METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, March 14, 2017

Kauli ya mwisho ya Sophia Simba

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM, Sophia Simba na wanachama wengine wamefukuzwa uanachama huku wengine wakipewa onyo kali.

Usaliti ndilo kosa lililowagharimu wanasiasa hawa akiwamo Simba ambaye ni mkongwe ndani ya chama hicho tawala. Siku chache kabla ya uamuzi huo kufanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Simba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), alitangaza kuwa hatagombea tena wadhifa huo.

Maswali yanayokuja ni je, alijua kinachokuja mbele yake kuwa ni kufukuzwa chama? Je, ataendelea na siasa kupitia vyama vingine? Alichokizungumza siku chache kabla ya kufukuzwa, kinaweza kutoa majibu ya maswali haya.

Mkutano wake na wana UWT, wilaya wa Temeke, mkoani Dar es Salaam uliojielekeza kwenye kuzungumza Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa Machi 8, ilikuwa ni miongoni mwa majukwaa ambayo mwanasiasa huyu alipata fursa ya kuwaaga wanachama.

Simba ambaye ifikapo Julai 27 mwaka huu, atatimiza umri wa miaka 67, aliwaeleza kuwa anaona vipindi viwili alivyotumika katika umoja huo vinatosha na kwamba sasa anawaachia wengine. “Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi alizonijaalia kwani nimekuwa mbunge kwa miaka 22 sasa na katika miaka hiyo nilibahatika kuteuliwa na kuwa waziri kwa kipindi cha miaka 10,” alikaririwa Simba.

Tamko la kutangaza kutogombea tena uenyekiti wa UWT lilikuwa linazingatia kwamba, mwaka huu utafanyika uchaguzi ndani ya CCM pamoja na jumuiya zake zote. Aliwahamasisha wanawake wote wanaojitambua kuwa wanaweza uongozi, hususan wana UWT wa kutoka kona zote za nchini, kujitokeza kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali.

“Naomba tusiogopane, nafasi zi wazi na hakuna nafasi ya mtu. Kumbukeni ule usemi wetu ‘Wanawake Jeshi Kubwa – Ushindi ni Lazima’. Sisi wanawake tupo wengi tupigiane kura tutashinda. Wanawake wa CCM tunaweza na chama chetu kinatambua hivyo,” anasema.

Waziri huyo wa zamani aliweka wazi alianzia katika nafasi ya ukatibu wa tawi la kazini NDC, kisha akawa mwenyekiti wa UWT wa kata ya Upanga Magharibi, Ilala kabla ya kupata udiwani. Wakati huo huo alishinda nafasi ya kuwa mbunge wa viti maalumu mwaka 1995.

Akaeleza anavyojivunia kuwa mwanachama mwaminifu wa CCM katika maisha yake yote. “Mimi nimekulia na kulelewa na wazazi wangu na viongozi wangu wana TANU na CCM katika maisha yangu yote,” alisema.

Alikiri kuwa uchaguzi ndani ya CCM mwaka huu, utazingatia azma ya mikakati madhubuti iliyokwishatangazwa na viongozi wa juu wa chama, hususani mwenyekiti Rais John Magufuli. Alikiri pia kuwa azma iliyopo, ni kukijenga chama upya na hatimaye Tanzania mpya.

Huku pengine akiwa hajui ambacho kingelimkumba, mwanasiasa huyu alimuomba Mungu amjaze hekima aendelee kuwa mwana CCM mwaminifu katika maisha yake yote yaliyobaki. “Hiki ndicho chama ninachokijua na mimi ni mwana CCM wa asili nisiyeyumba na namuomba Mwenyezi Mungu anijaze hekima ya kuendelea kuwa mwanaCCM mwaminifu katika maisha yangu yote yaliyobaki,” alisema.

Katika kauli zake kwenye mkutano huo, inaonesha Simba alikuwa na imani kuwa ataachia wadhifa huo baadaye mwaka huu baada ya kuitumikia jumuiya hiyo kwa mapenzi, utii, uaminifu na uadilifu mkubwa kwa kipindi cha kutosha. Kauli hii inadhihirisha hakujua kama Machi 11, 2017 ingekuwa ndiyo mwisho wa kushikilia wadhifa huo.

Akaeleza kuwa hana shaka iwapo wanawake wengine wenye uwezo wa kuendeleza harakati za kuwaunganisha wanawake na kuhakikisha chama kinaendelea kushika dola. “Likiwemo jukumu kubwa la kisiasa na la kipaumbele ndani ya jumuiya ya UWT. Ambalo ni kuhakikisha kuwa Chama chetu cha Mapinduzi kinaendelea kushika dola,” alisema mwenyekiti huyo.

Alisisitiza kuwa kwa hiari yake ameamua kutogombea nafasi hiyo ya uenyekiti wa UWT katika uchaguzi ujao kwa kuwa azma yake tangu aliposhika wadhifa, ilikuwa ni kutumikia vipindi viwili.
“Nitakabidhi kijiti hiki kwa uongozi utakaochaguliwa kama ilivyo mila na desturi za chama chetu. Sina shaka kabisa wapo wanawake wengine wenye uwezo wa kuendeleza harakati za kuwaunganisha wanawake katika kupigania maslahi na haki zao za msingi, haki na ustawi wa watoto na masuala ya jamii kwa ujumla.

Simba akawaeleza wana UWT Temeke kuwa ameamua kutangaza mapema azma ya kutogombea ili kuwaweka huru na kuwapa muda wa kujipanga vizuri wale wote wanaokusudia kugombea nafasi hiyo kubwa ndani ya jumuiya yao. Pia akasema ameamua kutangaza mapema ikiwa ni njia mojawapo ya kutoa majibu kwa wale walioku wa wakimuuliza na kumhamasisha aendelee kugombea.

Iwe, ama alijua au hakujua kama ungefanyika uamuzi mgumu ndani ya chama juu yake, kinachobaki ni kwamba, Sophia Simba si mwana CCM tena. Azma ya kujenga chama upya imemkumba na yeye. NEC imekomesha ndoto zake za kuendelea kuwa mwanaCCM mwaminifu katika maisha yake yote yaliyobaki kama alivyosema.

Sasa hatasubiri tena baadaye kuachia wadhifa huu wa UWT na kushiriki uchaguzi, bali anaachia mara moja kwa kuwa siyo mwanachama tena na ndoto za kuona CCM kinaendelea kushika dola kama ambavyo alikaririwa akisema hatasaidia kuzikamilisha.

Ni dhahiri Simba aliutumia mkutano huo wa Temeke kuwaaga wana UWT na chama kwa ujumla, ama kwa kufahamu au kwa kutofahamu. Katibu wa UWT wilaya ya Temeke, Zahra Mohamed alisema amelelewa naye (Simba). Akasema ‘kung’atuka’ kwake (sasa kufukuzwa kwake ndani ya chama) kunampa masikitiko.

“Lakini hakuna jinsi, huo ndio utaratibu wa chama kuongoza miaka 10,” alisema. Akaendelea kumwelezea: “Suala la vikoba, mikopo ya benki na miradi mbalimbali mwenyekiti wetu ndiye aliyekuwa anatuhimiza. Kulikuwa na jengo letu lile la Zain huyu mama alilirudisha kwani lilikuwa linapotea na hivi sasa pesa inaingia.

Vile vile mwenyekiti wetu huyo amekuwa akijitoa sana kwa akina mama kwa misaada mbalimbali,” anamwelezea Simba. Kwa mujibu wa wasifu kutoka katika tovuti ya Bunge, Simba ana Shahada ya Uzamivu ya Sayansi ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii aliyoipata mwaka 2007 katika Chuo Kikuu cha New Hempshire.

Aidha, mwaka 1997 alipata Stashahada ya Uzamili ya Sheria za wanawake kutoka Chuo Kikuu cha Zimbabwe. Mwaka 1992 alitunukiwa Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Baada ya kutumika katika taasisi mbalimbali ikiwamo MEIDA (1979-1995), Tantrust Group of Companies (1977-1978) na pia Shirika la Maendeleo – NDC (1971-1977), mwaka 1995 aliingia bungeni kwa mara ya kwanza na hadi anafukuzwa uanachama, alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com