Wafugaji wenye silaha wavamia msafara wa Maghembe
MSAFARA wa wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, umevamiwa na kuzuiwa barabarani na kundi la wananchi kutoka jamii ya wamasai, wakiwa na silaha za jadi, katika eneo la Arash, tarafa ya Loliondo, wakitaka wasikilizwe kero zao.
Wanaume wa jamii hiyo waliohusika katika tukio hilo, waliwatanguliza wanawake na watoto waliolala barabarani ili kuzuia magari yasipite, wao (wanaume) wakiwa na fimbo, mikuki na mapanga walifuata nyuma wakiamrisha magari yote ya wabunge, likiwemo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, yasimame.
Hata hivyo, askari polisi pamoja na maofisa usalama waliokuwa wakiongoza msafara huo uliokuwa ukitokea Wasso kuelekea Olduvai, walifanikiwa kuyachepushia baadhi ya magari, likiwemo la waziri, yapite upande mwingine katika pori hilo, ingawa baadhi ya magari yalilazimika kusimama baada ya kuzidiwa nguvu.
“Ni jambo la ajabu watu kuvamia msafara wa viongozi wakiwa na silaha, na si hivyo tu, bali pia kubainika kuwa walitumwa na makundi fulani ya watu kuzua vurugu,” alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Atashasta Nditiye. Kwa mujibu wa Nditiye, kamati ya Bunge ilikwenda Loliondo, kufanya shughuli za Bunge; “Tumekuja kujionea wenyewe mazingira ya eneo la mgogoro lilivyo kabla ya kurudi kwenda kuijadili ripoti ya Loliondo iliyowasilishwa kwa waziri mkuu wiki iliyopita,” alisema Mwenyekiti huyo wa Kamati.
“Sisi hatukuja kufanya mikutano ya hadhara, hiyo sio kazi yetu, lakini tumekutana na viongozi wa vijiji na wa wananchi, wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali na wawekezaji,” alisema Nditiye na kuongeza kuwa sasa kamati nzima yenye watu 28 waliokwenda Loliondo wamepata picha halisi.
Nditiye aliongeza kuwa baada ya vikao vya Loliondo, kamati itakutana pia na viongozi wa baraza la wafugaji la Wilaya ya Ngorongoro. Akizungumzia vurugu za Arash, Waziri Maghembe amewaomba wakazi wa wilaya ya Ngorongoro pamoja na watanzania kwa ujumla waiache kamati ya Bunge ifanye kazi yake.
“Bunge ni mhimili wa dola, una mamlaka kamili na njia zake za kufanya kazi zake; kamati hii iko huru na haitakiwi kufuata matakwa ya watu wachache, hususan wale wanaotumia mitandao kuichafua serikali na vyombo vyake,” alisema Profesa Maghembe.
0 comments:
Post a Comment