Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wadau waliohudhuria
mkutano wa siku mbili wa Usalama barabarani katika ukumbi wa Mwl. Julius
Nyerere jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara
nchini (RFB) Bw. Joseph Haule akitoa taarifa ya udhibiti wa ajali za
barabarani kwenye mkutano wa wadau wa usalama barabarani uliofanyika
jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akiongea na Naibu Waziri wa
Ujenzi na Mawasiliano wa Namibia Mhe. Sankwasa James Sankwasa wakati wa
mkutano wa siku mbili wa kutathmini usalama barabarani, Jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa
Chama cha Kimataifa kinachoshughulika na masuala ya barabara Dkt. Kiran
Kapila wakati wa mkutano wa siku mbili wa kutathmini usalama
barabarani, Jijini Dar es salaam.
Mmoja wa wanafunzi aliyeshinda tuzo ya
uchoraji wa picha ya usalama barabarani Veronica Shirima akitoa maelezo
kwa wadau wa usalama barabarani, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Wanne kulia) akiwa katika picha ya
pamoja na wadau wa Usalama barabarani mara baada ya kufungua mkutano
huo, Jijini Dar es salaam.
Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
WADAU WA BARABARA WATAKIWA KUWEKA MIKAKATI YA KUDHIBITI AJALI NCHINI
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wadau wa usafirishaji
kuweka mikakati dhabiti ya kupunguza ajali za barabarani nchini ili
kuokoa maisha ya watanzania wanaofariki dunia kila mwaka kutokana na
ajali hizo.
Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo
alipofungua mkutano maalumu wa kanda wa kujadili na kutathmini
changamoto za usalama barabarani na jinsi ya kuzikabili unaofanyika
jijini Dar es salaam.
Profesa Mbarawa amesema kuwa ajali za
barabarani zimekuwa zikikatisha maisha ya watanzania wengi kila mwaka
ambao wengi wao ni vijana na nguvu kazi ya taifa hivyo ni jukumu la
wadau kubadilisha hali ya usalama barabarani.
“Kama tukijifunza vizuri na kuyafanyia
kazi mafunzo haya tunaweza kubadili hali ya usalama barabarani kwani
inaumiza kuona vifo vya watu wengi vinavyotokana na ajali za barabarani
hivyo ni wakati wa Jeshi la Polisi, na Mamlaka ya Usafiri wa nchi Kavu
na Majini SUMATRA kushirikiana kukomesha ajali hizi”. Amesisitiza
Profesa Mbarawa.
Ameongeza kuwa Serikali itatoa
kipaumbele kwa yale yatakayojadiliwa na kuamuliwa katika mkutano huo ili
kuongeza kasi ya udhibiti wa ajali za barabarani hapa nchini na
kupunguza idadi ya ajali zinazoepukika.
Naye Mwenyekiti wa Mfuko wa Barabara
nchini (RFB), Bw. Joseph Haule amesema kuwa Bodi hiyo inashirikiana na
taasisi nyingine katika kuhakikisha ubora wa miundombinu ya barabara
inakuwa salama na kupitika wakati wote.
Kwa upande wake Kamanda wa kikosi cha
usalama barabarani hapa nchini Mohamed Mpinga amesema kikosi cha usalama
barabarani kitaendelea kuhakikisha kuwa ajali za barabara
zinadhibitiwa.
“Suala la ajali za barabarani ni jukumu
letu sote kwa pamoja hivyo tukiungana kwa pamoja na kushirikiana
tutaweza kupunguza ajali hizi kwa kiwango kikubwa”. Amesema Kamanda
Mpinga.
Mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo
jijini Dar es salaam umewakutanisha wadaau mbalimbali wa kimataifa wa
masuala ya ujenzi na usimamizi wa usalama wa watu na mali wawapo
barabarani .
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
0 comments:
Post a Comment