METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, May 16, 2017

JPM avunja CDA, wasomi waunga mkono

 Rais Magufuli

Imeandikwa na Joseph Sabinus
 
WATANZANIA wa kada mbalimbali wakiwamo wasomi wamepongeza uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuvunja Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) huku wakimtajia taasisi nyingine zinazostahili kuvunjwa kwa vile nazo hazina tija kwa taifa.

Jana Rais Magufuli aliivunja rasmi CDA na kuagiza mali na shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na CDA zihamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji wa huduma kwa wananchi. Hatua ya kunvuja CDA, ilifanyika baada ya Rais kutia saini hati ya Amri ya Rais ya kuivunja Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam mbele ya viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri kutoka wizara mbalimbali. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, Rais aliagiza hati zote za kumiliki ardhi zilizokuwa zikitolewa na CDA kwa ukomo wa umiliki wa miaka 33, zibadilishwe na kufikia ukomo wa umiliki wa miaka 99 kama ilivyo katika maeneo mengine nchini ili kuwavutia wawekezaji hasa wa viwanda.

Rais alisema wananchi wa Dodoma wamekuwa wakilalamikia suala hilo kwa muda mrefu na hatua hii ni utekelezaji wa moja ya ahadi zake wakati wa kampeni kuwa akiingia madarakani, atapambana kwa nguvu zote kuondoa kero za wananchi. “Wananchi wa Dodoma wamelalamikia tatizo hili kwa muda mrefu sana, hata nilipokuwa kwenye kampeni zangu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 walilalamika sana, sasa nimetekeleza niliyowaahidi, naamini kwa uamuzi huu malalamiko ya wananchi yatapata utatuzi na pia tutakuwa tumeondoa kikwazo cha umiliki wa muda mfupi wa ardhi uliosababisha wawekezaji kushindwa kujenga viwanda Dodoma,” taarifa imemnukuu Rais Magufuli. Ikaongeza, “Sasa majukumu yote yanahamishiwa Manispaa ya Dodoma, sitaki kuendelea kusikia visingizio, mkajipange mambo yaende vizuri.”

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walimwahidi Rais kusimamia kwa karibu mchakato wa kuhamisha majukumu ya CDA kwenda Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ikiwamo taarifa ya Ikulu, mkanganyiko huo ulikuwa ukisababishwa na mgongano kati ya vyombo hivyo viwili vya Serikali. “Rais Magufuli pia ameivunja Bodi ya CDA, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa CDA Mhandisi Paskasi Muragili atapangiwa kazi nyingine na ameagiza wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo wahamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na ofisi nyingine za Serikali kadiri inavyofaa,” ilisema taairfa ya Ikulu.

Wasomi mbalimbali wamepongeza hatua.Bana ataka ziangaliwe na nyingineAkizungumzia hatua hiyo ya Rais jana, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana aliipongeza Serikali akisema huo ni mwanzo mzuri wa Serikali kutumia vema rasilimali zake. Alishauri Serikali iziangalie pia taasisi nyingine zilizoundwa kwa mujibu wa sheria ili zenye majukumu yanayofanana na kuingiliana, zivunjwe.

“Wakati nampongeza Rais, nimuombe pia atumie Wizara inayohusika na utumishi kuona kama taasisi zote bado zina manufaa kwa nchi au ni mzigo unaoitafuna Serikali bure,” alisema. Alisema kwa maoni yake, bado zipo taasisi kama National Insitute for Product (NIP) na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima alizosema hazistahili kuendelea kuwapo kwa kuwa hakuna mchango zinazoutoa kwa manufaa ya taifa kiuchumi na kijamii zaidi ya kuwa mzigo kwa Serikali.

“Nadhani sasa ni muhimu Serikali pia ifanye ukaguzi ili kila taasisi ioneshe umuhimu wake na ioneshe dhahiri inafanya nini ili zile zisizo na tija zivunjwe na zenye majukumu yanayofanya na kuingiliana, ziunganishwe ili kuwe na ufanisi zaidi,” alisema Dk Bana. Alisema hakuna haja ya kuwa na mamlaka mbili zinazofanya kazi ileile. “Mbona Dar es Salaam, Tanga, Mwanza au Arusha na Mbeya ni majiji, lakini hayana mamlaka na badala yake zote zina halmashauri ya jiji,” alisema.

Akizungumzia utendaji wa CDA kabla ya kuvunjwa, msomi huyo alisema licha ya kuwepo, mji wa Dodoma ulikuwa hauna sura yoyote ya kuelekea kuwa makao makuu hadi Rais alipofanya mabadiliko chanya na kujenga Dodoma katika sura mpya. Dk Bashiru: Uamuzi huu uungwe mkono Kwa upande wake, Dk Bashiru Ally, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema uamuzi wa Rais Magufuli unapaswa kuungwa mkono kwa kuwa CDA ilikuwa imeshindwa kutimiza majukumu yake hususani katika mipango na matumizi ya ardhi.

Alisema uamuzi wa kuhamisha majukumu utawezesha wananchi kushiriki zaidi katika mipango na maendeleo ya ardhi. “Katika halmashauri kutakuwa na ushiriki wa watu katika kufanya maamuzi kuliko hali ilivyokuwa katika CDA ambayo haiwajibiki kwa wananchi,” alisema Dk Bashiru. Kessy wa EALA ataka matumizi bora ya ardhi Mbunge wa Afrika Mashariki (EALA), Ndelakindo Kessy, alisema sasa ni wakati kwa Watanzania kutumia vizuri ardhi na rasilimali zilizopo kuongeza pato la taifa. Mbunge huyo wa EALA kupitia chama cha NCCRMageuzi alisema unahitajika umakini zaidi katika umiliki na utumiaji wa rasilimali za nchi ikiwamo ardhi ili itumike kwa manufaa ya umma.

Dk Wetengere Kitojo (Chuo cha Diplomasia) Makamu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia (Mafunzo) kilichopo Kurasini Dar es Salaam, Dk Wetengere Kitojo, alisema uamuzi huu wa Rais ni hatua nzuri ya kutumia vizuri rasilimali zilizopo. “Hii ni awamu ya kasi katika kufanya kazi kwa tija. Awamu hii ya uongozi inataka kuona matokeo chanya... Watu wasifanye kazi kwa mazoea,” alisema. Kiini cha kuzaliwa CDA CDA ilianzishwa kwa Amri ya Rais Aprili 1, 1973 na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 230.

“Imevunjwa rasmi leo tarehe 15 Mei, 2017 kwa Amri ya Rais na kuchapishwa katika gazeti la Serikali,” alisema taarifa ya Ikulu. “Serikali ilipofikia uamuzi wa kuhamisha Makao Makuu ya nchi kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, ilibidi kuundwa Programu ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma ili ikidhi vigezo muhimu vya kuwa makao makuu ya nchi,” alisema Dk Kitojo. Kwa mujibu wa Sheria, majukumu ya CDA yalikuwa kutekeleza uamuzi wa Serikali wa kuhamishia Makao Makuu Dodoma, kuandaa mipango ya kuendeleza mji mkuu na kuiwasilisha kwa Rais ili aipitishe na kufuatia utekelezaji.

Jukumu lingine la CDAlilikuwa kushauri Serikali namna bora ya utekelezaji wa program ya kuhamia Dodoma, kutwaa na kumiliki ardhi na mali zisizohamishika kwa maelekeo ya Rais. Mengine yalikuwa kutoa huduma kwa idara na taasisi kadri zitakavyohitaji kuhusu machakato mzima wa kuhamia Dodoma, ujenzi wa miundombinu mbalimbali, upimaji wa viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali na ugawaji wa viwanja vya kila aina katika eneo la Manispaa ya Dodoma.

Mamlaka hiyo ilikuwa inawajibika katika uchaguzi wa sehemu za kujenga majengo ya aina mbalimbali, utoaji wa vibali kwa ramani za majengo na mipango mingine ya maendeleo, utoaji wa ruksa za kujenga na ukaguzi wa nyumba zinazojengwa pamoja na ukuzaji na uendelezaji wa misitu katika eneo la mji mkuu.

Chanzo: Habari leo
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com