METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, January 1, 2018

DC RUANGWA MTAFUTIE JENGO AFISA MADINI AKAE HAPA - WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

*Asema ni gharama kutoka Nachingwea kila mara
*Asema migodi mingi iko Ruangwa kuliko Liwale, Nachingwea

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Joseph Mkirikiti atafute jengo haraka kwa ajili ya ofisi ya madini wilayani humo.

Ametoa agizo hilo jana mchana (Jumamosi, Desemba 30, 2017) baada ya kubaini kuwa Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Bw. Ogesa Charles Tale anaishi Nachingwea lakini anahudumia wilaya tatu za Ruangwa, Liwale na Nachingwea yenyewe.

Waziri Mkuu yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi katika wilaya hiyo. Alikuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namungo, wilayani Ruangwa mkoani Lindi baada ya kukagua migodi ya wachimbaji wadogo iliyopo kijijini hapo.

“Sisemi ahamie hapa kwa sababu ni nyumbani, hapana. Ni kwa sababu najua ofisi yake iko Nachingwea lakini shughuli nyingi za madini ziko Ruangwa kuliko Liwale na Nachingwea,” alisema.

“Haiwezekani uwe kule, halafu uwahudumie huku wananchi walio wengi. DC mpe ofisi akae hapa, apite maeneo mengi ya huku na kuwasikiliza wachimbaji wadogo ambao ni wengi zaidi. Kule mashimo ni moja moja, ataenda mara moja kwa wiki. Kuanzia sasa, atakuwa Ruangwa ili afanye kazi kwa karibu zaidi na kundi kubwa la wachimbaji wadogo,” alisema.

Mapema, kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alitembelea mgodi wa dhahabu wa Namungo na kukagua shughuli za uzalishaji pamoja na mitambo inayotumiwa kwenye uchenjuaji wa mchanga wa dhahabu.

Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Meneja Mitambo ya Uchenjuaji (Processing Plant) wa kampuni ya Gemini inayomiliki mgodi huo, Bw. Emmanuel James alisema kwa sasa wamesimamisha mitambo kwa sababu wanakabiliwa na tatizo la umeme mdogo licha ya kuwa wameweka umeme wa njia tatu.

“Umeme upo wa njia tatu lakini tatizo hautoshi, pia transfoma iliyopo ni ndogo na haihimili umeme wa mgodini,” alisema.

Alipoulizwa wametoa ajira kwa watu wangapi, Bw. James alijibu kuwa wametoa ajira zaidi ya 200, ambapo kati ya hizo, ajira 40 ni za moja kwa moja.

Naye Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Bw. Ogesa Tale alimweleza Waziri Mkuu kwamba kuna mashimo zaidi ya 120 yanayomilikiwa na wachimbaji wadogo katika eneo hilo  lakini mashimo 47 yanaendelea na uzalishaji na mengine 32 yalifungwa ama kwa sababu za kiusalama ama kwa kuwa yamekamilisha kazi yake na hayana faida tena.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya jimboni kwake kwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya upandaji miche bora na mipya milioni 10.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMAPILI, DESEMBA 31, 2017.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com