Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa
kifo cha Msanii wa muziki wa taarab Bi. Shakila Said kilichotokea ghafla
nyumbani kwao Mbagala jijini Dar es Salaam jana Ijumaa ya tarehe
19/08/2016.
Shakila
ni msanii na mdau wa muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini. Amekuwa na
mchango mkubwa katika kukuza muziki wa taarab nchini hasa katika kubuni
kazi za Sanaa za muziki mbalimbali ambazo zilikuja kupata umaarufu
mkubwa. Moja ya kazi alizobuni na kupata umaarufu mkubwa ni pamoja na
'Macho yanacheka' na 'kifo cha mahaba'.
Mchango
wake katika muziki wa taarab hasa katika kubuni na kutunga nyimbo zenye
ubora, ujumbe na maadili kwa jamii hautasahaulika kamwe. Ni mwanamuziki
aliyeacha misingi katika sekta ya muziki na alijitolea kwa kiasi
kikubwa katika kuufikisha muziki wa taarab mahali ulipo leo.
Baraza,
wasanii na wadau wote wa Sanaa hatuna budi kuendelea kuenzi mema yote
aliyotuachia marehemu Shakila hasa katika kupenda kujitolea muda mwingi
katika kukuza muziki wa taarab na sekta ya muziki kwa ujumla.
Baraza
linatoa pole kwa ndugu wa marehemu, shirikisho la muziki, wasanii na
wadau wote wa Sanaa katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa
wetu.
Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Amen
0 comments:
Post a Comment