SMZ kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itahakikisha kwamba wanawake wanapata fursa zote muhimu ambazo zitawawezesha kupata maendeleo katika sekta ya elimu na kushika nafasi za juu za uongozi.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma wakati akizungumza na wanaharakati katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, iliyofanyika Kijangwani, mjini Unguja.
Alisema mafanikio makubwa yameanza kupatikana kwa upande wa sekta ya elimu ambapo wanawake asilimia 63 wanaojiunga katika vyuo vikuu nchini ni wanawake.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inaweka mazingira mazuri zaidi ambayo yatawafanya wanawake kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika elimu kwa ajili ya kushika nafasi za juu za uongozi.
Aidha aliwataka wazazi kuhakikisha kwamba wanatoa fursa zaidi kwa wanawake kupata elimu huku wakipinga ndoa za utotoni ambazo ni moja ya kikwazo kikubwa kwa wanawake kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar, Mzuri Issa aliitaka wizara ya elimu kuifanyia marekebisho Sheria ya Elimu namba 6 ya mwaka 1982 ambayo inatoa nafasi kubwa kwa mzazi kumuozesha mtoto wa kike wakati akiwa katika elimu ya lazima.
Alisema ipo hatari kubwa kushuka kwa maendeleo ya mtoto wa kike katika sekta ya elimu kwa sababu imebainika kwamba hivi sasa lipo wimbi kubwa la wazazi kuwaozesha watoto wa kike wakiwa katika elimu ya lazima.
Kwa mfano, mzazi atakayebainika kumuozesha mtoto wa kike wakati akiwa katika elimu ya lazima atatozwa faini ya Sh 1,500 au 3,000 kiwango cha fedha ambacho ni kidogo sana huku mzazi akipokea kiwango kikubwa cha fedha za mahari.
Mwenyekiti wa asasi za kiraia Zanzibar, Asha Aboud alisema mafanikio makubwa yamepatikana hivi sasa kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo wanawake wengi kushika nafasi za juu za uongozi katika ngazi za maamuzi.
Wanawake wa Zanzibar wanaadhimisha siku ya wanawake duniani huku wakikabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kuongezeka kwa kasi ya vitendo vya udhalilihaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji.
0 comments:
Post a Comment