METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, April 15, 2017

MAMIA WAJITOKEZA MAZISHI YA MZEE CHRISTIAN CHRISOSTOM

Mamia ya waombolezaji wamejitokeza katika Mazishi ya Marehemu Mzee Christian Chrisostom Kayombo yaliyofanyika Jana (April, 15, 2017) Mkoani Pwani.

Mzee Chrisostom  aliyezikwa jana Jumamosi Tarehe 15/04/2017 katika eneo maalumu lililotengwa na familia kwa ajili ya mazishi  nyumbani kwake Mtaa wa Kiluvya Kwa Komba, Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani alikuwa mcha Mungu katika kipindi chake chote cha Maisha yake na ameacha mke na watoto saba.

Mzee Chrisostom aliyezaliwa tarehe 12 Aprili, 1948 Mkoani Ruvuma, katika enzi za Uhai wake alikuwa Mwalimu aliyehudumu katika maeneo mbalimbali, baadae akawa Afisa Elimu Taaluma (W), Afisa Elimu Wilaya ya Sumbawanga, Afisa Elimu Wilaya ya Hanang-Manyara na Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora.

Akizungumza wakati wa ibada ya kumuombea marehemu ili apumzike kwa amani Peponi ikiwa ni muda mchache kabla ya Sala ya Buriani Father Maximilian Wambura kutoka Parokia ya Kiluvya Mkoani Pwani Alisema kuwa Mzee Chrisostom amefariki katika kipindi ambacho Wakristo kote Ulimwenguni wapo katika kipindi cha  kumbukizi ya Mateso ya Yesu Kristo yaliyopelekea kifo chake msalabani.

Padri Wambura Alisema kuwa Ndugu, Jamaa, Marafiki na Familia kwa ujumla wa Marehemu Mzee Chrisostom wanapaswa kumuombea mapumziko mema awapo kaburini kwani amekufa kifo kisichoacha shaka kwa wananchi wenzake kutokana na jinsi alivyokuwa anamcha Mungu katika kipindi cha Uhai wake.

Alisema kuwa wapo  wananchi karibu kote  Ulimwenguni ambao wanaishi kwa kiburi cha uzima lakini wamesahau kuwa Mungu humpatia  mwanadamu zawadi ya uzima ili ampende, amtumikie na hatimaye kifo chake.

"Nawasihi wananchi wenzangu kumtumikia Mungu kwa nguvu zote na kuacha kiburi cha uzima tulichonacho kwani hatujui Muda wala saa ambayo Mungu atatatuchukua" Alisema Padri Wambura

Akizungumza kwa niaba ya Watumishi wa Manispaa ya Ubungo na Mkoa wa Dar es salaam, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo Alisema kuwa katika Halmashauri hiyo ya Manispaa anayoiongoza msiba huo umewagusa kwa kiasi kikubwa kwani miongoni mwa mtumishi mwenzao ambaye ni Kaimu Mkuu wa Idara ya TEHAMA Manispaa ya Ubungo Bi Sophia Chrisostom Kayombo amempoteza  Baba yake Mzazi Mzee Christian Chrisostom Kayombo April 11, 2017 katika Hospitali ya Muhimbili Jijini Dar es salaam alipokuwa anapatiwa matibabu.

Mkurugenzi Kayombo ameisihi familia hiyo kuwa na umoja na mshikamo katika kipindi hiki kigumu ambapo ameiomba familia na wananchi kwa umoja wao kufanya maombi ya Mara kwa mara kwa ajili ya faraja sambamba na Sala za  kumuombea Marehemu.

Mzee Kayombo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Kisukari tangu Mwaka 1998 na badae matatizo ya Figo ugonjwa uliopelekea kifo chake kwani mpaka mauti inamkuta alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Aidha Mzee Kayombo alizidiwa Jumatatu ya Tarehe 3/4/2017 ambapo alipelekwa katika Hospitali ya Rabiansi-Tegeta ambapo Siku tatu baadae alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alipopatiwa matibabu kwa zaidi ya wiki moja.

Katika enzi za Uhai wake pia Mzee Christian Chrisostom Kayombo aliwahi kutibiwa katika Hospitali ya Tumbi Mkoani Pwani.

BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE

Imetolewa na Kitengo cha Uhusiano

Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo

Marehemu Mzee Christian Chrisostom Kayombo
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisaini kitabu cha wageni Mara baada ya kuwasili Msibani
Waombolezaji
Waombolezaji
Waombolezaji
Waombolezaji
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com