METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 15, 2017

‘Acheni kutumia majivu, mkaa kuosha vinywa’

DAKTARI David Mapunda kutoka Chama cha Madaktari wa Vinywa na Meno Tanzania (TDA), amewashauri baadhi ya wananchi wenye kutumia majivu, mkaa na sabuni kuoshea vinywa vyao na meno, waache mara moja kwani vinaleta madhara ya kuharibu mishipa ya fahamu.

Daktari huyo alisema hayo mjini Shinyanga wakati wa kutoa ushauri na tiba katika kituo jumuishi, kinacholea watoto wenye ulemavu mbalimbali kilichopo Buhangija, ikiwa matibabu hayo yalikuwa yamelenga kwa watoto wenye ualbino wenye kuishi kwenye kituo hicho.

Dk Mapunda alisema matumizi ya vitu hivyo, siyo sahihi kwa afya ya kinywa na madhara yake ni kuharibu meno na mishipa ya fahamu, sababu mikaa na majivu huwa sio laini, inaweza kuleta madonda ya mchubuko katika kinywa, jambo ambalo pia ni hatari.

Alisema wapo baadhi ya wananchi hasa wa vijijini, hupenda kusukutua au kuosha kinywa hususani meno kwa majivu, sabuni na mkaa, wakiamini wapo salama.

“Baadhi ya wamekuwa wakitumia majivu, sabuni na mkaa kusafisha meno kwa imani kuwa vitu hivi hutumika kuondoa uchafu, bila ya kufahamu ni hatari kwa afya ya vinywa vyao elimu na ushauri tunaendelea kuvitoa kila mahali,” alisema Dk Mapunda.

Aidha, alisema dawa za meno zilizothibitishwa kitaalamu, ndio sahihi kwa matumizi ya kusafisha kinywa na kinga ya meno, sababu huwa zina madini ya florine ambayo humfanya mtu kuwa salama.
Rais wa Madaktari wa Chama cha Kinywa na Meno Tanzania, Dk Lorna Carneiro akizungumza wakati wakitoa huduma ya kutibu meno kwa watoto albino mjini Shinyanga, alisema watajitahidi kutoa elimu ya afya ya kinywa maeneo yote ya vijijini.

Pia Dk Carneiro alitoa mwito kwa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga, kuendeleza huduma hiyo ya kutibu afya ya kinywa na meno kwa watoto hao hasa waliokuwa wamelengwa wenye ualbino ikiwa mkataba wao wa miaka mitatu umefika kikomo.

Mlezi Mkuu wa Kituo hicho jumuishi, Suleiman Kipanya alikipongeza chama hicho kwa kutoa huduma ya kinywa na meno ndani ya miaka mitatu mfululizo kwa watoto hao na kuwafanya meno yao kuendelea kuwa imara.

Credit:Habari Leo
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com