METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, April 6, 2017

MD KAYOMBO ATIBIWA KITUO CHA AFYA, ASIFU SEKTA YA AFYA INAVYOJITAHIDI KUBORESHA HUDUMA

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisubiri majibu mara baada ya kupima afya katika kituo cha Afya Kimara
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akikagua hali ya usafi wa mazingira katika Kituo cha Afya Kimara
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akikagua usafi wa vyoo katika Kituo cha Afya Kimara
Baadhi ya wagonjwa waliofika kutibiwa katika kituo cha Afya Kimara

Na Mathias Canal, Dar es salaam

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo ameeleza kufurahishwa na huduma zitolewazo na vituo mbalimbali vya afya nchini kwa jinsi ambavyo huduma zinazidi kuboreshwa mwaka hadi mwaka.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Mitandao wa www.wazo-huru.blogspot Mara baada ya kupatiwa huduma za matibabu katika Kituo cha Afya Kimara kilichopo katika Kata ya Kimara, Manispaa ya Ubungo.

MD Kayombo amesema kuwa amejisikia fahari kupatiwa huduma nzuri katika kituo hicho ambazo kwa kiasi kikubwa zinawafanya wagonjwa kuanza kupata ahueni kabla hata ya kuhudumiwa.

Alisema kuwa Sekta ya afya nchini imepiga hatua za kimaendeleo kwa kiasi chake katika miaka ya karibuni ambapo Moja ya hatua za kupongezwa kabisa ni kupungua kwa idadi ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka vifo 147 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 1999 hadi vifo 49 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2015, huku vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja vikipungua kutoka 99 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 1999 hadi vifo 35 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2015; na hivyo kuifanya Tanzania kuweza kufikia malengo ya maendeleo ya milenia ya mwaka 2015.

Pia alisema vifo vya akina mama wajawazito vilipungua kutoka vifo 529 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi vifo 398 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015; japokuwa malengo ya milenia ya mwaka 2015 hayakufikiwa katika kipengele hiki cha kupunguza vifo vya kinamama wajawazito. Tafiti pia zinaonyesha kuwa , idadi ya watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi imepungua kutoka asilimia 15% mwaka 1999 hadi asilimia 5.1 mwaka 2011/12 Umri wa wastani wa kuishi wa Mtanzania pia umeongezeka kutoka miaka 51 mwaka 2002 hadi miaka 61.8 mwaka 2015.

MD Kayombo ameeleza kuwa Pamoja na mafanikio hayo, bado kumekuwa na changamoto kadhaa zinazoikabili sekta ya afya katika nchi yetu ambapo Changamoto kubwa zaidi ni msongamano mkubwa wa wagonjwa hasa katika hospitali za rufaa za mikoa, za kanda na pia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

MD Kayombo alisema kuwa changamoto hii inachagizwa kwa kiasi kikubwa na huduma hafifu ambazo zimekuwazikipatikana katika vituo vya afya na zahanati; na hivyo kusababisha wananchi kutoamini au kushindwa kupata huduma ambazo wangeweza kuzipata katika zahanati na hivyo wengi kukimbilia katika hospitali za rufaa kwa matatizo ambayo yangeweza kutatuliwa na hospitali za ngazi za chini.

Ametolea mfano; Kati ya dawa 14 za msingi, ni dawa 7 tu ambazo zinaweza kupatikana katika asilimia 70 ya vituo ambavyo vinatoa huduma ya afya nchini.

Mfano mwingine ni upatikanaji mdogo wa vipimo vya msingi; ambapo ni vipimo vya malaria na VVU (Virusi Vya UKIMWI) tu, ndivyo vinapatikana kwa asilimia 90 ya vituo vinavyotoa huduma ya afya huku vipimo vingine vya msingi vikipatikana kwa asilimia chini ya 50 ya vituo vyote.

Tatizo lingine linalochangia msongamano wa wagonjwa ni upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta ya afya nchini; ambapo uwiano wa daktari kwa wagonjwa ni daktari mmoja kwa wagonjwa 75,000 wakati kulingana na miongozo ya kimataifa, uwiamo unaotakiwa ni daktari mmoja kwa wagonjwa 7,000.

"Ushirikishwaji mdogo wa wananchi katika kutatua changamoto za sekta ya afya pia ni tatizo kubwa, na hili linaonekana kuanzia katika ngazi ya vituo vya afya husika, hadi katika ngazi ya uongozi wa afya wa mkoa. Kwa mfano,ni asilimia 39 tu ya vituo vinavyofanya vikao vya utawala mara kwa mara hushirikisha jamii zinazowahudumia katika vikao hivyo, hivyo Manispaa ninayoiongoza ya Ubungo nimejipanga pamoja na watumishi wenzangu hususani katika sekta ya afya kuanza kuwashirikisha wananchi kutambua umuhimu wa huduma za afya na namna bora ya kuwa ni matibabu bora na imara". Alisema MD Kayombo

Hata hivyo Mkurugenzi huyo Alisema kuwa ili Kupambana na changamoto ya msongamano mkubwa wa wagonjwa, serikali imeweka dhabiti ambao utawezesha mfumo wa rufaa uweze kufanya kazi vizuri ili kuweza kuchuja wagonjwa ambao wanaweza kuhudumiwa katika ngazi ya zahanati/vituo vya afya ili kupunguza msongamano katika hospitali za wilaya na hospitali ya mkoa na ya kanda.

"Hatua ya kwanza ambayo imeanza kufanywa na serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli katika kulitekeleza hili ni kuboresha huduma za afya zinazotolewa katika ngazi hizi ambapo itapelekea wagonjwa kutokuwa na sababu ya kuruka ngazi hii ya huduma" Alisema MD Kayombo John L.

Sambamba na hayo yaliyosemwa na Mkurugenzi Kayombo pia serikali inatakiwa kuongeza nguvu kazi katika sekta ya afya ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa watumishi katika hospitali zake nchini.

Serikali inapaswa kuongeza idadi ya wauguzi, madaktari, na wafanyakazi wengine wa afya ili kwenda sambamba na ongezeko la watu na kuboresha huduma za afya zinazotolewa na taasisi za serikali.

Pia, serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya inatakiwa kubuni mfumo na mikakati ambayo itawezesha wafanyakazi wa afya kutoa huduma katika vituo vya vijijini badala ya kukimbilia mijini.

Mikakati hiyo ni kama vile kuwa na mfumo wa kuwapatia posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu, na motisha mbalimbali kama mafunzo ya ziada kwa wafanyakazi hawa.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com