Dkt.Ama Kasangala kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, akizungumza na Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani Simiyu. Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) na Dkt.Ama Kasangala kutoka Wizara ya Afya wakizungumza jambo katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani humo Baadhi ya Watendaji Kata, Mitaa na Vijiji kutoka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani humo. Baadhi ya Watendaji Kata, Mitaa na Vijiji kutoka kwa Halmashauri ya Mji Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(wa tano
kulia) akiwa katika picha ya pamoja na
Baadhi ya Watendaji Kata, Mitaa na Vijiji kutoka kwa Halmashauri ya
Wilaya ya Bariadi.
Na
Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema iwapo Mpango wa Huduma ya Afya ngazi
ya Jamii utatumika vizuri utasaidia kuokoa Afya na maisha ya wananchi wengi
Mkoani humo.
Mtaka
ameyasema hayo katika kikao kilicho wahusisha Viongozi ngazi ya Mkoa,Wilaya, watendaji
wa Kata, Mitaa na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya Bariadi, Itilima na Mji wa
Bariadi, ambacho kililenga kutoa elimu kuhusu utekelezaji wa mpango wa huduma
ya Afya ngazi ya Jamii mkoani humo.
Mtaka amesema mwamko wa kupata huduma za afya katika
vituo vya kutolea huduma za afya kwa wananchi katika maeneo mengi mkoani
humo uko chini, hivyo mpango huu wa
kutoa huduma ngazi ya kaya utasaidia kuhamasisha wananchi kutafuta huduma za
afya katika vituo hivyo badala ya kutegemea tiba za kienyeji.
“Tukitumia huduma hii ya Afya Majumbani vizuri
itasaidia sana, tukifika mahali ambapo jamii yetu itapata mwamko wa kupata
matibabu katika vituo stahiki vya afya tutakua tumeokoa jamii yetu, kwa sababu bado wapo wanaoamini kupata
matibabu katika tiba za kienyeji; tungehitaji wananchi wetu huduma ya kwanza
kwenye afya iwe vituo vyetu kutolea huduma za afya na siyo tiba mbadala”
amesema Mtaka.
“........kwa sisi ambao tunatengeneza Mkoa wetu
katika Uchumi, Uchumi ni Afya wananchi hawawezi kufanya kazi wakajenga uchumi
kama hawatakuwa na afya njema” alisisitiza.
Aidha, Mtaka amewataka Watendaji wa Kata, Mitaa na
Vijiji kufanya utambulisho wa kutosha wa wahudumu wa afya ya Msingi ngazi ya
jamii watakaokuwa wakitoa huduma kwa wananchi katika maeneo yao ili wataalam
hao wasije wakapata madhara yoyote wakati wakitekeleza majukumu yao.
Mkuu huyo wa Mkoa pia amewataka wananchi kuachana na
taratibu za kimila zinazoathiri utendaji wa watumishi wa Umma ikiwemo kutumia
mahakama za kimila (dagashida) na akawataka viongozi hao kuwasaidia wananchi
kubadilika ili wahudumu wa afya ngazi ya Jamii watakaopelekwa katika maeneo
yote ya mkoa huo watekeleze majukumu yao bila vikwazo vyovyote.
Wakati huo huo Mtaka ameomba Shirika lisilo la
Kiserikali la AMREF lisaidie katika kuajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii
walipewa mafunzo, ili wasaidie kutoa huduma na kupunguza changamoto ya upungufu
wa watoa huduma wakati Serikali ikiendelea kushughulikia suala hilo.
Vile vile ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa afya
ikiwemo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
kushughulikia suala la upatikanaji wa vifaa ili watoa huduma ngazi ya jamii
watakapowafikia wananchi waweze kutoa huduma stahiki kwa wakati.
Kwa upande
wake Afisa wa Mpango wa Huduma ya Afya ngazi ya Jamii kutoka Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt.Ama Kasangala amesema Wizara
imetengeneza miongozo ya kuwafundisha wahudumu hao wanapokuwa kazini ili
waimarike na kutoa huduma nzuri.
Naye Kaimu Mratibu wa Mpango wa Huduma ya Afya Ngazi
ya Jamii, Dkt. Bahame Ntelemko amesema mpango umelenga kuwatumia wahudumu wa
Afya Ngazi ya Jamii kusaidia kuboresha huduma za afya hususani katika huduma za
mama wajawazito na uzazi kwa ujumla.
Dkt. Ntelemko amesema kwa mwaka 2016 wanawake
takribani 45 walipoteza maisha kutokana na masuala ya uzazi ambapo vifo vingi
vinatokana na ukosefu wa elimu ikiwemo kutojua umuhimu wa kuwahi katika vituo
vya kutolea huduma, ambapo amesema uwepo wa huduma katika kaya utasaidia
kupunguza idadi ya vifo hivyo.
Mafunzo yanayofanywa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa
kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la AMREF, kuhusu utekelezaji wa
Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoa wa Simiyu, yameshawafikia
Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji zaidi ya 350.
0 comments:
Post a Comment