METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, April 24, 2017

DC UBUNGO ASULUHISHA MGOGORO WA ARDHI GOBA



Mkuu wa wilaya ya Ubungo Mh. Kisare Matiku Makori (mwenye miwani).
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mh. Kisare Matiku Makori amesuluhisha mgogoro wa ardhi uliokuwepo kati ya wakazi wa Mtaa wa Kulangwa na Tegeta A Kata ya Goba kwa kuamuru kusimama kwa mpango wa upimaji wa maeneo yenye mgogoro uliokuwa unafanywa na familia ya Seif Ngane na badala yake kuwapatia maeneo yao wakazi waliopewa maeneo hayo na serikali ya kijiji katika mitaa ya Kulangwa na Tegeta A Kata ya Goba.

Agizo hilo amelitoa leo wakati wa mkutano kati ya pande zote zilizokuwa na mgogoro wa ardhi katika eneo hilo.

Mgogoro huo wa ardhi unaohusisha familia ya Seif Ngane na wananchi waliopewa maeneo na serikali ya kijiji kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa wakati huo ndugu Yusuph Makamba unahusisha umiliki wa eneo linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa ekari 99.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Mkuu wa Wilaya alisema;- "Wote waliopewa maeneo na serikali ya kijiji na wana ushahidi wa maandishi wapeleke vielelezo vyao kwenye ofisi za Serikali ya Mtaa na Kata ili kuhakiki vielelezo hivyo kama sehemu ya mchakato wa kupimiwa maeneo hayo na kupatiwa Hati ya umiliki wa eneo husika" alisema .

Aidha, Mhe. Kisare ameagiza wale wote wanaoendelea kutumia maeneo ya ardhi ambayo Seif Ngane alishinda kesi dhidi yao Mahakamani wasitishe kuyatumia mara moja na wasiyaendeleze maeneo hayo.
Kuhusu eneo ambalo Seif Ngane alimuuzia Ndg. Octavian William Temu, Mhe Kisare ameelekeza pande mbili zinazohusika kukutana ofisini kwake Alhamisi wiki ijayo kwa sababu pande zote mbili zimeshindwa kuthibitisha kwa vielelezo kiasi cha ardhi walichouziana.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi waliokuwa na mgogoro huo Mwenyekiti wa kikundi hicho Ndg. Venance Mhingwa alimshukuru sana Mkuu wa Wilaya kwa busara aliyotumia na hatimaye kutoa maamuzi ya haki kwa pande zote zilizokuwa na mgogoro huo.

Wananchi wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Wilaya ya Ubungo (hayupo pichani).
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com