na Jumuiya zake  na baadaye kupitishwa na Mkutano Mkuu Maalum wa CCM wa Machi 12, 2017.

Nilipata faraja kuona kwamba Mageuzi haya yaligusa baadhi ya maeneo ambayo nilipendekeza katika Hoja yangu Binafsi yakiwemo mfumo wa usimamizi wa Mali za jumuiya ambayo kwa sasa mali zote zitakuwa chini ya baraza la udhamini la chama, na mfumo wa ajira ambapo ajira zote za jumuiya zipo chini sekretarieti ya CCM.

Ili kuendana na mageuzi ya chama UVCCM ulilazimika kufanya mabadiliko ya kanuni ili kutekeleza maelekezo ya chama ambapo mabadiliko makubwa yalikuwa kupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi kwa kupunguza idadi ya vikao, idadi ya wajumbe katika vikao mbalimbali na kuingiza Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu kuwa chini ya UVCCM.

Mabadiliko haya hayaondoi ukweli wa mahitaji ya mageuzi endelevu ya UVCCM ili kukidhi haja na matakwa ya chama na hatimaye kuifikia kilele cha mafanikio ya ujenzi wa taasisi bora ya Vijana barani Afrika.

Hoja yangu ni kwamba, pamoja na mabadiliko yaliyofanyika, taasisi hii bado inahitaji kuimarisha mifumo yake ya ndani ya uendeshaji wa taasisi ambayo ndiyo msingi wa kuimarisha taswira ya nje ya taasisi yetu, kwani:-

Kwa upande wa mali za jumuiya, pamoja na hatua muhimu ya kuziweka mali zote chini ya baraza la wadhamini la chama, bado UVCCM utakuwa na wajibu wa kuendelea kuhakikisha kwamba taasisi hii inajitegemea kimapato kuanzia ngazi ya Taifa hadi tawi na kwamba mapato yake yanatumika kuimarisha taasisi kwa maslahi ya vijana wa CCM na Taifa kwa  ujumla.

Pamoja na jukumu la kuajiri watumishi kuwa chini ya Sekretarieti ya Chama, bado UVCCM utabaki kuwa na jukumu la  kujua unahitaji watumishi wa aina gani sambamba na kuwa msimamizi mkuu wa rasirimali watu hawa, hivyo kuwa na wajibu wa kuandaa mfumo bora wa Menejimenti ya rasirimali watu kutokana na ukweli kwamba miongoni kwa rasirimali zote za taasisi yeyote ile rasirimali watu ndiyo moyo wa taasisi.

Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu kwa sasa ipo chini ya UVCCM. Mimi ni miongoni mwa vijana walioshiriki katika hatua za mwanzo kabisa za mjadala wa kuandaa muongozo wa uendeshaji wa Shirikisho la wanachama wa CCM Vyuo Vikuu Tanzania.

Hivyo, natambua umuhimu wake na nafasi yake katika kuandaa makada wasomi na viongozi wa Chama na Taifa. Kimuundo ni idara kama zilivyo idara zingine za UVCCM lakini kiutendaji ni kama taasisi ambayo inahitaji mfumo madhubuti wa usimamizi na uendeshaji ili kuhakikisha kwamba inakidhi haja ya kuanzishwa kwake.

Vilevile UVCCM unabakia kuwa chombo au mamlaka ya kufanya uteuzi wa baadhi ya nafasi nyeti hasa wakuu wa idara, hivyo kuwa na wajibu wa kuandaa vigezo vilivyokubalika vya uteuzi ili kuepusha maslahi binafsi kujipenyeza ndani yake, lengo likiwa ni kuhakikisha kila idara inatimiza wajibu wake ipasavyo.

Ibara ya 98 ya Kanuni ya UVCCM, Toleo la 2017 inaainisha Miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa taasisi ikiwemo muongozo wa uchaguzi wa uvccm (ni vyema iwe “uchaguzi na uteuzi”), kanuni za usalama na maadili, muongozo wa taratibu za utumishi, muongozo wa taratibu za Fedha, muongozo wa uendeshaji wa Vyuo na Vyuo Vikuu, na muongozo wa chipukizi. Maandalizi, usimamizi na utekelezaji wa miongozo hii inahitaji utayari wa menejimenti (management will), utashi wa kisiasa, uelewa wa umuhimu wake, sambamba na dhamira ya dhati.

Kwa kuzingatia misingi hii, hoja na haja ya Mageuzi Endelevu ya Kitaasisi bado ina mashiko (relevant) ili kujenga taasisi inayoakisi kasi ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa JMT Dr. John Pombe Magufuli, na Makamu wake, Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein.

HITIMISHO

Nimeamua kucharaza wino huu, ili kueleza bayana nini hatma ya hoja ambayo niliibua siku za nyuma na kuweka bayana kwa vjana wenzangu kwa nini taasisi yangu inahitaji kuendelea kufanya mageuzi ya kitaasisi. Aidha, mimi na wenzangu ambao tumejitahidi kadri ya uwezo wetu kuifikisha hapa ilipofikia, yawezekana tumefanya vizuri au hatujafanya vizuri, lakini bado tunatamani kuiona taasisi hii katika siku za usoni ikiwa bora zaidi  ya hapa tunapoiacha, hivyo iendeleze jukumu lake la kuoka viongozi bora wa Taifa letu kama vile tulivyoshuhudia na tunavyoshuhudia baadhi yao wakiwemo Jakaya Mrisho Kikwete, Mohamedi Seif Khatibu, William Lukuvi, Mrisho Gambo, Mboni Mhita, Anthony Mavunde, Anthony Mtaka, Issa Gavu, Hamad Masauni, Paul Makonda, Ruge Mutahaba, Nehemiah Msechu, Erick Shigongo, Nape Nnauye, Ridhiwani Kikwete, Elias Masala, Dr. Emmanuel Nchimbi, Martin Shigela, Sixtus Mapunda na wengine wengi ambao aidha wamewahi kuwa viongozi wa taasisi hii au wamewahi kufanya kazi za taasisi hii nyeti.

Kadhalika, mimi ninaamini kwamba ukiwa kiongozi na ukahitaji fikra, falsafa na mawazo yako yasaidie taasisi yako na kizazi cha sasa na baadae basi ni sharti uyaweke mawazo  yako kwenye maandishi kama ambavyo viongozi wengi walivyowahi kufanya wakiwemo Hayati Mwalimu Nyerere, Nelson Mandela, Barack Obama na wengine wengi. Katika makala hii nimejitahidi kuandika kwa ufupi sana lakini katika siku zijazo panapo majaaliwa ya Mwenyezi Mungu nitaandika Kitabu kuhusu Taasisi za vijana za vyama vya siasa ili iwe rejea kwa kizazi cha sasa na baadae. 

Miaka mitano kama mjumbe wa baraza kuu si haba, nimejifunza mengi na nimeifahamu taasisi hii kiunagaubaga hivyo, wakati tukielekea ukingoni, ni wajibu wangu kutoa uchambuzi wa kina na kurithisha haya maarifa niliyonayo kwa wengine ili yawe msaada kwa vijana wenzangu ambao wanawaza kuja kuitumikia taasisi hii katika siku za usoni.

Kuhusu Uchaguzi unaoendelea ndani ya Chama na Jumuiya zake, Chama kupitia kwa Katibu Mwenezi Taifa ndugu Humphrey Polepole kimetoa maelekezo na miongozo wa aina ya viongozi wanahitajika kwa mustakabali wa Chama chetu. Sina shaka kwamba kupitia uchambuzi huu, vijana wenzangu wamepata picha ya aina ya taasisi yetu na kwamba tunahitaji aina gani ya viongozi ambao watasaidia kukidhi matarajio ya Chama na matarajio ya vijana wa Taifa letu.

Niwahamasishe vijana wenzangu kujitokeza kuchukua fomu za kugombea katika nafasi mbalimbali za  Chama na Jumuiya ili wawe sehemu ya kuongoza mageuzi ya Chama na hasa mageuzi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi.

Mwandishi wa Makala hii ni Mjumbe wa Baraza Kuu UVCCM Taifa kutoka mkoa wa Lindi, Mchambuzi wa Masuala ya Siasa na Uongozi, na Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili (masters) ya Uongozi na Menejimenti, Katika Chuo Kikuu Mzumbe.

Anapatikana kwa: Barua Pepe; jabirimakame@ymail.com
Simu: +255 753276347

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com