Na Debora Charles
Kwanza kabisa napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa dhati Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya pamoja na Serikali yote ya Awamu ya Tano katika mchakato wa kuimarisha Uchumi wa Viwanda unaotupa Dira ya kutufikisha kwenye uchumi wa kati. Hakika juhudi hizi zimekuwa tunu kwa Taifa zima kwa sababu zimechochea kwa kiasi kikubwa dhana ya SIASA SAFI na UONGOZI BORA wenye tija kwa MAENDELEO ya Taifa letu la Tanzania.
Ipo haja kama taifa kuendelea kufahamu kwa kina na kuamini kuwa tupo katika kipindi cha mpito chenye mrengo wa kuziba mianya yote ya wapiga dili, wala rushwa na wabadhilifu wa mali za umma kwa lengo la kuleta maendeleo ya Taifa zima. Lazima tuendelee kuwa wavumilivu, tutimize wajibu wetu na tujivunie faida za utawala tulionao kwa kuuishi uzalendo, uadilifu na maadili ya Taifa letu ili kwa pamoja na kwa umoja wa vizazi vyetu vya sasa na baadae tuweze kushiriki kikamilifu katika kufurahia matunda ya nchi yetu.
Tunayosababu ya kufanya KAZI KWA BIDII, kukubali KUWAJIBIKA na kuwa tayari KUJIENDELEZA sisi wenyewe. Tukijiendeleza tutapanua mtazamo wa fikra katika kutambua nini haswa tunapaswa kufanya, kwa nini, kwa namna gani na kwa hatua zipi za kukanyaga katika njia tunazozipita. Tutatambua wajibu wetu, Tutaitambua nchi yetu; historia yake tulipotoka, tulipo na tunapokwenda. Tutakuwa na uwezo wa kujenga hoja zinazotekelezeka, tutatambua shida zetu, njia za kuzitatua na njia halali ya kutoa mapendekezo kwenye mambo tunayoazimia tunapokuwa tukijadiliana.
Serikali imeanza ujenzi wa Reli ya Kati (Standard Gauge), imenunua ndege ikiwa ni pamoja na kusaidia kukuza sekta ya utalii kutoka watalii wachache waliokuwa chini ya 1,500,000 mpaka 2,000,000 au zaidi. Imeimarisha barabara, inapanua bandari za Dar es Salam, Tanga na Mtwara, inaendelea na ukarabati wa meli zilizopo na mipango ya kununua meli mpya kwa ajili ya kutumika kwenye Ziwa Viktoria na ziwa Tanganyika.
Kadharika imeendelea kurahisisha mfumo wa kukusanya na kuongeza mapato ya Taifa (mfumo wa kielektroniki) mfumo ambao ufanisi wake hauhitaji nguvukazi kubwa na unaminya mianya ya wakwepa kodi. Imeendelea kuimarisha miradi mikubwa ya umeme unaotokana na gesi ukiwemo mradi wa Kinyerezi I ambao unatanuliwa uwezo wake kufikia Megawati 335 kutoka Megawati 150 na Kinyerezi II wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 240. Kadharika vijiji vingi kufikiwa na umeme kupitia wakala wa umeme vijijini (REA), Elimu bure msingi mpaka kidato cha nne ambapo mpaka sasa kila mwezi zinatengwa bil. 18.77 na mengine mengi.
Katika kuimarisha uchumi hususani kilimo uvuvi na mifugo, madini, misitu na biashara ambazo nazo zinaajiri watanzania walio wengi, Serikali imeedelea kuiona haja ya kukuza sekta ya viwanda.
Takwimu zinaonyesha kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani takribani viwanda 2169 vimesajiliwa vikiwemo vya mbolea, saruji, chuma na usindikaji wa mazao.
Hakika hizi ni hatua kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuchakata uchumi wa kati. Lakini kama Taifa, lazima tutambue kuwa maendeleo hayaletwi na Serikali pekee isipokuwa na juhudi zetu wenyewe za mtu kwa mtu, kikundi kwa kikundi hatimaye kwa nchi nzima. Taifa lenye maendeleo lina watu wanaotumia muda mwingi kuzalisha, kutafakari namna bora ya kujiimarisha kiuchumi na kuthubutu kutenda.
Takwimu za National Bureau of Statistics (NBS) zinaonyesha kuwa nguvukazi ya nchi yetu ya Tanzania (Working age of National) ya kuanzia miaka 15 na kuendelea ni takribani watanzania Mil. 23.2 yaani hawa ni watu wenye uwezo wa kufanya kazi na kuliingizia kipato taifa letu kwa ujumla. Lakini asilimia sabini na moja 71% ya watu (nguvukazi) hawa wanatumia muda wao katika masuala ambayo hayana tija ikiwa ni pamoja na kuamka asubuhi na kwenda kijiweni kujadili mpira, kuchati watsup, kujadili siasa, wapiti njia n.k.
Watafiti waligundua kuwa moja ya sababu kubwa ya umaskini wa nchi yetu ya Tanzania unatokana na KUSHINDWA KUWAJIBIKA ipasavyo. Yaani leo hii mzazi wa kitanzania akiona binti/kijana wake ambaye hana kazi ameleta pesa nyumbani hachukui hatua yoyote ya kumuwajibisha ikiwa ni pamoja na kutaka kujua ni wapi hasa pesa hizo zimetoka, na kwanini, badala yake huzifurahia na kuziingiza kwenye bajeti ya matumizi ya kila siku. Lakini pia asilimia kubwa ya watu wamekuwa wakieleza kwamba tafsiri sahihi ya ajira ni kuhudhuria ofisini peke yake na kulipwa mshahara mwisho wa mwezi na si vinginevyo jambo ambalo linakiuka misingi ya uwajibikaji.
Uwajibikaji ni pamoja na kujua jambo unalopaswa kulifanya ikiwemo uzalishaji, kujua miiko na maadili ya uraia wako, kujua taratibu za nchi, kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu nchi yako n.k kisha KUTEKELEZA kwa kufuata sheria na miogozo iliyopo.
Kuwajibika ni pamoja na kufanya kazi. Kazi ni utu. Kazi ndio msingi wa MAENDELEO na kazi ni uhai. Taifa lolote lenye maendeleo lina watu wanaofanya kazi kwa bidii. Mpaka kufikia mwaka 1961 mataifa ya Tanzania na China yalikuwa sawa kiuchumi, lakini kushindwa kuwajibika na kufanya kazi ipasavyo imekuwa ni sababu kubwa kwa Taifa letu kubaki kuwa nyuma kiuchumi.
Lazima tupanue wigo wa fikra, tusifungwe na maeneo ya makuzi yetu pekee. Mwaka uliopita Serikali ilifanikiwa kupata soko la zao la dengu nchini India na Mihogo nchini China. Upo uwezekano mkubwa kwa wakulima wengi wa mazao haya kushindwa kunufaika na fursa hii katika kujiingizia kipato chenye faida kwa sababu tu ya ufinyu wa exposure na mtandao mkubwa wa watu. Lazima tukubali kubadilika ili kuendana na dunia ya sasa iliyogeuka kuwa kijiji. Tuwekeze muda mwingi kutambua mambo yanayofanywa duniani kwenye field za kazi zetu pindi tunapokuwa kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii.
Mwl Nyerere aliwahi kusema naweza kukujengea nyumba lakini siwezi kukufanya ujivunie au ujiamini kuwa wewe ni sawa na mwingine. Hiyo inafanywa na wewe mwenyewe. Tafsiri yake ni nini? kumpambanua mwanadamu hakutokani na namna mtu mwingine anavyoweza kumsimamia isipokuwa ni jinsi anavyotoa mchango wake kwenye jamii, namna anavyoweza kuzalisha uchumi wake mwenyewe na namna anavyoweza kuwa msaada kwa wengine kifikra, mtazamo na nyanja zingine za kimaisha.
Lazima tuwe tayari kunufaika na umeme unaosambazwa vijijini kwa kuzalisha bidhaa nyingi, bora na za uhakika kupitia kilimo cha umwagiliaji (drip irrigation), Green House n.k. Lazima tuwe tayari kusafirisha bidhaa na malighafi zetu kwenye masoko makubwa kupitia njia za usafirishaji kama Reli ya kati (Standard Gauge) na Meli zinazoboreshwa ili kujipatia pesa za kutosha kuwawezesha watoto wetu kupata elimu zitakazowakomboa kifikra na mitazamo kwenye maisha yao. Lazima tuwe tayari kubuni vivutio mbalimbali vitakavyotoa hamasa kwa watalii wengi watakaoongezeka kutokana na kuimarishwa kwa usafiri wa anga (kuongezeka kwa ndege). Lazima tuwe tayari kubuni fursa zitakazopatikana kwenye viwanda vinavyoanzishwa kuliko kutegemea kuajiriwa humo. Lazima tuwe tayari kuzalisha pesa zitakazotuwezesha kustarehe na kuwa na ustawi wa maisha bora yenye amani, utulivu na furaha na upendo.
Kuendelea ni pamoja na kujitegemea kifikra. Lazima tuwe tayari kuwajibika kwa moyo wa dhati ili kuweza KUJIENDELEZA SISI WENYEWE NA HATIMAE TAIFA ZIMA.
0 comments:
Post a Comment