MWENYEKITI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku
Na John Nditi, Morogoro
MWENYEKITI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amewataka wasomi nchini kupunguza lugha ya ugomvi baina yao kuhusu hatua zinazochukuliwa na Rais John Magufuli juu ya ukombozi wa awamu ya pili ya kiuchumi.
Badala yake, washirikiane na washauriane na kuwa kitu kimoja kutetea na kulinda rasilimali za taifa. Butiku alisema hayo juzi kwenye kongamano la kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli, lililoandaliwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA).
Alisema, Rais Magufuli ameanzisha awamu ya pili ya ukombozi wa kiuchumi, hivyo watanzania wote hatuna budi kumuunga mkono katika mapambano hayo ya kiuchumi. “Sasa tumeingia katika ukombozi wa awamu ya pili ya kiuchumi na ukombozi huu umeanzishwa na Rais wetu Dk John Magufuli kutokana na ujasiri wake na kujiamini, hivyo ni vyema watanzania wote tumuunge mkono, tuwe nyuma yake katika jambo hili,” alisema Butiku.
Aliwataka vijana wasomi kupunguza lugha ya ugomvi baina yao kwenye suala hilo, bali washauriane na kuwarudisha kundini wenzao wenye mitazamo tofauti na lugha moja ya kutetea na kulinda rasilimali za taifa.
Mwenyekiti wa Mviwata, Veronica Sophu alisema wakulima wanaunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kupigania rasilimali za nchi hususani madini na kuwatetea wananchi wanyonge.
Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe alisema wakulima wameonesha moyo wa uzalendo kwa kuonesha hisia zao dhidi ya Rais Magufuli kwa kumuunga mkono kwa vitendo. Kongamano hilo linashirikisha wanachama zaidi ya 1,000 kutoka mikoa ya Morogoro, Arusha, Iringa, Manyara, Kilimanjaro na Dodoma.
0 comments:
Post a Comment